'Walikuwa wanatulazimisha kufanya matambiko wakati wa mazishi ya baba'

w

Chanzo cha picha, Anastasia Mukabwa

Anastasia Mukabwa, msanii kutoka Kenya ni jina tajika katika nchi za kanda ya Afrika Mashariki na Kati, lakini kile ambacho wengi hawakifahamu ni kuwa msanii huyu alilelewa katika maisha ya dhiki na taabu nyingi pindi baba yake mzazi alipofariki dunia akiwa na miaka 11.

Msanii huyu wa nyimbo za injili amepata umaarufu mkubwa kutokana na nyimbo zake zilizovuma kama ‘Kiatu kivue ‘ na watangoja sana miongoni mwa nyimbo nyingine kadhaa .

Mwanadada huyu alizaliwa katika Kaunti ya Busia , eneo la Budalang’i na baadaye wazazi wake walihamia mji wa Mombasa ambapo baba alikuwa anafanya kazi kama mhasibu.

Kando na hayo baba alikuwa ni mchungaji katika Kanisa moja mjini Mombasa kwa hiyo Anastacia alikulia kwenye mazingira ya ibada ya nyimbo za injili na anasema kuwa alianza kuimba nyimbo hizo akiwa bado binti mdogo.

“Mimi ni binti wa mchungaji na maisha yangu ya tangu utotoni yaliongozwa na maswala ya dini na wakati mwingi nilikuwa ninashughuli za kuimba kanisani ”anasema Anastasia.

w

Chanzo cha picha, Anastasia Mukabwa

Maelezo ya picha, Anastasia Mukabwa akiwa na mume wake

Kifo cha baba yake Anastasia

Mwanadada huyu anasema kwamba wakati baba yake alipoanza kuugua , walikuwa wamezaliwa wakiwa kaka na dada watano , japo mama yake alikuwa mjamzito wakati huo.

Mahangaiko ya kufahamu ni ugonjwa gani uliokuwa ukimhangaisha baba yaliwatembeza katika hospitali nyingi, lakini hatimaye alifariki. Akiwa ndio tegemeo katika jamii yake Anastasia anaeleza kuwa kilikua kipindi kigumu ambacho kilianza pindi baba alipofariki .

Mipango ya mazishi ilianza upande wa Mombasa washiriki wa Kanisa la baba waliandaa kwa namna yao , ila pia nyumbani kijijini kwa akina Anastasia alikozaliwa baba Kaunti ya Busia familia ilikuwa inaendeleza shughuli za matanga.

Mazishi yalipangwa kufanyika kijijini ambako mama yake Anastasia na ndugu zake waliusindikiza mwili wa baba yao hadi huko.

w

Chanzo cha picha, Anastasia Mukabwa

Maelezo ya picha, Anastasia Mukabwa ni muimbaji maarufu wa nyimbo za injili

'Vuta nikuvute mazishini'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Msanii huyu anasema kuwa baadhi ya watu katika familia yake walikuwa na maoni tofauti kuhusu jinsi baba yao angepewa buriani yake ya mwisho. Iliibuka kuwa ni lazima kungefanywa matambiko ya kimila kama njia ya kuwa ‘takasa’ – ni hali ambayo haikuambatana na Imani ya mama yake Anastasia na kwa hiyo alisimama kidete na kukataa kat kata kujihusisha na matambiko.

Kulingana na mwanadada huyu ni hali ambayo ilileta vurumai na hali ya mshikemshike katika kijiji chao cha Ikhula, huku baadhi ya watu wa karibu katika jamii wakilazimisha mama na watoto kuwa kwenye matambiko.

Hatimaye ilionekana kuwa hawangeweza kuwashurutisha, na baba yao aliishia kuzikwa huku wakiwa wametengwa. Japo anasema kuwa ni mama aliyedhulumiwa na kutukanwa kwa kutaa kushiriki katika matambiko hayo, ‘’wengi walimuona kama ndie aliye muua baba yetu na ndio maana alikataa kushiriki mila hizo’’, anasema .

“Kabla ya kumzika baba, walikuwa wameleta kisahani kilichokuwa na damu , na walikuwa wanasukuma sisi wote tuilambe, ni mama aliyetoa sauti na kutukataza kukaribia sahani ile”, anakumbuka Anastasia

Siku kadhaa baada ya baba yao kuzikwa, mama alipata uchungu wa uzazi na kwa kuwa kulikuwa kuna hali ya kutosikilizana , Anastasia anasema kuwa mama aliishia kujifungua mtoto pekee yake nyuma ya nyumba yao usiku wa manane.

Usiku huo huo mama yake Anastasia aliwashurutisha waondoke kwa njia yoyote warejee Mombasa kwani alihisi kana kwamba hakuna aliyekuwa anawapenda pale kijijini , na pia alikuwa na wasiwasi kuwa huenda wakamshurutisha kushiriki mila nyingine baada ya kujifungua.

Anastasia anasimulia jinsi usafiri ulivyokuwa shida , na anasema mama yao alikuwa na maumivu ya kujifungua na vilevile hakuwa na nauli ya kutosha kwa watoto wote kurejea Mombasa.

Licha ya mahangaiko mengi walipata wasamaria wema waliogharamia nauli yao wakaweza kusafiri hadi mji wa Mombasa.

‘Maisha ya tabu Mombasa’

Kurejea katika Kaunti ya Mombasa , kulimaanisha kuwa bila baba maisha yangebadilika - jamii iliyokuwa imezoea kula minofu sasa ilianza kuhangaika .

Anastasia anakumbuka akiandamana na ndugu yake hadi soko la Kongowea , kutafuta mabaki ya chakula yeyote kutoka kwa wachuuzi, anasema wakati mwingine hali ingelazimu kuokota hata nyanya zilizooza , mboga zilizobadilisha rangi na kadhalika ili mradi wapate kitu cha kula kwa siku.

'Harakati za kuwa msanii tajika'

h

Chanzo cha picha, Anastasia Mukabwa

Maelezo ya picha, Anastasia Mukabwa anafahamika kwa wimbo maarufu ''Kiatu Kivue'' uliovuma ndani na nje ya Kenya

Anastasia alianza kuimba Kanisani mjini Mombasa , Pilka pilka za kuimba katika huduma mbali mbali zilimkutanisha ana kwa ana na msanii mwengine tajika Rose Muhando kutoka Tanzania. Rose aligundua kipaji cha uimbaji cha Anastasia na hapo hapo walikubaliana kufanya kazi pamoja.

Nyimbo za Anastasia kwa kibao cha cha pili alimshirikisha Rose Muhando na nyimbo hizo kuwa na umaarufu wa aina yake katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Vile vile Anastasia anasema kuwa urafiki wake na Rose umeendelea kwa miaka mingi baada ya hapo na Anastasia anasema ‘’ndie aliyempeleka Rose Muhando hospitalini na baadae aliwashirikisha waimbaji wenzake wakati wa dhiki ya kuugua kwa dada Rose hadi kupata nafuu’’.

Anastasia ni mama na ni mke na anaamini kuwa ni muhimu vijana kusaidiwa kuelewa vipaji vyao na kupata watu waliowatangulia katika talanta na vipaji vyao kwa mfano fani ya uimbaji hadi kuanza kuona matunda ya talanta hizo.

‘’Mtu yeyote asikate tamaa maishani jitume na umtegeme Mungu ipo siku Mungu atakufuta Machozi Anastasia Mukabwa’’ alikamisha mazunguzo yake na BBC.