Marekani yajiondoa katika mpango wa nyuklia wa Iran

Theresa May (katikati), Angela Merkel (kulia) na Emmanuel Macron kushoto

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uingereza, Ufaransa na UJerumani ilitoa taarifa ya pamoja wakiunga mkono mkataba huo

Viongozi wa mataifa ya magharibi wanasema kuwa wataendelea kuuunga mkono makubaliano ya kinyuklia ya Iran muda mfupi baada ya Marekani kutangaza kuwa inajiondoa katika makubaliano hayo.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinasema kuwa watafanya kazi pamoja na matiafa yote yaliosalia katika mkataba huo huku ikiitaka Marekani kutovuruga utekelezwaji wake.

Mataifa mengine yalioweka mkataba huo wa 2015- Urusi na China pia yamesema yataendelea kuunga mkono makubaliano hayo.

Iran imesema kuwa inafanya kazi kunusuru makubaliano hayo bila ya ushirikiano wa Marekani.

''Mataifa yetu yataendelea kuunga mkono makubaliano hayo na yatafanya kazi na mataifa yanaoendelea kuunga mkono mkataba huo'', Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zilisema katika taarifa ya pamoja.

Siku ya Jumanne rais wa Iran Hassan Rouhani alisema: "Nimeagiza wizara ya maswala ya kigeni kujadiliana na mataifa ya Ulaya ,China na Urusi katika majuma yajayo''.

''Iwapo tutaafikia malengo ya makubaliano haya kwa ushirikikiano wa wanachama wengine basi makubaliano hayo yataendelea kuheshimiwa''.

Mkakati wa pamoja uliizuia Iran kuendelea na mpango wake wa kinyuklia huku Umoja wa mataifa ukikubali kuiondolea vikwazo Iran vilivyowekwa pamoja na, Marekani na bara Ulaya.

Kwa nini Marekani ilijiondoa?

Katika taarifa katika runinga ya taifa siku ya Jumanne , rais alisema kuwa Marekani itajiondoa katika mkakati huo wa pamoja JCPOA.

Aliutaja kuwa mkataba mbaya unaopendelea upande mmoja ambao haungewahi kuafikiwa.

Rais Donald Trump wa Marekani
Maelezo ya picha, Rais Donald Trump wa Marekani

Mbali na kuilinda Marekani na washirika wake, alisema umeweka masharti hafifu kuhusu mipango ya kinyuklia ya serikali hiyo na kwamba haikuwekewa vikwazo vyovyote kuhusu tabia yake ikiwemo vitendo vyake vibaya nchini Syria , Yemen na mataifa mengine.

Rais huyo aliongezea kuwa makubaliano hayo hayakuangazia utengezaji wa silaha za masafa marefu za Iran huku uchunguzi wake ukiwa hafifu.

Amesema kuwa atarudisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo ambavyo vilikuwa wakati makubaliano hayo yalipotiwa saini 2015.

Ni lini vikwazo hivyo vitaanza kutekelezwa?

Wizara ya fedha nchini Marekani imesema kuwa vikwazo vya kiuchumi havitawekwa dhidi ya Iran mara moja, bali vitategemea kipindi cha kati ya miezi mitatu na sita ijayo.

Katika taarifa iliowekwa katika mtandao wake , ilisema kuwa vikwazo hivyo vitalenga viwanda vilivyotajwa katika makubaliano hayo, ikiwemo sekta ya mafuta, uuzaji wa ndege, biashara ya vyuma mbali na harakati za taifa la Iran kununua noti za dola za Marekani.

Mshauri wa maswala ya usalama wa kitaifa nchini Marekani John Bolton ameripotiwa akisema kuwa mataifa ya Ulaya yanayofanya biashara na Iran yatalazimika kusitisha biashara hiyo katika kipindi cha miezi sita la sivyo ziwekewe vikwazo na Marekani.

Kumekuwa na hisia gani duniani?

Wizara ya maswala ya kigeni nchini Urusi imesema kuwa imeshangazwa na hatua hiyo ya Marekani kufuatia kitendo hicho cha rais Trump.

Japan imesema kuwa itafuatilia kwa karibu athari za kujiondoa kwa Marekani. Mjumbe mkuu wa muungano wa Ulaya Federica Mogherini, amesema kuwa Ulaya iko tayari kulinda makubaliano hayo.

Aliyekuwa rais wa Marekani Barrack Obama ambaye alichukua jukumu kubwa katika makubaliano hayo alisema katika mtandao wa Facebook kwamba makubaliano hayo yanalinda maslahi ya Wamarekani.

''Kujiondoa katika makubaliano hayo ya pamoja kunaiweka Marekani katika hali mbaya na washirika wake wa karibu katika makubaliano ambayo wajumbe wakuu wa taifa letu, wanasayansi na wapelelezi wetu walijadiliana na kuafikia'', alisema.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema kuwa ana wasiwasi mkubwa kuhusu tangazo hilo na kuwataka washirika wengine kuunga mkono.

Lakini waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema kuwa anaunga mkono hatua ya Trump kujiondoa kutoka katika mkataba huo alioutaja kuwa janga. Na Saudia Arabia ambaye ni hasimu mkuu wa Iran imesema kuwa inaunga mkono hatua ya rais Trump.

Ni nini kilichokubaliwa katika mkataba huo?

Mataifa yenye uwezo mubwa dunia JCPOA yaliilazimu Iran kukubali kupunguza utengezaji wa madini ya Uranium ambayo hutumika kutengeza mafuta yanayotumika kutengeza silaha mbali na silaha za kinyuklia- kwa takriban miaka 15 huku utengezaji wa uranium ukisitishwa kwa miaka 10.

Iran pia ilikubali kubadilisha kifaa cha kutengeza maji mazito ili kutozalisha madini ya plutonium yanayotumika kutengeza bomu.

Iran ilipunguza mpango wake wa kinyuklia kwa leng la kuondolewa vikwazo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Iran ilipunguza mpango wake wa kinyuklia kwa leng la kuondolewa vikwazo.

Iran ilitarajia kwamba vikwazo ilivyowekewa na UN, US na EU ambavyo vilikuwa vimeathiri uchumi wa Iran vitaondolewa.

Makubaliano hayo yaliafikiwa kati ya Iran na mataifa matano ambayo yana uanachama wa kudumu katika baraza la usalama la umoja wa Mataifa -Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Urusi pamoja na Ujerumani

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa kinyuklia ni wa amani na kwamba imekuwa ikitekeleza makubaliano hayo.