Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Katika mlipuko mmoja, Khalil Khader alipoteza watoto wake wote
- Author, Fergal Keane
- Nafasi, BBC News, Jerusalem
Hakuna kukosea anachokiona anapopanda kifusi.
Kuna kitambaa juu ya kifusi cha kijivu. Khalil Khader anachukua nguo za kulalia za mtoto zenye vumbi na zilizochanika na moja kwa moja anatekwa na hisia za kumbukumbu.
Mtoto mchanga akiwa amevalia pajama. Rosa, binti yake wa miezi 18, mtoto wa familia.
Khalil anaonyesha video kwenye simu yake. Rosa amevaa nguo za kulalia zilezile za buluu na ameshika mikono ya binamu wawili wakubwa. Wote watatu wanacheza kwenye duara.
Video hiyo ilirekodiwa kwa mwendo wa polepole, kwa hivyo inaonekana kana kwamba watoto wanayumba katika upepo mwanana. Wanatabasamu. Ni wakati wa kucheza na maisha yao bado hayajaathiriwa na vita.
Khalil mwenye umri wa miaka 36, ni mhandisi wa kompyuta katika hospitali ya Al-Najjar huko Rafah, na baba wa watoto wanne wadogo: Ibrahim, mwenye umri wa miaka tisa; Amal, mwenye umri wa miaka mitano; Kinan, miaka miwili na nusu, na Rosa mzaliwa wa mwisho.
Khalil anapiga hatua kwa uangalifu kwenye kifusi. Nyumba iko umbali wa dakika chache tu kutoka hospitali. Sasa kuna kilima cha uashi na chuma, vitu vya nyumbani na vifaa vya kuchezea vya watoto. Ngoma ndogo. Piano ya kuchezea.
Usiku ambao kombora lilipiga - Oktoba 20 - Khalil alikuwa akifanya kazi hospitalini.
"Bomu kubwa lililipuka," aliambia mwenzangu mmoja wa BBC ambaye alienda naye kwenye eneo la shambulio.
"Majirani zangu walikuwa wakija hospitalini. Kwa hiyo nikauliza, 'Mlipuko huo ulikuwa wapi?' Nao wakaniambia, 'Ilikuwa karibu na nyumba yako.' Ilinibidi nikimbilie eneo hilo ili kuangalia familia. Nilijaribu kupiga simu lakini hakuna mtu aliyejibu. Na kama unavyoona ... nyumba nzima ilipigwa kwa bomu."
Watu kumi na mmoja wa familia yake waliuawa.
Walikuwa ni pamoja na watoto wake wanne, dada zake wawili, baba yake mwenye umri wa miaka 70, kaka yake na dada-mkwe wake, na binti zao wawili. Walikuwa wamevishwa sanda nyeupe kwenye ua wa hospitali hiyo.
Mkewe alijeruhiwa vibaya sana. Anatibiwa majeraha ya kuungua na majeraha mengine aliyopata nyumba ilipoporomoka.
Khalil amewahi kushuhudia huko Gaza. Eneo hilo dogo la ardhi - lenye ukubwa wa kilomita za mraba 141 - limekumbwa na migogoro isiyoisha kwa miongo kadhaa. Hali hiyo ilimfanya awe na wasiwasi wa kulea familia huko Gaza.
"Nakumbuka katika vita vya 2014, mke wangu alikuwa mjamzito," anakumbuka, "na majirani zetu walipigwa kwa bomu. Alikuwa katika mwezi wake wa saba na karibu aanguke kwenye ngazi kutokana na mlipuko huo. Na nilikuwa nikijiuliza, nitaweza vipi kulea watoto wangu kwenye mazingira haya?"
Lakini alifikiria pengine mambo yatabadilika na watakuwa na maisha bora.
"Nilikuwa na ndoto kwa kila mtoto wangu. Ibrahim alikuwa wa kwanza shuleni kwake na nilitamani kumuona akiwa daktari siku moja. Amal alikuwa mbunifu sana, alipenda kuchora. Na alikuwa akinionyesha michoro yake, na wakati mwingine ningechora pamoja naye.
"Kinan alikuwa anacheza sana - kila mtu alimpenda. Na alikuwa akimtunza dada yake mdogo. Kila wakati alikuwa karibu na Rosa, na alikuwa akisema, 'Usimguse, yeye ni mtoto wangu!' Na sasa wote wametoweka."
Khalil bado anatafuta mwili wa dada yake chini ya kifusi. Na lazima amsaidie mkewe hospitalini. Watoto wake wameangamia.
Lakini anapoonyesha picha yao moja baada ya nyingine- ya Ibrahim, Amal, Kenin na Rosa, kuna kitu ambacho hakitawahi kubadilika.
Daima atasalia kuwa baba yao.
Ripoti ya ziada kutok kwa Mahmoud Bassam huko Gaza, na Hanin Abdeen, Alice Doyard, Morgan Gisholt Minard, na John Landy huko Jerusalem.