Ales Bialiatski: Mshindi huyu wa tuzo ya amani ya Nobel ni nani hasa?

ALES BIALIATSKI

Chanzo cha picha, ALES BIALIATSKI/FACEBOOK

Ales Bialiatski ni mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu wa Belarus, ambaye kwa sasa anashikiliwa gerezani bila kufunguliwa kesi. Bw. Bialiatski, 60, ndiye mwanzilishi wa Kituo cha Haki za Kibinadamu cha Viasna (Spring) nchini humo, ambacho kilianzishwa mwaka 1996 ili kukabiliana na ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya mitaani na kiongozi wa kimabavu wa Belarus Alexander Lukashenko.

Viasna alitoa msaada kwa waandamanaji waliofungwa na familia zao, akiandika kuhusu mateso dhidi ya wafungwa wa kisiasa na mamlaka ya Belarus.

"Amejitolea maisha yake katika kukuza demokrasia na maendeleo ya amani katika nchi yake," alisema mkuu wa Kamati ya Nobel ya Norway, Berit Reiss-Andersen, akitangaza washindi watatu wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka huu.

Bw Bialiatski - ambaye amepokea tuzo nyingi za kimataifa za haki za binadamu - alikaa jela miaka mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kukwepa kulipa kodi ambayo amekuwa akikanusha kila mara mwaka wa 2011. Aliachiliwa huru mwaka wa 2014.

Bialiatski

Chanzo cha picha, ALES BIALIATSKI/FACEBOOK

Alikamatwa na kuzuiliwa tena mwaka wa 2021 kufuatia maandamano makubwa ya barabarani kuhusu kile wanaharakati wa upinzani wanasema kuwa uchaguzi ulikuwa na udanganyifu ambao ulimweka Bw Lukashenko mamlakani mwaka uliotangulia.

"Mamlaka za serikali zimejaribu mara kwa mara kumnyamazisha Ales Bialiatski," Bi Reiss-Andersen alisema.

"Licha ya matatizo makubwa binafsi, Bw Bialiatski hajajijipatia chochote katika kupigania haki za binadamu na demokrasia nchini Belarus," aliongeza.

Kabla ya kukamatwa kwake miaka miwili iliyopita, Bw Bialiatski alikosoa mamlaka za Belarus kupitia ukurasa wake wa Facebook kufanya kazi kitawala na kibabe. "Mamia ya maelfu ya waandamanaji kote Belarusi, na mamia [yao] wanazuiliwa, alisema."

Afya ya sasa ya Bw Bialiatski haijulikani. Mke wa mwanaharakati huyo, Natallia Pinchuk, alisema "alizidiwa na hisia".

Bwana Lukasjenko - anayetajwa na nchi za Magharibi kama dikteta wa mwisho dhidi ya Ulaya - ametawala Belarusi kwa mkono wa chuma tangu 1994.

Amekuwa akimruhusu Rais wa Urusi Vladimir Putin, mshirika wake wa karibu, kutumia eneo la Belarus kufanya mashambulizi mabaya ya makombora dhidi ya Ukraine, na kutuma wanajeshi wa ardhini wa Urusi na hifadhi ya silaha huko tangu uvamizi wa Moscow ulipoanza tarehe 24 Februari.

Nobel

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Pamoja na, Bw Bialiatski, Shirika la uhuru wa kiraia la Ukraine (CCL) ni moja ya washindi watatu wa pamoja wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka huu.

CCL ni mojawapo ya mashirika ya haki za binadamu nchini Ukraine, lilianzishwa mwaka wa 2007, wakati viongozi wa makundi ya haki za binadamu kutoka nchi tisa za baada ya Soviet walipoamua kuunda kituo cha usaidizi wa rasilimali za mipaka huko Kyiv.

Tangu kuanzishwa kwake, imefuatilia mateso ya kisiasa katika eneo la Crimea inayokaliwa kwa mabavu, peninsula ya kusini ya Ukraine iliyotwaliwa na Urusi mwaka 2014; iliweka kumbukumbu za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa vita katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine; na kuandaa kampeni za kimataifa za kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa wa Kremlin.

Baada ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022, CCL imejihusisha na juhudi za kutambua na kuweka kumbukumbu za uhalifu wa kivita wa Urusi dhidi ya raia wa Ukraine.

Katika tweet baada ya tangazo la Ijumaa, CCL ilisema "ni fahari kutunukiwa" Tuzo ya Amani ya Nobel.

Nobel

Chanzo cha picha, Reuters

Mshindi mwingine wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka huu ni shirika la kutetea haki za binadamu la Urusi, Memorial - ambalo lilifungwa na mamlaka za Urusi mapema mwaka huu.

Kwa zaidi ya miaka 30, Shirika hilo lilifanya kazi ya kuangazia mamilioni ya watu wasio na hatia waliouawa, kufungwa gerezani au kuteswa katika enzi ya utawala wa Sovieti.

Kazi yake ilikumbwa na misukosuko kutoka kwa mamlaka ya Urusi. Mwaka 2006 ilitahadharishwa, na mnamo 2014 iliongezwa kwenye orodha ya iliyoitwa "vibaraka wa kigeni" - orodha ya mashirika na watu binafsi ambao serikali inadai kupokea ufadhili kutoka nje ya nchi.

Kisingizio cha kulifunga kundi hilo ni kushindwa kuweka alama kwenye baadhi ya machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii kuweka neno "wakala wa kigeni", kwa mujibu wa sheria.

Mnamo Desemba 2021, Mahakama Kuu ya Urusi iliamuru Shirika hilo na matawi yake ya kanda kufungwa kwa sababu ilikuwa limekiuka sheria ya wakala wa kigeni ya 2012.

Kulikuwa na kelele za "aibu!" kutoka kwa walio mahakamani wakati uamuzi huo ukisomwa.