Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waandishi wa BBC wanajibu maswali yako kuhusu mzozo wa Israel na Hamas
Ni wiki tatu zimepita tangu Hamas ilipofanya shambulizi ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini Israel na kuua watu 1,400. Israel imelipiza kisasi kwa mashambulizi makali ya makombora kwenye Ukanda wa Gaza - wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema zaidi ya watu 5,000 wameuawa.
Viongozi wa nchi za Magharibi wamekuwa wakizuru Israel kuonyesha uungaji mkono wao kwa nchi hiyo - na kuwaomba viongozi wa Israel kuzingatia sheria za kimataifa na kuwalinda raia huko Gaza. Uvamizi wa ardhini wa Gaza unatarajiwa, ingawa haijuulikani lini hilo litafanyika.
Waandishi wetu wanaofuatilia mzozo huo, wanajibu maswali yaliyowasilishwa na wasomaji wa BBC - unaweza kusoma majibu yao hapa chini.
Kuna uwezekano wa vita vikubwa zaidi kuzuka?
Paul Adams, mwandishi wetu wa diplomasia, akiwa Jerusalem, anasema:
Jambo kubwa linalotia wasiwasi ni mpaka wa kaskazini mwa Israel, kurushiana makombora kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wenye nguvu wa Shia wa Lebanon, Hezbollah, kumeongezeka siku baada ya siku.
Israel imepeleka wanajeshi na silaha mpakani na kuchukua hatua ya kuwahamisha makumi ya maelfu ya raia kutoka katika jamii zilizo hatarini za mpakani.
Hezbollah inaungwa mkono na Iran, ambayo imeonya huenda ikalazimika kuingilia kati ikiwa hali ya Gaza itaendelea kuwa mbaya.
Kwa Israel, maghala ya makombora ya Hezbollah ni tishio zaidi kuliko yale ya Hamas.
Marekani imetuma meli za kivita zenye ndege za kivita mashariki mwa Mediterania kama ishara kwa Hezbollah na Iran kukaa mbali na mzozo huo.
Lakini wakati ghasia zinazidi kupamba moto, bado haionekani kwamba Hezbollah imechukua uamuzi wa moja kwa moja wa kujiunga na vita.
Je, kuna chakula, umeme na mafuta yanayoingia Gaza?
Mwandishi wa Mashariki ya Kati Tom Bateman, huko Jerusalem, anajibu:
Israel ilisema inaweka mzingiro kamili Gaza. Waziri wa Nishati, Israel Katz alisema baada ya mashambulizi ya Hamas hakutakuwa na usambazaji wa umeme au maji hadi mateka waachiliwe."
Tangu mwaka 2006, Israel imeweka vizuizi vikali Gaza, ikiungwa mkono na Misri, baada ya Hamas kuimarisha udhibiti wake katika eneo hilo. Israel ilisema vizuizi hivi ni kuzuia vifaa vya kutengenezea silaha kuingia.
Lakini vizuizi hivyo vilichangia maisha kwa raia wa kawaida kuwa magumu kwani Israel na Misri wanadhibiti kila kitu kilichoingia na kutoka; isipokuwa kile kinachofika Gaza kupitia njia za magendo kutoka Misri.
Kwa sasa hakuna njia ya kufikisha mahitaji isipokuwa yale malori machache ya misaada yanayovuka mpaka kutoka Misri tangu Jumamosi na Israel imeruhusu maji ya bomba saa chache kwa siku mashariki mwa Khan Younis.
Inamaanisha vyanzo pekee vilivyobaki vya nishati na maji ya kunywa ndani ya Gaza ni akiba ya kabla ya mzozo huu - ikiwa ni pamoja na dizeli ya jenereta kutoka watu binafsi, akiba ya maji ya chupa na visima vya watu binafsi - maji ambayo mara nyingi huchafuliwa na yanahitaji kuchujwa.
Je, Israel itaweza kuwaokoa mateka?
Mwandishi wa masuala ya usalama, Frank Gardner anasema:
Kwa sababu ya idadi kubwa ya mateka wanaoshikiliwa Gaza - zaidi ya 200 - uwezekano wa Israeli kuwaokoa wote kwa nguvu sio mkubwa.
Kama tunavyojua, mateka wawili waliachiliwa Ijumaa iliyopita baada ya upatanishi na Qatar - na wengine wawili waliachiliwa Jumatatu.
Qatar inaamini mateka zaidi wataachiliwa lakini baadhi ya watu wanadhani hii inaweza kuwa mbinu ya Hamas ya kuizuia Israel kufanya uvamizi wa ardhini.
Israel ina utaalamu mwingi katika uokoaji wa mateka kupitia Kikosi Maalumu, Sayaret Matkal, kimepata mafunzo ya kina kwa operesheni kama hiyo.
Lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa. Baadhi au mateka wote kuna uwezekano wanashikiliwa kwenye mahandaki ya chini ya ardhi, katika baadhi ya matukio wakihamishwa kutoka eneo moja la siri hadi jingine.
Ikiwa watekaji wao watadhani mateka wao wako karibu kuokolewa wanaweza kuwaua. Kwa hivyo, operesheni yoyote ya uokoaji itakuwa hatari sana.
Hamas wanapata wapi pesa?
Yolande Knell, mwandishi wa Mashariki ya Kati huko Jerusalem, anasema:
Katika siku zake za mwanzo, Hamas ilifadhiliwa na baadhi ya Wapalestina kutoka nje na wafadhili binafsi, hasa katika Ghuba ya Kiarabu. Baadhi ya taasisi za Kiislamu pia zilituma pesa.
Vyanzo hivyo vya ufadhili vilianza kukwama baada ya Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine, kuliweka kundi hilo katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Hamas sasa inapokea msaada wa vifaa na fedha kutoka Iran.
Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na hali mbaya ya kiuchumi huko Gaza, Qatar - ambayo hutoa misaada kwa eneo la Palestina - imeruhusiwa kusaidia kulipa mishahara kwa maelfu ya wafanyakazi wa serikali huko Gaza.
Hazina ya Marekani pia inasema Hamas ina hazina ya siri ya uwekezaji wa kimataifa, ambayo inazalisha kiasi kikubwa cha pesa na mali yake inakadiriwa kuwa na thamani ya mamilioni ya dola, kutokana na makampuni yanayofanya kazi nchini Sudan, Algeria, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine.
Je, nchi za Magharibi zitatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano?
Paul Adams anajibu:
Idadi ya vifo kufikia sasa, zaidi ya Waisraeli 1,400 wameuawa na zaidi ya Wapalestina 5,000, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas wameuawa.
Kutokana na uzoefu wangu, nchi za Magharibi zinairuhusu Israel kuiadhibu Hamas kabla ya kuanza kutoa wito wa kusitishwa mapigano. Serikali za Magharibi kwa ujumla zinaunga mkono Israel kuwaadhibu Hamas.
Lakini Israel hailengi kuwaadhibu tu Hamas - wakati huu imedhamiria kulitokomeza kabisa vuguvugu hilo kisiasa na kijeshi.
Hilo litasababisha mateso makubwa kwa raia, na kwa kuzingatia uungaji mkono wa Magharibi - licha ya onyo la Joe Biden kwa Israel kutochukua hatua kwa hasira - inaonekana, Israel itaweza kutimiza malengo yake kabla washirika wake hawajasema imetosha.
Je, Fatah itaendesha tena Gaza?
Yolande Knell anajibu:
Fatah ni mrengo wa kisiasa usio wa kidini na ni mshindani mkuu wa Hamas.
Kiongozi wa Fatah ni Rais Mahmoud Abbas - anaongoza Mamlaka ya Palestina (PA) ambayo inasimamia sehemu za Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Yeye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina (PLO) - kundi linalotambuliwa kimataifa kuwawakilisha watu wa Palestina.
Hamas na Islamic Jihad si sehemu ya PLO, ambayo imeingia katika upatanishi katika duru zilizopita za mazungumzo ya moja kwa moja ya amani na Israel.
PA ilitawala Gaza lakini Hamas ilichukua udhibiti kamili mwaka 2007, na kuviondoa vikosi vya usalama vya PA katika vita vya umwagaji damu mitaani. Iikuwa ni mwaka mmoja baada ya Hamas kushinda uchaguzi wa wabunge.
Tuliona Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akikutana na Rais Abbas alipotembelea eneo hilo baada ya vita vya Gaza kuanza.
Wiki iliyopita, nilikutana na Sabri Saidam, waziri wa zamani wa PA, ambaye ni afisa mkuu wa Fatah na yuko karibu na Abbas. Nilimuuliza kama PA iliombwa kurudi Gaza baada ya vita hivi.
Aliniambia: "Israel inataka kujadili hali ya baadaye, Marekani inataka kujadili hali ya baadaye. Uongozi wa Palestina uko wazi kabisa - hautaidhibiti Gaza na watu wa Gaza kwa msaada wa vifaru vya Israeli."
Je, serikali za Magharibi zina mstari mwekundu kwa Israel?
Frank Gardner anajibu:
Hakuna msimamo mmoja wa pamoja kwa nchi za Magharibi juu ya mzozo huu, kama vile msimamo wa Nato juu ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka jana.
Unyama na ukatili mkubwa wa shambulio la Hamas dhidi ya raia kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba ulimaanisha - viongozi wengi wa nchi za Magharibi watakimbilia kuinga mkono Israel kikamilifu.
Hata hivyo, mashambulizi ya anga ya kulipiza kisasi ya Israel yameivuruga Gaza, na kusababisha vifo vingi vya raia, kuna wasiwasi unaoongezeka miongoni mwa marafiki wa Israel kwamba serikali ya Netanyahu inachupa mipaka.
"Usipofuliwe na hasira kama zilivyoipofua Marekani baada ya shambulio la Septemba 11," ni ujumbe Rais Biden alioutoa Israel wakati wa ziara yake fupi juma lililopita.
Viongozi wote wa nchi za Magharibi wameitaka Israel kutokiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, lakini mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaishutumu Israel kushambulia kwa makombora maeneo yenye watu wengi na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni moja kuondoka makwao.