Machozi, jasho na damu: Fahamu pandashuka za maisha ya mwanamiereka Hulk Hogan

Muda wa kusoma: Dakika 4

Hulk Hogan, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 71, alikuwa shujaa wa miereka wa Wamarekani wote, huku mchanganyiko wake wa riadha na uchezaji wake wa maonyesho makubwa ukiwa sehemu kubwa ya mchezo huo uliokuwa maarufu katika miaka ya 1980.

Akipewa jina Terry Gene Bollea baada ya kuzaliwa, alianza kazi yake huko Florida katika miaka ya 1970 na anajulikana kupata jina la utani la "Hulk" baada ya kuwa mwigizaji wa filamu ya The Incredible Hulk Lou Ferrigno kwenye kipindi cha TV cha ndani.

Kisha akawa Hogan baada ya kujiunga na Shirikisho la Miereka Duniani (WWF) - ambalo mmiliki wake Vince McMahon alitaka mpiganaji mwenye jina la Ireland.

Hogan akipigwa picha ya pamoja na wazazi Peter na Ruth nyuma ya jukwaa katika ukumbi wa Madison Square Garden huko New York mnamo 1984.

Umaarufu wake ulienda sambamba na kuibuka kwa miereka kama tamasha la televisheni, mchezo unaochanganya tamthilia, wahusika na hadithi za biashara ya maonyesho.

Huku watu wazuri wakipambana na wabaya, alikuwa shujaa wa kipekee na kipenzi cha mashabiki.

Hogan alitumia ujuzi wake wa uigizaji kwenye skrini alipoigiza kama Thunderlips, mpinzani wa Sylvester Stallone kwenye pambano la hisani, katika filamu ya Rocky III ya 1982.

Pia aliigiza Starlight Starbright katika onyesho la Dolly Parton mwaka wa 1987, huku mwimbaji huyo akionekana kama shabiki wake mkuu katika video ya wimbo wake Headlock On My Heart.

Wakati Wrestlemania V ilifanyika katika jumba la Trump Plaza huko Atlantic City, New Jersey, mwaka wa 1989, Hogan alikutana na mwenyeji wake na baadaye kumuidhinisha Donald kama rais.

Alitengeneza taaluma ya Hollywood nje ya ulingo katika filamu zikiwemo No Holds Barred, Suburban Commando, Mr Nanny (pichani) na Santa with Muscles.

Akiwa ulingoni, alikumbana na kizazi kipya cha nyota wa miereka katika miaka ya 2000, akiwemo Dwayne "The Rock" Johnson katika pambano lililoitwa "Icon vs Icon" kwenye Wrestlemania X8.

"Nina umbo bora kuliko yeye," Hogan aliambia Reuters, miezi mitano kabla ya siku yake ya kuzaliwa ya 50 - lakini The Rock aliibuka mshindi.

John Cena alihisi nguvu ya Hulk Hogan - au angalau ilionekana - katika onyesho la pamoja katika Tuzo za Teen Choice za 2005.

Hogan aliendelea kupigana huku umaarufu wake ukiendelea kupanda juu licha ya miaka kusonga mbele - pichani akichuana na mkongwe mwenzake Ric Flair mwaka wa 2009.

Hadithi zinaweza kuwa ziliandikwa mapema lakini damu ilikuwa halisi.

Kwa jumla, Hogan alishinda ubingwa mara sita wa WWF/WWE, aliongoza WrestleMania mara nane, na aliingizwa mara mbili kwenye Ukumbi wa Umaarufu wa WWE.

Pia alifurahia mafanikio ya TV katika kipindi chake cha Hogan Knows Best, pamoja na mke wake Linda na watoto wao wawili kutoka 2005-07.

Umaarufu wake ulipata pigo mwaka 2015 aliposimamishwa kazi na WWE kwa kutumia lugha ya ubaguzi kwenye video iliyovuja. "Tafadhali nisamehe," alisema katika mahojiano ya kilio katika kipindi cha ABC cha Good Morning America . "Mimi ni mtu mzuri," aliongezea.

Katika miaka ya hivi majuzi, alizungumziwa sana na mashabiki kama mmoja wa wafuasi mashuhuri wa Donald Trump, akimuidhinisha kwa mtindo wake wa maonyesho katika hafla kama vile Kongamano la Kitaifa la Republican mwaka mmoja uliopita, na mkutano wa kampeni katika ukumbi wa Madison Square Garden huko New York mnamo Oktoba (pichani).

Imetafsiriwa na Seif Abdalla