Kundi la Waislamu ambao hawafungi wala kuswali swala tano

gfv

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Rukia Bulle
    • Nafasi, Mshindi wa Tuzo ya Komla Dumor
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Jioni inapoingia katika kijiji cha Mbacke Kadior, katikati mwa Senegal, nyimbo zenye mahadhi za waumini wa dini ya Kiislamu waliovalia mavazi yenye mabaka mabaka, huimbwa.

Wakiwa wamekusanyika kwenye mduara nje ya msikiti, wafuasi wa Baye Fall wanayumba na kuimba huku miale ya moto ukitoa vivuli.

Nyimbo hizo zinaweza kudumu kwa saa mbili - na hufanyika mara mbili kwa wiki. Baye Fall, kikundi kidogo cha wana ndugu wa Mouride, ni tofauti na kundi jingine lolote la Waislamu.

Wanaunda sehemu ndogo ya wakazi milioni 17 nchini Senegal, nchi yenye Waislamu wengi Afrika Magharibi. Na matendo yao yasiyo ya kawaida yanaaminiwa na wengine kuwa yanakwenda kinyume kabisa na kanuni za Uislamu.

Pia unaweza kusoma

Imani za Baye Fall

trfg
Maelezo ya picha, Huko Mbacke Kadior watu hutengeneza nguo za viraka na wengine hufanya kazi za kilimo

Kwa wafuasi wa Baye Fall, imani haionyeshwi kupitia swala tano za kila siku au kufunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kama Waislamu wengi wanavyofanya, lakini huonyeshwa kupitia bidii ya kufanya kazi na kutoa huduma kwa jamii. Kwa mtazamo wao, mbinguni si mahali pa kuishi tu bali ni zawadi kwa wale wanaofanya kazi kwa bidii.

Mara nyingi hawaelewani na Waislamu wengine - na pia kuna dhana potofu kwamba wengine hunywa pombe na kuvuta bangi, mambo ambayo si sehemu ya maadili yao.

"Falsafa ya Baye Fall inajielekeza katika kazi. Ambapo kazi yenyewe inakuwa ni sehemu ya kujitolea kwa ajili ya Mungu," anasema Maam Samba, kiongozi wa kundi la Baye Fall huko Mbacke Kadior.

Wanaamini kila kazi - iwe kulima mashamba chini ya jua kali, kujenga shule, au kutengeneza bidhaa - ina umuhimu wa kiroho. Kwao kazi ni tendo la kiroho, na ni aina ya ibada.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika kijiji cha Mbacke Kadior, jamii hii inaamini mwanzilishi wao ni Ibrahima Fall, wanaamini alikutana na Sheikh Ahmadou Bamba, aliyeanzisha udugu wa Mouride katika Karne ya 19, tawi la Uislamu wa Sufi, ambao una wafuasi wengine nchini Senegal.

Fall inasemekana alijitolea moja kwa moja kumhudumia Bamba na mara nyingi alipuuza mahitaji yake mwenyewe, ikiwa ni pamoja na kula, kufunga, kusali na kujitunza.

Wafuasi wake wanasimulia kwamba baada ya muda nguo zake zilichakaa na kutiwa viraka, dalili ya kujitolea kwake. Hivi ndivyo falsafa ya Baye Fall na mila ya mavazi yenye viraka ilivyotokea.

Wanawake na wanaume hufanya kazi kwa umakini wa utulivu ya kushona nguo zao. Vipande hivi vinapokamilika husambazwa katika masoko kote Senegal.

"Mtindo wa Baye Fall ni wa asili," anaeleza Bw Samba, ambaye marehemu baba yake alikuwa sheikh anayeheshimiwa wa Baye Fall, au marabout kama viongozi wa kidini wanavyojulikana nchini Senegal.

Waislamu wanapofunga kutoka asubuhi hadi jioni wakati wa Ramadhani, Baye Fall wao hujitolea kuandaa chakula kwa ajili ya mlo wa jioni wa futari wakati mfungo misikitini.

Kujitolea huku sio tu kwa kazi za mikono. Baye wameanzisha vyama vya ushirika, biashara za kijamii, na mashirika yasiyo ya kiserikali yenye lengo la kukuza maendeleo katika maeneo ya vijijini ya Senegal. Kwao, kazi si njia ya kuishi tu bali ni tendo la kiroho.

"Tuna shule, vituo vya afya na mashirika ya kijamii ili kuunda kazi," anaeleza Samba. "Katika falsafa yetu ya maisha, kila kitu lazima kifanywe kwa heshima, upendo, na umakini."

Baye Fall halisi na wa uongo

RF

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Takriban watu 700,000 ni wafuasi wa Baye Fall

Lakini kundi hilo pia limepokea shutuma kwa tabia yake ya kuomba omba mitaani. Ingawa kuomba fedha si kinyume na mfumo wa imani wa Baye Fall, kwa kawaida hufanywa kwa nia ya kuchukua michango hiyo na kuipeleka kwa kiongozi, ambaye anaigawa upya kwa manufaa ya jamii.

"Kuna Baye Fall halisi na Baye Fall wa uongo," anasema Cheikh Senne, makamu mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Alioune Diop katika mji wa Bambey na mtaalamu wa udugu wa Mouride.

"Katika miji mikubwa kama mji mkuu, Dakar, vituo vya uongo vya Baye Ball vimeenea. Hawa ni watu wanaovaa kama sisi na kuanza kuomba omba barabarani lakini hawachangii katika jamii. Ni suala zito linaloharibu sifa yetu," anasema Senne.

Kazi ni jibu la mahitaji ya kiuchumi

TF

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baye Fall nje ya Msikiti wa Grande katika mji mtakatifu wa Touba

Msisitizo wa Baye Fall juu ya kufanya kazi kwa bidii na kufanya shughuli za kijamii umekwenda nje ya mipaka ya Senegal.

Miongoni mwa wafuasi wao ni Keaton Sawyer Scanlon, Mmarekani ambaye alijiunga na jumuiya hiyo baada ya kutembelea mwaka 2019. Tangu wakati huo amepewa jina la Kisenegali Fatima Batouly Bah.

"Moyo wangu ulitambua ukweli. Huu ulikuwa mwamko mkubwa wa kiroho kwangu," ameiambia BBC.

Bi Bah sasa anaishi miongoni mwa Baye Fall, akishiriki katika miradi yao na kufuata maadili yao. Yeye ni sehemu ya idadi ndogo lakini inayoongezeka ya wafuasi wa kimataifa ambao wamekubali njia ya kikundi hiki.

Baye Fall wana jukumu kubwa katika jamii ya Senegal na ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za kilimo na kiuchumi.

Kila mwaka wanaapa utii kwa kiongozi wa sasa wa Mouride, anayejulikana kama khalifa au marabout mkuu, kwa kutoa pesa, ng'ombe na mazao ili kuonyesha uaminifu wao.

Pia wanautunza Msikiti wa Grande katika mji mtakatifu wa Senegal wa Touba, kitovu cha udugu wa Mouridism - na wanasimamia msikiti huo.

Huko Touba wanatumika kama walinzi wasio rasmi katika Msikiti wa Grande wakati wa hafla kubwa, kama hija ya kila mwaka ya Magal, pale maelfu ya watu wanapokuja mjini.

Kwa mfano, wanahakikisha watu wamevaa mavazi ya kujisitiri, hakuna dawa za kulevya zinazouzwa katika eneo hilo na Khalifa hadharauliwi.

"Baye Fall huhakikisha usalama wa khalifa na jiji," anasema Senne. "Hakuna mtu anayethubutu kutenda isivyofaa wakati Baye Fall wako karibu."

Licha ya kutokukubalika na baadhi ya watu, athari za Baye Fall katika mazingira ya kitamaduni na kidini ya Senegal zinaongezeka - ingawa wanakabiliwa na changamoto katika kutunza mila na usasa.

Uhaba wa rasilimali hutatiza mipango yao. Hata hivyo maono yao yanabakia kuwa wazi: maendeleo endelevu, yanayotokana na imani na huduma kwa jamii, ambayo yanaweza pia kusaidia idadi kubwa ya vijana wasio na ajira nchini Senegal ambao wanakata tamaa ya kupata riziki.

Maelfu ya wahamiaji wanaovuka bahari hatari kwenda Ulaya wanatoka Senegal.

Anasema Samba. "Tunataka kutengeneza ajira zaidi - kwa sababu vijana wanahitaji ajira hapa Senegal. Tunahitaji ushirikiano na serikali na mashirika ya kimataifa. Hili ndilo tumaini letu la siku zijazo."

Kwao, kufanya kazi kwa bidii ni jibu la mahitaji ya kiuchumi na ya kiroho.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi