Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi majambazi walivyowateka nyara watu 30 wakati wa swala ya alfajiri
Ripoti kutoka jimbo la Zamfara kaskazini mwa Nigeria, zinasema takriban watu 30 walitekwa nyara na majambazi siku ya Alhamisi katika msikiti wa mtaa wa Tsafe walipokuwa wakiswali.
Pia, washambuliaji walivamia mitaa katika mji wa Dansadau ambapo waliwaua watu na kuwateka nyara watu zaidi wakiwemo wanawake.
Miji ya Dankurmi, Fari Ruwa, Tungar Kawo, Dan Ma'aji na mingineyo ya Dansadau, Maru na Tsafe yote iko katika jimbo la Zamfara, na imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi mara kwa mara.
Wakaazi wa miji hiyo waliambia BBC – siku ya Alhamisi asubuhi, washambuliaji hao waliwateka nyara watu 30 walipokuwa katikati ya swala ya Fajr katika mji wa Tsafe.
Mbali na kuwateka nyara watu ili wapate fidia, walisema pia wanawaachilia wanyama shambani kula mazao wanayolima, na wakasema watampiga risasi mtu yeyote anayezungumza, mkulima ambaye aliomba jina lake lisitajwe aliiambia BBC.
“Kwa sababu hatukupata kulima wakati wa masika. Tuliamua kufuga Wanyama. Wakati wa mvua walitunyanyasa, kuua watu, kuteka nyara watu na hivyo kuwazuia watu kulima.
“Walichukua kila kitu tulicholima, katika vijijini ambako hawapati fedha za fidia wanauwa watu,” alisema mkulima huyo.
Katika mji wa Farinruwa mtaa wa Maru, hali ni sawa na hiyo kulingana na mkazi wa mji huo.
“Hata wakati huu tunapozungumza na nyinyi BBC wanateka watu. Usipowaruhusu wakuue, watakuteka nyara na kucheza nawe. Hakuna maafisa wa usalama hapa kabisa."
Hata hivyo, serikali ya Jimbo la Zamfara imesema imechukua hatua za haraka baada ya kupokea taarifa hizi, na imewasiliana na Jeshi la Nigeria. Inasema ndege za kijeshi zimetumwa kupambana na majambazi hao.
Sulaiman Bala Idris, msemaji wa gavana wa jimbo la Zamfara naye alitoa taarifa zaidi kuhusu suala hilo.
"Tulipata habari hii, na gavana aliambia vikosi vya usalama mara moja. Kuhusu kisa cha kutekwa nyara kwa watu majira ya asubuhi walipokuwa wakiswali, tunachunguza,” alisema.
Jimbo la Zamfara linakumbwa na mashambulizi ya majambazi, wanaowateka nyara watu ili kuwakomoa, wakati mwingine wanachoma nyumba na mali na kuiba mifugo ya watu.
Hata hivyo, mamlaka za jimbo hilo zimeanzisha kundi la askari wa Zamfara ambao wanapambana na shughuli za majambazi hao, lakini mashambulizi bado yanaongezeka.
Jeshi la Nigeria limekuwa likijikita zaidi katika mashambulio ya angani yanayolenga ngome za magenge hayo. Akaunti rasmi ya Twitter ya jeshi mara kwa mara huweka kanda ya video na picha, ikidai kuwa imefanikiwa kutokomeza makundi ya majambazi.
Wanigeria wengi wanaishi katika hofu ya mara kwa mara ya kutekwa nyara na kushikiliwa na magenge yenye silaha, hasa kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, ambako maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao.
Mamia ya watoto wa shule wamekuwa wakitekwa nyara na kuachiliwa, na serikali ya majimbo hayo huwaambia wakaazi kujihami dhidi ya majambazi hao ishara kwamba haina jinsi ya kukabiliana na majambazi hao.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi