Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ayman al-Zawahiri: Jinsi shambulizi la Marekani lilivyomuua kiongozi wa al-Qaeda - bila kugusa familia yake
Zaidi ya saa moja baada ya jua kuchomoza tarehe 31 Julai, mkuu wa muda mrefu wa kundi la al-Qaeda Ayman al-Zawahiri alitoka kwenye roshani ya eneo la katikati mwa jiji la Kabul - inaripotiwa kuwa amekuwa akifanya hivyo kila baada ya maombi .
Lingekuwa jambo la mwisho angefanya.
Saa 06:18 saa za ndani (01:38 GMT), makombora mawili yalirushwa kwenye roshani hiyo, na kumuua mzee huyo wa miaka 71 lakini kombora hilo likawaacha mkewe na bintiye ndani bila majeraha yoyote.
Uharibifu wote uliotokana na shambulio hilo ulifanyika tu kwenye eneo la balkoni hiyo .
Je kombora hilo lilikuwa na usahihi wa kiwango gani?
Siku za nyuma Marekani ilishutumiwa kwa kutekeleza mashambulizi ambayo yaliwaua raia wasio na hatia.
Lakini katika tukio hili, hivi ndivyo jinsi aina ya kombora hilo lilivyo, na uchunguzi wa karibu wa tabia za Zawahiri, ulivyofanikisha shambulizi hilo - na kwa nini mashambulizi zaidi kama hayo huenda yakafuata.
Usahihi wa silaha ya teknolojia ya laiser
Aina ya kombora lililotumika lilikuwa muhimu - na haya yalisemwa na maafisa wa Marekani kuhusu kombora hilo la Hellfire - aina ya kombora linaloweza kurushwa kutoka angani hadi ardhini na ambalo ndilo ambalo limekuwa likitumika na Marekani katika siku za hivi karibuni kukabiliana na ugaidi ughaibuni miongo kadhaa tangu shambulizi la Septemba 11 2001 .
Kombora hilo linaweza kurushwa kutoka kwa majukwaa tofauti, ikiwa ni pamoja na helikopta, magari ya ardhini, meli au, kwa upande wa Zawahiri, kutoka kwa ndege isiyo na rubani.
Marekani inaaminika kutumia kombora la Hellfire kumuua jenerali wa Iran Qassem Soleimani huko Baghdad mapema mwaka wa 2020, na mwanajihadi wa Islamic State aliyezaliwa Uingereza anayejulikana kama "Jihadi John" nchini Syria mwaka 2015.
Miongoni mwa sababu kuu za matumizi ya mara kwa mara ya kombora la Hellfire ni usahihi wake.
Linaporushwa kutoka kwa ndege isiyo na rubani, mwelekezaji wa silaha - wakati mwingine akiwa amekaa kwenye chumba cha kudhibiti chenye kiyoyozi nchini Marekani - huona mtiririko wa video ya moja kwa moja ya shabaha, ambayo vihisi vya kamera ya droni hujibu kupitia satelaiti.
Kwa kutumia seti ya "mabano ya kulenga" kwenye skrini, mwelekezaji huyo wa kamera anaweza "kufunga" shabaha na kuelekeza laiser. Mara kombora linaporushwa, hufuata njia ya laiser hiyo hadi kugonga shabaha.
Kuna taratibu zilizo wazi na zinazofuatana ambazo wafanyakazi wanaoendesha ndege hiyo ni lazima wafuate kabla ya kuchukua hatua, ili kupunguza hatari ya vifo vya raia. Katika mashambulizi ya awali ya kijeshi ya Marekani au CIA, hii ilijumuisha kuwaita wanasheria wa kijeshi kwa mashauriano kabla ya amri ya kushambulia kutolewa.
Profesa William Banks, mtaalamu wa mauaji ya shabaha na mwanzilishi wa Taasisi ya Sera na Sheria ya Usalama ya Chuo Kikuu cha Syracuse, alisema kuwa maafisa wangelazimika kusawazisha hatari ya vifo vya raia na thamani ya mtu anayelengwa.
Shambulizi la Zawahiri, aliongeza, "linaonekana kama utumizi wa mfano" wa mchakato huo.
"Inaonekana walikuwa waangalifu sana na walikusudia katika tukio hili kumpata mahali na wakati ambapo wangeweza kumpiga yeye tu na wasimdhuru mtu mwingine yeyote," Prof Banks alisema.
Katika tukio la shambulizi la Zawahiri, imependekezwa, lakini haijathibitishwa, kwamba Marekani pia ilitumia toleo lisilojulikana la silaha ya Hellfire - R9X - ambalo linatumia kifaa cha kusidia kuongoza shabaha kwa kutumia nishati yake ya kinetiki.
Mnamo mwaka wa 2017, kiongozi mwingine wa al-Qaeda na mmoja wa manaibu wa Zawahiri, Abu Khayr al-Masri, aliripotiwa kuuawa kwa kombora la Helfire toleo la R9X nchini Syria.
Picha za gari lake zilizopigwa baada ya shambulizi hilo zilionyesha kuwa kombora hilo lilikuwa limetoboa shimo kwenye paa na kuwauwa watu waliokuwa ndani yake, lakini bila dalili za mlipuko au uharibifu wowote kwa gari hilo.
Jinsi Marekani ilivyofuatilia mienendo ya Zawahiri katika balkoni
Maelezo bado yanaibuka kuhusu taarifa za kijasusi ambazo Marekani ilikusanya kabla ya kutekeleza shambulio hilo la kabul.
Baada ya shambulio hilo, hata hivyo, maafisa wa Marekani walisema walikuwa na taarifa za kutosha kuelewa "mfumo wa maisha" wa Zawahiri katika nyumba hiyo - kama vile tabia yake ya balkoni.
Hii inaonyesha kwamba wapelelezi wa Marekani walikuwa wakiitazama nyumba hiyo kwa wiki, ikiwa sio miezi.
Marc Polymeropoulos, afisa mkuu wa zamani wa CIA, aliambia BBC kwamba kuna uwezekano kwamba mbinu mbalimbali za kijasusi zilitumika kabla ya shambulio hilo, ikiwa ni pamoja na majasusi waliokuwa ardhini na kuashiria taarifa za kijasusi.
Baadhi pia wamekisia kwamba ndege zisizo na rubani za Marekani au ndege zilichukua zamu kufuatilia eneo kwa wiki au miezi kadhaa, bila kusikika na kutoonekana kutoka chini chini.
"Unahitaji kitu ambacho kina uhakika kwamba ni mtu binafsi, na pia lazima kifanyike katika mazingira huru, kumaanisha hakuna majeruhi ya raia," alisema. "Inachukua uvumilivu mwingi."
Shambulizi la Zawahiri, Bw Polymeropoulos aliongeza, lilinufaika kutokana na uzoefu wa miongo kadhaa ya jumuiya ya kijasusi ya Marekani kufuatilia watu binafsi wa al-Qaeda na shabaha zingine za kigaidi.
"Sisi ni bora katika hili. Ni jambo ambalo serikali ya Marekani imefanikiwa sana kwa zaidi ya miaka 20," alisema. "Na Wamarekani wako salama zaidi kwa hilo."
Walakini, shughuli za Marekani za aina hii haziendi kila wakati kulingana na mpango. Mnamo tarehe 29 Agosti 2021, shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye gari kaskazini mwa uwanja wa ndege wa Kabul, lililolenga kushambulia tawi la ndani la kundi la Islamic State, liliua watu 10 wasio na hatia badala yake. Pentagon ilikubali kwamba "kosa la kutisha" lilikuwa limefanywa.
Bill Roggio, afisa mwandamizi katika Taasisi ya Kutetea Demokrasia ambaye amekuwa akifuatilia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani kwa miaka mingi, alisema kwamba huenda shambulio la Zawahiri lilikuwa "gumu zaidi" kuliko mauaji ya awali kutekeleza, kutokana na kutokuwepo kwa serikali ya Marekani au mali iliyo karibu.
Mashambulizi ya zamani ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Pakistan iliyo karibu, kwa mfano, yalisafirishwa kutoka Afghanistan, wakati mashambulizi dhidi ya Syria yangefanywa kutoka maeneo rafiki nchini Iraq.
"[Katika maeneo hayo] ilikuwa rahisi zaidi kwa Marekani kufikia maeneo hayo. Hii ilikuwa ngumu zaidi," alisema. "Hili ni shambulizi la kwanza dhidi ya al-Qaeda au Islamic State nchini Afghanistan tangu Marekani kuondoka. Hili si jambo la kawaida.
‘’Je hili linaweza kufanyika tena?’’
Bw Roggio alisema "hatashangaa" ikiwa mashambulizi kama hayo dhidi ya malengo ya al-Qaeda yatafanyika tena Afghanistan.
"Hakuna uhaba wa malengo," alisema. "Kuna uwezekano viongozi wafuatao [wa al-Qaeda] huenda wakahamia Afghanistan, kama hawapo tayari."
"Swali ni iwapo Marekani bado ina uwezo wa kufanya hivyo kwa urahisi, au itakuwa mchakato mgumu?" aliongeza.