Mke wa Magufuli alazwa Muhimbili, Tanzania

Mke wa Rais wa Tanzania John Magufuli, Janeth, amelazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.

Ikulu imetoa picha ya Rais Magufuli akimjulia hali katika wodi ya Sewa Haji.

Hata hivyo, haijajulikana anaugua maradhi gani.

Novemba mwaka jana, siku chache baada ya kuapishwa hospitali hiyo ni miongoni mwa taasisi za serikali ambapo Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza.

Alisema alisikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini.

Aidha, alikuta baadhi ya vifaa vya kufanyia kazi na mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN vikiwa havifanyi kazi kwa muda wa miezi kadhaa.

Alibadilisha usimamizi wa hospitali hiyo.

Taarifa ya ikulu inasema leo, alipokuwa anamjulia hali mkewe, pamoja na mke wa balozi na waziri mstaafu wa Tanzania Omar Ramadhan Mapuri, wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Sewa Haji wamemshukuru "kwa hatua zilizochukuliwa na serikali kuboresha hospitali ya taifa ya Muhimbili na wamebainisha kuwa licha ya kuboreshwa kwa mazingira ya hospitali, pia wanapata huduma nzuri kutoka kwa madaktari na wauguzi."