Viza ya Dhahabu ni nini na kwa nini ina utata?

fd

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Visa vya dhahabu na pasipoti ya dhahabu ni maarufu miongoni mwa watu matajiri

Uhispania inakusudia kuondosha mpango wa Viza ya Dhahabu, ambayo hutoa makazi ya kudumu na ya haraka kwa raia kutoka nje ya Jumuiya ya Ulaya badala ya uwekezaji mkubwa wa kifedha.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez alisema, hatua hiyo inalenga "kuhakikisha kuwa suala la makazi ni jambo la kuwa na haki na sio kwa sababu za kibiashara.’’

Wawekezaji wengi wanaona mpango huo kama fursa ya kuanza maisha mapya, au kuepuka hatari za kisiasa, kijamii au kiuchumi katika nchi zao za asili.

Lakini wanaharakati wa kupambana na ufisadi na wanasiasa wanaonya wahalifu wanatumia mfumo huo kwa maslahi yao binafsi.

Kuna pasipoti ya dhahabu pia, ambayo hutolewa kwa watu matajiri na kuwapa haki zote na uhuru kama raia, ikiwa ni pamoja na haki ya kufanya kazi na kupiga kura katika nchi wanaoishi.

Pia unaweza kusoma

Nchi gani hutoa?

REFV

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Bei ya makazi katika mji mkuu wa Uhispania, Madrid, imepanda kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji wa aina hii

Kuna takriban nchi 60 zinazotoa visa ya dhahabu, anasema Dk. Christine Surak, profesa wa sayansi ya umma katika chuo cha London School of Economics na mwandishi wa kitabu cha The Golden Passport: The Global Mobility of Millionaires.

Anasema takribani nchi 20 zinatoa uraia halali kupitia uwekezaji, na nusu ya nchi hizo hupokea waombaji zaidi ya 100 kwa mwaka.

Dk. Surak anasema, Türkiye ndiye muuzaji mkubwa wa uraia. Pasipoti ya Dhahabu ya Kituruki huchangia takribani nusu ya mauzo ya paspoti za aina hiyo duniani kote, kulingana na utafiti wake.

Anasema nchi nyingi zinazotoa uraia kwa ajili ya uwekezaji ni nchi zinazoendelea, huku Malaysia na Falme za Kiarabu zikiwa maarufu pia.

Nchi za Saint Kitts, Dominica, Vanuatu, Grenada, Antigua na Malta ni miongoni mwa wauzaji mashuhuri wa pasipoti za dhahabu.

Nchi 14 za Umoja wa Ulaya zilitoa viza ya dhahabu mwaka 2020. Ugiriki, Latvia, Ureno na Uhispania zilichangia asilimia 70 ya utoaji huo barani Ulaya. Lakini nyingi ya nchi hizi zimeamua kuweka vikwazo kwenye mpango huo.

Mwaka 2022, serikali ya Uingereza ilisitisha mpango huo. Mwaka uliofuata, Ireland ilikomesha viza yake ya dhahabu, huku Ureno ikifanya marekebisho ya viza hiyo.

Jinsi ya Kupata Viza ya aina hii

FVC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Türkiye inatoa pasipoti ya dhahabu kwa wageni wanaonunua mali yenye thamani ya dola 400,000 au zaidi

Visa ya dhahabu na paspoti ya dhahabu ni maarufu miongoni mwa matajiri, kutafuta fursa bora za biashara, mtindo bora wa maisha, elimu bora au huduma bora za afya.

Kanuni hutegemea aina ya uwekezaji. Kwa mfano, Türkiye inatoa pasipoti ya dhahabu kwa wageni wanaonunua mali yenye thamani ya dola 400,000 au zaidi.

Baadhi ya nchi nyingine, kama vile Luxemburg, hutoa njia mbalimbali za kupata viza ya dhahabu. Moja ni uwekezaji wa angalau dola 536,000 katika kampuni iliyoko Luxembourg, au kuweka dola milioni 21.4 katika taasisi ya kifedha.

Kwa mujibu wa utafiti wa Dk. Christine Surak, asilimia 14.4 ya uwekezaji wa moja kwa moja wa wageni nchini Ureno ulitokana na viza ya dhahabu kati ya 2013 na 2019. Asilimia 12.2 nchini Latvia na zaidi ya asilimia 7 nchini Ugiriki.

Kwa nini mpango huu una utata?

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Malaysia na Falme za Kiarabu ni maarufu miongoni mwa nchi zinazotoa viza ya dhahabu
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanaharakati wanaonya juu ya maswala mawili makuu kuhusu mpango huu; ufisadi na kuchochea shida ya makazi kwa wakaazi wa maeneo hayo.

Transparency International, shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kupambana na ufisadi katika zaidi ya nchi 100, linaonya kwamba kwa nchi za Ulaya mpango huo hauhusu uwekezaji au uhamiaji – bali unahusu kutimiza maslahi ya ufisadi.

Kulingana na Eka Rustmashvili, mwanaharakati wa Transparency International, anasema, "kuna ripoti za watu kukimbia mkono wa sheria kwa kuomba viza ya dhahabu au hati za kusafiria za dhahabu kabla au baada ya kuhusika katika ufisadi au njama za ulaghai kufichuliwa."

Mwaka 2022, Kamati ya Bunge la Ulaya ya Uhuru wa Kiraia, Haki na Masuala ya Ndani ilipiga kura kuunga mkono marufuku ya utoaji wa hati za kusafiria za dhahabu na kuzitaka nchi ambazo raia wake wanaweza kuingia EU bila viza kusitisha mpango wa pasipoti za dhahabu.

Uchunguzi wa shirika la Organized Crime and Corruption Reporting Project, uliochapishwa Oktoba 2023 ulibaini kanali wa zamani wa Libya anayetuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na mfanyabiashara wa Kituruki aliyehukumiwa kifungo nchini Uturuki waliweza kununua pasipoti ya Dominika kupitia mpango huu.

Mwaka 2023, ukaguzi wa viza za dhahabu nchini Uingereza, ulioidhinishwa na Ofisi ya Mambo ya Ndani, ulihitimisha kuwa "baadhi ya wawekezaji wa kigeni wanahusika na mambo ya rushwa au uhalifu uliopangwa.

Jambo la pili, ni bei ya juu ya makazi. Ingawa nchi nyingi hutoa aina mbalimbali za uwekezaji, wengi wa waombaji huchagua kununua mali isiyohamishika.

Ununuzi wa mali isiyohamishika mara nyingi hufanyika katika miji na vitongoji vinavyopendwa na wageni.

Mji wa pwani wa Antalya ulio kusini mwa Türkiye ni mojawapo ya miji hiyo. Mji huo ni maarufu kwa watalii wa Urusi na Ukraine na umekuwa kimbilio la kudumu baada ya kuzuka kwa vita nchini Ukraine.

Wakazi wa jiji hilo wanalalamika kuwa ongezeko la mahitaji ya nyumba limesababisha bei ya nyumba kupanda sana.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi