Arikomban: Simulizi ya kusikitisha kuhusu tembo wa India anayependa mpunga

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa zaidi ya mwezi mmoja tu, tembo mwitu nchini India amekamatwa mara mbili, kudungwa sindano ya kumlemazwa mara nyingi na kuhamishwa zaidi ya kilomita 280 (maili 173) kutoka msitu wake wa asili katika jitihada za kumweka mbali na makazi ya watu akitafuta chakula.
Arikomban ("pembe ya mpunga" katika lugha ya Kimalayalam) – anayedaiwa kuvamia maduka kwa ajili ya mchele – amehamishwa kutoka katika majimbo ya kusini ya Kerala na Tamil Nadu hata wakati mamlaka inapambana kumtafutia makazi ya kudumu. Tembo pia amekuwa katikati ya vita vya kisheria na mjadala juu ya haki za wanyama.
Huko Kerala, Arikomban amekuwa "ishara ya ustahimilivu katika kukabiliana na ukosefu wa haki," anasema mwanaharakati Sreedevi S Kartha.
"Matukio yameonyesha jinsi mchakato wa kuhamishwa unaweza kuwa wa kikatili kwa tembo," aliiambia BBC. "Imechochea dhamiri za watu katika jimbo."
Mapema mwaka huu, kikundi cha wenyeji karibu na makazi ya asili ya Arikomban, Chinnakanal katika wilaya ya Idukki ya Kerala, walidai kuhamishwa kwake baada ya kusumbuana mara kwa mara na wanadamu hali iliosababisha maandamano..
Maafisa wanasema tembo huyo ameua watu kadhaa kwa miaka mingi - madai ambayo yamekanushwa na jamii za eneo hilo.
Idara ya misitu ya Kerala ilitangaza kuwa inapanga kumkamata Arikomban na kumfanya kuwa tembo aliyefunzwa. Wanaharakati wa haki waliwasilisha ombi kwa mahakama kuu, wakitaka kuingilia kati ili kuhakikisha usalama wa mnyama huyo.
Bi Kartha, mwanachama wa People for Animals, mojawapo ya makundi ambayo yaliwasilisha ombi hilo mahakamani, anasema serikali haikutoa ushahidi wowote wa ndovu huyo kuua binadamu.
Mnamo Aprili, kamati iliyoteuliwa na mahakama ya wataalam iliamua kuwa itakuwa bora kumuhamisha tembo huyo.
Zaidi ya siku mbili, maafisa 150 walifanya operesheni kubwa huko Chinnakanal ili kumkamata Arikomban. Mnamo tarehe 29 Aprili, tembo huyo alihamishwa hadi kwenye Hifadhi ya Tiger ya Periyar takriban kilomita 80 (maili 50) kutoka.
Takriban mwezi mmoja baadaye, maafisa wa misitu huko Tamil Nadu, jimbo jirani, walijikuta wakifanya operesheni kama hiyo ya kumhamisha mnyama huyo kwa mara nyingine.
Tembo huyo alikuwa ameonekana katika mji wa Cumbum mnamo tarehe 27 Mei. Video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mnyama huyo akipita katika mji huo wenye watu wengi, akiharibu majengo na magari.
Watu watatu walijeruhiwa - mmoja wao, mzee wa miaka 65, alikufa kwa majeraha siku mbili baadaye. Amri ya kutotoka nje iliwekwa huku mamlaka ikijaribu kumkamata tembo huyo.

Chanzo cha picha, SUPRIYA SAHU and Twitter
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Arikomban sasa alijikuta katikati ya vita vya mahakama. Mwanasiasa aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Kerala akiomba tembo huyo arejeshwe jimboni. Ombi katika Mahakama Kuu ya Madras lilitaka kulipwa fidia kwa uharibifu aliosababisha huko Tamil Nadu.
Waziri wa misitu wa Kerala, AK Saseendran, alisema mgogoro huo ulithibitisha mpango wa serikali yake wa kufanya Arikomban kuwa tembo aliyefungwa na kuwalaumu wanaharakati kwa uhamisho wa tembo huyo.
Lakini tukio la Cumbum lilionyesha kuwa Arikomban hakuwa tishio kwa maisha ya binadamu, Bi Kartha anasema. "Alipata kiwewe na kukimbizwa lakini hakushambulia wanadamu huko."
Mnamo tarehe 5 Juni maafisa wa msitu wa Tamil Nadu walimlemaza na kukamata tembo huyo. Picha za hivi punde za kunaswa kwa Arikoban ziliibua wasiwasi kuhusu mara ambazo alidungwa sindano ili kutulia na majeraha ambayo mnyama huyo alipata alipokuwa akisafirishwa na maafisa kwa lori la wazi.
Stephen Daniel, mwanaharakati wa wanyamapori, alisema kuwa mnyama huyo alikuwa akilipa bei kwa maamuzi ya sera ya serikali ambayo ilisababisha makazi ya watu kwenye njia za tembo.
"Maumivu ya kiakili na ya kimwili ambayo mnyama huyo alikuwa akipata hayawezi kueleweka na idara za misitu za majimbo hayo mawili zina mengi ya kujibu," alisema.
Huko Kerala, vikundi vya kikabila huko Chinnakanal vimedai kwamba tembo arudishwe kwenye makazi yake ya asili. Wanapanga Kwenda mahakamni kumrudisha tembo huyo.
"Kuna haja gani ya kukamata na kuhamisha tembo kwenye hifadhi ya simbamarara ikiwa atateseka kwa namna hiyo?" muandamanaji mmoja aliambia kituo cha habari Malayala Manorama.
Idara ya misitu ya Tamil Nadu ilisema kuwa Arikomban alikuwa amehamishwa ndani kabisa ya Hifadhi ya Tiger ya Kalakkad Mundanthurai, zaidi ya kilomita 200 kutoka Cumbum.
Ripoti zilisema wenyeji wanaoishi karibu walipinga kuhamishwa kwake, wakiwa na wasiwasi kwamba tembo huyo anaweza kusababisha uharibifu katika makazi yao.
Supriya Sahu, afisa wa msitu wa Tamil Nadu, alisema uhamishaji huo "umefaulu". Makazi yake mapya yalikuwa na "msitu mnene na maji mengi" na tembo alikuwa akila vizuri, alisema katika sasisho kwenye Twitter.

Chanzo cha picha, TAMIL NADU GOVERNMENT
Afisa mkuu alisema uhamisho wa Arikomban hadi kwenye hifadhi ya simbamarara huko Tamil Nadu ulikuwa "umefaulu"
Wafanyakazi wa msitu wa jimbo hilo pia walikuwa wamepiga kambi katika hifadhi hiyo, wakifuatilia afya ya Arikomban na kufuatilia mienendo yake.
"Ana afya njema na majeraha yake yamepona," afisa wa misitu Srinivas Reddy aliambia BBC Tamil wiki iliyopita.
Lakini matukio ya hivi majuzi yanathibitisha kwamba tembo huyo atarejea katika maeneo ya makazi hata baada ya kuhamishwa ndani kabisa ya msitu, Bw Saseendran aliambia wanahabari.
"Uhamisho ni suluhisho la muda tu," alisema. "Hatuwezi kusema tembo huyo hatarudi Kerala."
Maafisa wa misitu huko Kerala bado wako macho iwapo Arikomban angejitosa karibu na mipaka ya jimbo hilo.
"Tembo wana uwezo mkubwa wa mazoea nyumbani," Bi Kartha asema. "Arikomban amekuwa akijaribu kurejea nyumbani tangu alipohamishwa kwa mara ya kwanza [mwezi Aprili]."
"Ikiwa atajaribu kurejea katika makazi ya watu, mrejeshe Kerala - hilo ndilo suluhisho pekee la kudumu," anasema












