Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rwanda yanunua ndege ya kisasa ya Airbus
Shirika la ndege la Rwanda, RwandAir, limezidisha ushindani katika uchukuzi wa ndege Afrika Mashariki na Kati kwa kununua ndege aina ya Airbus A300-200.
Ndege hiyo itawezesha shirika hilo kufika masoko ya Ulaya na bara Asia.
Ndege hiyo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa kimataifa wa Kanombe, Kigali.
Mkuu wa shirika la RwandAir John Mirenge amewaambia waandishi wa habari kuwa ndege hiyo yenye nafasi ya abiria 244 ndiyo ya kwanza katika ukanda huu na ina teknolojia ya kisasa na ya hali ya juu.
"Ukiwa angani ndani ya ndege hii unaweza kupiga simu, kupata ujumbe wako wa simu, ujumbe wa barua pepe, ujumbe wa WhatsApp na mawasiliano mengine. Haya hayakuwepo katika ndege nyingine tulizo nazo," amesema.
"Hata katika ukanda huu na kwingineko barani Afrika hakuna shirika lenye ndege iliyo na uwezo huo."
Ni ndege iliyotengenezwa nchini Ufaransa ilinunuliwa dola milioni 200 za Marekani.
Bw Mirenge, anasema safari za shirika la ndege la RwandAir zilikuwa zinajikita sana Afrika magharibi na kati na kwamba ndege hii sasa inalipatia shirika hilo uwezo wa kuvamia masoko ya Ulaya, Asia na kusini mwa Afrika.
Safari ya kwanza ya ndege hiyo inatarajiwa kufanyika tarehe 8 Oktoba kuelekea mjini Dubai.
Shirika hilo sasa linalenga kuwa likisafirisha abiria laki 750 kila mwaka ifikapo mwishoni mwa mwaka 2017.