Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi na China zatumia kura ya turufu kuisaidia Syria
Urusi na China zimetumia kura ya turufu kuzuia jaribio la Umoja wa Mataifa la kutaka kuiwekea vikwazo serikali ya Syria.
Marekani, Uingereza na nchi nyengine katika Baraza la Usalama, zilitaka kuiadhibu Damascus kwa tuhuma za kutumia silaha za sumu katika maeneo ya waasi.
Ni mara ya saba sasa Urusi inatumia kura yake ya VETO kuikinga serikali ya Rais Assad na tuhuma za kimataifa.
Katika hotuba yake iliyojawa hisia kabla ya kura, balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Matthew Rycroft, alisimulia kifo cha mwathirika mmoja ambae alipelekwa katika hospitali baada ya shambulio la gesi yenye sumu.
Hata hivyo, kwa upande wake, balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Liu Jieyi, ameliambia Baraza la Usalama kwamba bado hakuna vilelezo kwamba serikali ya Syria imetumia silaha za kemikali.
Naye Rais Vladmir Putin amesema vikwazo vitazuia jitihada za mazungumzo ya amani yanayoendelea Geneva baina ya serikali na wapinzani wake.
Marekani imesema Urusi na China zimekataa kuwajibisha vikosi ambavyo viliangusha gesi za sumu na kusababisha vifo vya wanaume, wanawake na watoto.