Tillerson: Mazungumzo yataendelea na Korea Kaskazini hadi "bomu la kwanza lianguke"

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani Rex Tillerson, amesisitiza kuwa Donald Trump anataka kutatua mzozo na Korea Kaskazini kwa njia ya mazungumzo.

"Hilo litaendelea hadi bomu la kwanza lianguke," aliiambia CNN.

Vikwazo na mazungumzo , alisema, vimeleta umoja wa kimataifa dhidi ya mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini.

Mwezi uliopita, Bw. Trump alimuambia Bw. Tillerson asitupe muda wake kutafuta mazungumzo na Kim Jong-un.

Wakati wa mahojiano ya leo Jumapili, Tillerson alikataa kuzunguma ikiwa alimuita Bw. Trump mjinga.

Miezi ya hivi karibuni Korea Kaskazjni imekaidi maazimio ya kimataifa na kuendea na majaribio silaha za nyuklia na kurusha makombora kupitia anga ya Japan.

Wadadisi wanasema kuwa taifa hilo liko mbioni kuunda kombora lenye uwezo wa kufika nchini Marekani.