Ni kipi wanachopitia watu wanaosoma elimu ya juu wakiwa watu wazima?

Na, Asha Juma,

BBC Swahili

Sio siri kuwa elimu inaweza kufungua enzi mpya ya fursa.

Watu wamekuwa wakijikuta katika kurejea kusoma hata baada ya kumaliza pengine elimu ya sekondari au chuo muda mrefu uliopita na kipindi hicho tayari wamesonga mbele kimaisha kiasi cha hata kuwa na familia.

Suala hili linaweza kuonekana kuwa rahisi kulitamka kwa mdomo na kulipanga akilini kuliko namna ya kulitekeleza.

Kwa sababu inapofika wakati wenyewe, kuna maswali unaweza kuona unaanza kujiuliza kama vile je, huu ndio muda muafaka wa mimi kurejea shuleni, familia yangu itastahimili vipi ikiwa nitakuwa na majukumu mengi kupita kiasi kinachoweza kukubalika kwa uendelezaji wa masuala mengine muhimu ya nyumbani ambayo bado ni majuku yangu?

Hata hivyo, unapofikiria sana, unaweza kujipata ukijifariji moyoni kwamba, kumekuwa na wengi nyuma yako waliopitia hali hii ya kurejea kusoma wakati tayari wameanza familia na kufanikiwa maishani, sasa mbona wewe ulifanye kuwa suala zito.

Ili kufahamu kwa undani nini kinachokumba wahusika, nilizungumza na Joyce Juma ambaye alipata masomo yake ya shahada ya uzamili akiwa na familia na kuangazia jinsi safari yake ilivyokuwa.

Joyce Juma anasema kuwa baada ya kuolewa na kupata watoto, aliketi chini na akathmini hali ilivyo kazini kwake na kuamua kwamba kuna umuhimu wa kurejea darasani.

Hitaji hili lilichochewa na uchu wake wa kutaka kupandishwa cheo kazini na alipopima kwa mizani hali ilivyo, aligundua ushindani mkubwa hasa miongoni mwa wafanyakazi wa ngazi yake kwasababu wengi wao, kiwango chao cha elimu kilikuwa kinatoshana.

Changamoto za kusoma ukiwa mtu mzima

Joyce anakiri kwamba mwanzoni aliona hali ni rahisi lakini mambo yakaendelea kuwa magumu kadiri siku zilivyoendelea kusonga mbele.

"Inafika mahali sasa unapata uzito wake ndio unaanza kuushuhudia, kuna mambo ya família yanakungojea, kuna kazi za shule zinakusubiri, mtoto amepewa kazi ya ziada, mume akiingia ndani ya nyumba pia naye ana mahitaji lazima umshughulikie kama kawaida kwasababu alikuwa kazini.

Joyce anasema kuna kipindi alihisi kuchanganyikiwa, yaani hajui aendelee au aachane na masomo hayo. Ingawa ile ari ya kutaka kufikia malengo yake ilimpa motisha wa kusonga mbele kila uchao.

"Kuna wakati ulifika, mpaka nikawa nafikiria niache kusoma. Kwasababu ukiingia nyumbani, mtoto ni mgonjwa na wakati huo huo umepewa muda wa ukomo wa kuwasilisha kazi ulizopewa kwa ajili ya masomo yako. Sasa hujui upeleke mtoto hospitali au ufanye kazi ulizopewa na mhadhiri na kuziwasilisha kwa wakati stahiki."

Anasema hapo, alianza kukimbizana na wahadhiri ili wachukue kaze yake lakini kuna wengine ambao hawakumuelewa, walikuwa wakisema ikiwa hujawasilisha kwa wakati uliwekwa, moja kwa moja unapata sufuri.

"Ikifika wakati huo, nilikuwa naamua kwanza kutulia, kisha namfuata mhadhiri baadaye, nianze kumuelezea kilichofanya nisiwasilishe kazi kwa wakati kwasababu akisema kwamba atanipa sufuri, hiyo ilimaanisha nimefeli somo hilo."

Unapoamua kurejea kusoma ukiwa na familia, mara nyingi mzazi hulazimika kukaa macho hadi usiku mwingi, wengine wakiwa wamelala, hapo ndio unapata nafasi ya kufanya masomo yako wakati umepunguza shughuli zingine za familia. Katika uzoefu wake, Joyce pia amekubaliana na hili.

"Unajipata huna muda wa kusema napumzika au nalala mapema na wakati huo huo, unatakiwa urauke asubuhi na kuendelea na shughuli zingine.

"Wakati mwingine ukiwa umefika shuleni, unajihisi kama jana yake uling’ang’ana ukafanya kazi ya shule uliotakiwa kufanya, lakini mhadhiri akiangalia kazi yako, anakwamba uliofanya yote sivyo, umekosea."

Pia kingine anaongeza, kuna wakati anaingia darasani kama wengine, mwalimu anafundisha lakini yeye hakuna anachoshika kwa siku hiyo, hadi mhadhiri anamaliza somo lake.

"Wakati mwingine unashtukia mwalimu anakuuliza swali lakini hata yeye anajua tu, huyu hayuko hapa kwasababu unajibu tofauti na kile alichofundisha."

Hiyo ilimaanisha kwamba baada ya masomo ataanza kuomba wenzake vitabu, akasome tena kile walichoandika akifika nyumbani, kabla ya kuanza kufanya kazi ya ziada aliyoacha mhadhiri kwa siku ile.

Kingine alichokumbana nacho ni changamoto ya kulipa ada kwasababu watoto wanahitaji kulipiwa ada na yeye naye vilevile. Ilikuwa inafika mahali akiona hataruhusiwa kufanya mtihani hadi amalize kulipa ada, anatafuta wa kumkopa kunusuru masomo yake.

Ipi iliyokuwa nguvu ya Joyce kusonga mbele

Joyce anasema kwake yeye anashukuru sana Mungu kwasababu mume wake alikuwa mstari wa mbele kumuunga mkono. Na pengine hatua hii ilitokana na wao kuketi chini mwanzoni, wakazungumza na kukubaliana.

"Yeye pia alikuwa akiona kuna wakati narejea nyumbani nikiwa na msongo wa mawazo, kwasababu pengine kazini mambo hayakwenda vile ilivyotakikana, au pengine wafanyakazi wenzangu wamepandishwa cheo na mimi nimebaki pale pale."

Hata wakati ambapo Joyce alikuwa ametaka kabisa kuacha masomo, akihisi kuwa anajaribu kadri ya uwezo wake lakini bado wahadhiri wanampa alama ya kufeli katika baadhi ya masomo, mume wake alimpa moyo na kumshika mkono.

Kuna wakati ambapo aliingilia kati na kufanya majukumu mengine ya nyumba.

"Lakini na mimi nilikuwa najitahidi, siku ile nimepata nafasi, ninafanya majukumu yangu vizuri zaidi.

Kulingana na yeye, siri yake kuu ilikuwa akifika nyumbani tu, anaanza kwa kumsaidia mtoto kazi yake ya shule, anaangalia masuala ya chakula na mwisho ndio anaingia kwenye masomo yake.

Kipi kipya atakachofanya akiwa tena katika hali hii?

Joyce anasema ikiwa pengine kuna kitu ataweza kurekebisha kutokana na safari yake ya kwanza, atajaribu sana kuweka sawa masuala ya pesa, yeye pamoja na watoto wasitatizike katika ulipaji wa ada.

Pia ushauri wake, anaona ni bora zaidi ikiwa mtu atarejea kusoma watoto wakiwa wamekua kidogo ki umri.

Hili ni kutokana na kwamba wanapokuwa wadogo wanakuwa katika hatari ya kuwa wagonjwa mara kwa mara ikilinganishwa na watoto ambao wamekua kidogo kiumri.

Uzuri ni kwamba watoto wake nao walifika wakati wakaanza kuelewa kwamba mama pia naye anasoma.

"Walikuwa wananiuliza, mwalimu wako amekupa kazi ya kufanya nyumbani, leo amekupa ruhusa usiende?", Joyce anasema.

Bila shaka kulingana na simulizi ya Joyce, safari yake hii ya kupata shahada ya uzamili akiwa tayari na família, kama mwingine yeyote haijawa rahisi.