Zaidi ya nyangumi 200 waliokwama ufuoni New Zealand warudi baharini

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanamazingira nchini New Zealand, wanasema zaidi ya nyangumi 200 waliokuwa wamekwama ufuoni sasa wamemudu kurudi wenyewe maji makuu.
Hata hivyo bado kuna wengine 17 ambao wangali wamekwama ufuoni na sasa wanatunzwa hadi pale mawimbi yatakapokuwa makubwa ili wasaidiwe kurudi baharini.
Eneo hilo la pwani la kilomita 20, lenye maji ya kina kifupi, ni gumu kwa nyangumi kuogelea.

Chanzo cha picha, AFP
Jana maafisa na watu wa kujitolea walisaidia kundi lingine la nyangumi karibu 100 waliokwama kwenye ufuo huohuo wa Farewell Spit huko New Zealand.
Nyangumi hao walikuwa ni sehemu ya wale 400 waliokwama baharini juzi huku waliosalia 300 wakifariki, katika kisa ambacho kinatajwa kuwa kibaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo.

Chanzo cha picha, Reuters
Bado wanasayansi hawajafanikiwa kufahamu ni kwa nini nyangumi hufika kwenye ufuo wa bahari.
Lakini inadhaniwa huwa inatokea kwa sababu nyangumi huzeeka , huugua au huwa wameumia na kupoteza mwelekeo.
Wakati mwingine, nyangumi anapokwama baharini, huwalilia wenzake ambao watafika kujaribu kumuokoa lakini kisha nao wanajipata wamekwama.

Chanzo cha picha, Reuters













