Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kambi ya wahamiaji ya Calais kubomolewa Ufaransa
Maafisa wa serikali nchini Ufaransa wanatarajiwa kuanza kubomoa kambi ya wahamiaji ya Calais ambayo imekuwa ikifahamika kama "Jungle".
Wahamiaji zaidi ya 2,300 ambao wamekuwa kwenye kambi hiyo waliondoka kwa hiari Jumatatu kuelekea vituo mbalimbali vya kuhudumia wahamiaji kwa muda ambayo vimetengwa Ufaransa.
Wahamiaji wengine waliokuwa wamesalia walitarajiwa kuondoka leo.
Kambi hiyo ya Calais ilifahamika zaidi na kuwa kama moja ya 'nembo' ya mzozo wa wahamiaji Ulaya idadi ya wahamiaji wwanaotaka kuingia Ulaya ilipoongezeka tangu mwaka jana.
Inadakiriwa kwamba wahamiaji kati ya 7,000-8,000 wamekuwa wakiishi katika kambi hiyo, wakitaka kufika Uingereza.
Shughuli ya kuwaondoa wahamiaji hao imekuwa ya amani kufikia sasa lakini kuna wasiwasi kwamba huenda baadhi ya wahamiaji wakaamua kuendelea kukaa katika kambi hiyo, wakihofia kuondoka kwao kutadidimiza matumaini yao kuvuka mlango wa bahari wa Uingereza na kuingia Uingereza.
Kumekuwa na tahadhari kwamba huenda wale wasiotaka kuhama wakapiga hema maeneo ya makazi yaliyo karibu ubomoaji unapoendelea.
Watoto ndio pekee wameruhusiwa kusalia Calais. Wataruhusiwa kuishi kwenye mabehewa ambayo yamegeuzwa kuwa vyumba vya makazi.