Lula amshinda Bolsonaro katika uchaguzi mkuu Brazil

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Lula da Silva

Taifa la Brazil limechukua mkondo wa kushoto huku rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva akimshinda Jair Bolsonaro katika uchaguzi wa rais.

Baada ya kampeni ya mgawanyiko ilioshuhudia wapinzani wawili wa pande tofauti za wigo wa kisiasa wakipambana, Lula alishinda kwa 50.9% ya kura.

Ilitosha kumshinda Jair Bolsonaro, ambaye wafuasi wake walikuwa na uhakika wa ushindi.

Lakini mgawanyiko ambao uchaguzi huu umeangazia hauwezi kutoweka.

Ni jambo la kustaajabisha kwa mwanasiasa ambaye hangeweza kugombea katika uchaguzi uliopita wa urais mwaka wa 2018 kwa sababu alikuwa gerezani ambapo alikuwa amepigwa marufuku kugombea wadhifa huo.

Alikuwa amepatikana na hatia ya kupokea hongo kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya Brazil kama malipo ya kandarasi na kampuni ya mafuta ya serikali ya Brazil Petrobras.

Lula alikaa gerezani kwa siku 580 kabla ya hukumu yake kubatilishwa na akarejea kwenye siasa.

"Walijaribu kunizika nikiwa hai na niko hapa," alisema, akianzisha hotuba yake ya ushindi.

Vitu 5 muhimu kuhusu Lula

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Lula alimkumbatia mkewe Rosangela baada ya ushindi wake
  • Umri wa miaka 77
  • Mrengo wa kushoto
  • Mfanyikazi wa zamani wa kampuni ya chuma
  • Rais 2003-2010
  • Alifungwa 2018 lakini akaondolewa hatia baadaye
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kura za maoni zilipendekeza tangu mwanzo kwamba angeshinda uchaguzi huo, lakini wakati uongozi wake katika duru ya kwanza ulikuwa mwembamba kuliko ilivyotabiriwa, Wabrazili wengi walianza kutilia shaka usahihi wao.

Wafuasi wa Jair Bolsonaro - waliotiwa moyo na madai ya mgombea wao kwamba vyombo vya habari vilikuwa dhidi yake walikuwa na imani kamili katika ushindi wake.

Ushindi huo wa viongozi wa mrengo wa kushoto huenda ukawakutanisha mashabiki hawa wa Bolsonaro, ambao mara kwa mara humtaja Lula kuwa "mwizi" na kusema kuwa kubatilishwa kwa hukumu yake hakumaanishi kwamba hakuwa na hatia, bali tu kwamba utaratibu ufaao wa kisheria haukufuatwa.

Na wakati Jair Bolsonaro ameshindwa, wabunge wa karibu naye walipata kura nyingi katika bunge la Congress, ambayo ina maana kwamba Lula atakabiliwa na upinzani mkali kwa sera zake katika chombo cha kutunga sheria.

Lakini Lula, ambaye alihudumu mihula miwili ofisini kati ya Januari 2003 na Desemba 2010, si mgeni katika kuunda miungano ya kisiasa.

Kama mgombea mwenza wake wa makamu wa rais alimchagua mpinzani wa zamani Geraldo Alckmin, ambaye alishindana na Lula katika chaguzi zilizopita.

Mkakati wake wa kuunda tikiti ya "umoja" inaonekana kuwa umeleta matunda na kuwavutia wapiga kura kwenye kundi ambalo huenda hawakufikiria kupigia kura Chama chake cha Wafanyakazi.

Katika hotuba yake ya ushindi, aligusia sauti ya maridhiano, akisema atatawala kwa ajili ya Wabrazil wote na sio tu wale waliompigia kura.

"Nchi hii inahitaji amani na umoja. Idadi hii ya watu hawataki kupigana tena," alisema.

Jair Bolsonaro bado hajakubali. Kampeni hiyo kwa kiasi fulani ilikuwa ya mvutano kwa sababu rais wa mrengo mkali wa kulia alitilia shaka - bila kutoa ushahidi wowote - juu ya kutegemewa kwa mfumo wa upigaji kura wa kielektroniki wa Brazil.

Hili lilizua hofu kwamba huenda asikubali matokeo ikiwa yataenda kinyume chake.

Siku moja kabla ya duru ya pili hata hivyo, alisema kwamba: "Hakuna shaka hata kidogo. Yeyote aliye na kura nyingi, anachukua [uchaguzi]. Hiyo ndiyo demokrasia."

Mambo 5 muhimu kuhusu Bolsonaro

.

Chanzo cha picha, Reuters

  • Umri wa miaka 67
  • Mrengo wa kulia
  • Kapteni wa zamani wa jeshi
  • Amewania kwa muhula wa pili mfululizo
  • Ametilia shaka uaminifu wa mfumo wa kupiga kura wa kielektroniki wa Brazili

Siku yenyewe ya uchaguzi, mabasi yaliyokuwa yamewabeba wapiga kura kwenda kupiga kura yalizuiliwa na polisi katika kile ambacho kampeni ya Lula ilisema ni jaribio la kuwazuia kupiga kura.

Mkuu wa mahakama ya uchaguzi, Alexandre de Moraes, aliamuru polisi wa barabara kuu kuondoa vizuizi vyote vya barabarani .

Alisema kuwa wakati baadhi ya wapiga kura wamecheleweshwa, hakuna aliyezuiwa kupiga kura. Lakini matukio hayo yaliibua mvutano mkubwa.

Sasa kuna matarajio mengi kuhusu lini na nini Bw Bolsonaro atasema sasa kwa kuwa ni rasmi kwamba kura chache zilipigwa kwa ajili yake kuliko Lula.

Uchaguzi huo haujafuatiliwa kwa karibu tu nchini Brazil, bali pia nje ya nchi, huku wanaharakati wa mazingira wakiwa na wasiwasi hasa kwamba miaka mingine minne ya serikali ya Bolsonaro ingesababisha ukataji miti zaidi katika msitu wa Amazon.

Lula alirejelea hofu hizi katika hotuba yake ya ushindi akisema kuwa "yuko wazi kwa ushirikiano wa kimataifa kulinda Amazon".

"Leo tunauambia ulimwengu kuwa Brazil imerejea. Ni kubwa mno kufukuzwa kwenye jukumu hili la kusikitisha la kutengwa kimataifa," aliongeza katika kumchambua mpinzani wake.

Lakini kiini cha hotuba yake ilikuwa ahadi ya kukabiliana na njaa, ambayo imekuwa ikiongezeka nchini Brazil na ambayo inaathiri zaidi ya milioni 33.

Jambo kuu kwa umaarufu wa Lula wakati wa mihula yake miwili ya kwanza ofisini ilikuwa ni kuwaondoa mamilioni ya Wabrazili kutoka kwenye umaskini.

Lakini katika uchumi wa baada ya janga, kupata fedha za kuweka mkatakati kama haitakuwa kazi rahisi, haswa iwapo atapata upinzani kutoka bungee la Congress.