Trump adai Pakistan imeihadaa Marekani muda mrefu

Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Rais wa Marekani Donald Trump ameishutumu Pakistan na kusema imekuwa ikiihadaa na kuidanganya Marekani kwa muda mrefu.

Amesema taifa hilo limeendelea kuilaghai Marekani, ilhali inazidi kupokea mabilioni ya dola ya msaada, hasa katika miaka ya hivi karibuni.

Bw Trump amesema Pakistan imepokea jumla ya dola bilioni 33 katika miaka 15 iliyopita "na hawajatusaidia kwa chochote ila uongo na ulaghai, wakiwafikiria viongozi wetu kuwa wapumbavu".

Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Bw Trump amedai kuwa, Pakistan inawapa hifadhi magaidi, ambao wanatafutwa na wanajeshi wa Marekani walioko nchini Afghanistan.

Marekani inadhamiria kuendelea kuzuilia zaidi ya dola milioni 250 ya msaada kwa Pakistan, ambayo ilichelewesha makusudi kuwashilishwa kwa taifa hilo la bara Asia, tangu mwezi Agosti mwaka jana.

Wakati huo, Wizara ya nchi za kigeni nchini Pakistan, iliahidi kuwa itazidisha juhudi zake za kimataifa za kupambana na magaidi.