Je, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anatoa dalili gani kwa kumuonesha bintiye mbele ya ulimwengu?

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza akiwa na bintiye.

Pamoja na hayo, uvumi wa muda mrefu kuhusu yeye kuwa na binti pia umethibitishwa.

Siku ya Ijumaa wiki iliopita, wakati Kim Jong alipokagua kurushwa kwa kombora la masafa marefu, binti yake pia alikuwa pamoja naye. Inaaminika kuwa jina la bintiye ni Kim Chu Aye.

Baba na binti walisimama pamoja wakiwa wameshikana mikono wakati wa jaribio la kombora. Marekani imelikosoa jaribio hilo la kombora.

Korea Kaskazini ni mojawapo ya mataifa ya ajabu duniani na hakuna habari nyingi kuhusu maisha ya kibinafsi ya kiongozi wake Kim Jong Un.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA limechapisha picha za Kim Jong Un na bintiye wakiwa wameshikana mikono. Wote wawili walionekana wakizungumza na viongozi, wakikagua makombora na kutazama kurushwa kwa kombora kutoka kwa jumba la kutazamia.

Uchambuzi wa Jean Mackenzie.. Mwandishi wa habari wa Seoul

Siku ya Ijumaa, Korea Kaskazini ilifanyia majaribio ya kombora lake lenye nguvu zaidi la masafa marefu ambalo linaaminika kuwa na uwezo wa kufika Marekani.

Lakini wachambuzi waliokuwa wakifuatilia Korea Kaskazini walipendezwa zaidi na picha ya Kim akiwa na binti yake kuliko jaribio la kombora.

Kwa nini? Kwa sababu inasema mengi kuhusu mustakabali wa nguvu za Korea Kaskazini na mpango wake wa nyuklia. Au angalau inazua maswali mengi ya kuvutia.

Kwanza, je amechaguliwa kuwa mrithi wa Kim Jong Un na siku moja ataiongoza Korea Kaskazini? Hili linawezekana sana. Hii ni nasaba ya familia. Hii ina maana kwamba Kim angependa mmoja wa watoto wake kuchukua mamlaka ya nchi baada yake.

Pili, kwa nini ililetwa duniani sasa hivi tu? Msichana huyo bado ni mdogo sana. Ikiwa wanamtayarisha kuchukua wadhifa huo, ina maana kwamba Kim Jong Un mwenye umri wa miaka 38 anaugua ugonjwa mbaya?

Daima kumekuwa na uvumi kuhusu afya yake, na pia imeonekana kuwa afya yake ndiyo tishio kubwa kwa uthabiti wa mamlaka ya Korea Kaskazini.

Tatu, hii inaashiria nini kuhusu mpango wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini?

Kumleta mbele ya ulimwengu wakati wa jaribio la kufyatua kombora inamaanisha kuwa siku moja atakuwa na jukumu muhimu katika utengenezaji wa silaha za Korea Kaskazini. Hivi majuzi, Kim Jong Un alisema kwamba hataachana na mpango wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini kwa hali yoyote ile.

Hii pia ni njia yao ya kuonyesha ulimwengu kuwa silaha zao za nyuklia zitabaki, kizazi baada yao pia kitazishughulikia.

Kizazi cha nne cha Kim

Michael Madden, mtaalamu wa Korea Kaskazini katika Kituo cha Stimson huko Washington, aliiambia BBC kwamba alikadiria bintiye Kim kuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 13.

Anasema kwamba kwa kumtoa binti huyo hadharani, Kim anapaswa kuonyesha ulimwengu kwamba "kizazi cha nne kitatoka kwa damu yangu."

Mnamo Septemba, wataalamu wengi waliokuwa wakifuatilia Korea Kaskazini walisema kwamba Kim Chu Aye pia alionyeshwa wakati wa sherehe za Siku ya Kitaifa ya Korea Kaskazini.

Lakini hii ilikuwa ni uvumi tu, na haikuthibitishwa na maafisa wa Korea Kaskazini.

Fahamu familia ya Kim

Kuwepo kwa bintiye Kim kulifichuliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2013 wakati mchezaji wa mpira wa vikapu mwenye utata kutoka Marekani Dennis Rodman aliposafiri kwenda Korea Kaskazini.

Rodman alisema alikuwa ametumia muda wake mwingi na familia ya Kim katika ufuo wa bahari na "alimshikilia Choo Aye," binti yao.

Wataalamu wanaamini kwamba Kim anaweza kuwa na watoto watatu - binti wawili na wa kiume, huku Chu akiwa mkubwa.

Lakini kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un haruhusu taarifa zozote kuhusu familia yake kufichuliwa na amekuwa akiweka familia yake kuwa siri.

Hata habari kuhusu mkewe Ri Sol Joo haikuruhusiwa kutoka hadi muda mrefu baada ya ndoa.