Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanariadha wa Marathon washambuliwa na mavu Japan
Miongoni mwa changamoto zinazowakumba wanariadha wanaoshiriki mbio ndefu za Marathon, kushambuliwa na mavu wenye hasira huwa hakutarajiwi, lakini hilo ndilo lililowakumba wanariadha katika mbio za hivi majuzi nchini Japan.
Wakimbiaji walikabiliwa na mavu, mdudu anayekaribia kufanana na nyuki, pale walipokuwa wamefika kilomita 7 (maili 4.3) katika mbio za nusu marathon za Daikon Radish mjini Hida - ambayo hutumika katika maadhimisho ya ukuzaji wa mboga katika eneo hilo.
Mavu hao wenye rangi ya manjano na wenye asili yao nchini Japan, waliamshwa na wanariadha hao walipokuwa wakivuka daraja ambalo lina maskani yao.
Hayo ni kwa mjibu wa gazeti linalochapishwa kila siku nchini Japan la The Mainichi daily.
Bila ya wao kufahamu, wadudu hao hatari walikuwa wamejenga maskani yao chini ya ukuta wa daraja na walipandwa na hamaki, pale walipotatizwa na kutikisika kwa daraja hilo, wakati wakimbiaji hao walipokuwa wakilivuka wakikimbia.
Mavu hao walithibitisha kwamba wao ndio mabingwa, baada ya kuwadunga vikali wanariadha 115, walipokuwa wakilivuka daraja hilo.
"Hatukufahamu kuhusu maskani ya wadudu hao siku ya kufanyia majaribio njia hiyo. Tunataka kuwatumia barua ya masikitiko yetu kwa wote walioumwa," afisa mmoja mkuu wa mji huo aliwaambia wanahabari, huku akiongeza kusema kuwa, mwaka ujao watakuwa waangalifu zaidi ili kuzua janga kama hilo.
Wale walioumizwa wamepewa matibabu huku kukiwa na idadi ya karibu wanariadha 30 au 40 walioshindwa kumaliza mbio hizo kutokana na hatari na uchungu wa kuumwa.
Walioibuka washindi walituzwa mboga ya aina mbalimbali ikiwemo figili na mchicha.
Waandalizi wa mbio hizo wameomba msamaha na wamefaulu kuondoa maskani ya mavu hao.