Rais Macron amshitaki mwanaharakati aliyedai mke wa rais huyo ni mwanaume

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mkewe Brigitte wamewasilisha kesi dhidi ya mshawishi wa Marekani Candace Owens kwa kumdhalilisha bi Brigitte Macron .
Owens, anayejulikana kwa kueneza nadharia kwenye podikasti yake na mitandao ya kijamii, amedai mara kwa mara kwamba mke huyo wa kwanza wa Ufaransa alizaliwa akiwa mwanaume.
Kesi hiyo ya Macrons, iliyowasilishwa Jumatano katika jimbo la Delaware nchini Marekani, inadai kuwa Owens amekuwa akieneza "simulizi za kupita kiasi, za kukashifu na zisizoeleweka."
Owens ametoa kauli hizi mara kadhaa kwenye podcast yake maarufu na mitandao ya kijamii.
Mnamo Machi 2024, alitangaza kwamba alikuwa akiweka taaluma yake katika 'hatari' kwa ukweli kwamba Brigitte Macron ni mwanamume."

Chanzo cha picha, Getty Images
Madai ya Candace Owen
"Owens amechanganua mwonekano wao (wa Macrons), ndoa, urafiki, familia na historia ya kibinafsi, na kugeuza yote kuwa simulizi ya kutisha iliyoundwa kuwasha na kudhalilisha," kesi hiyo, iliyoripotiwa na Reuters, ilisema.
Anaongeza kuwa matokeo ya hili yamekuwa "unyanyasaji usiokoma katika kiwango cha kimataifa."
Nadharia hiyo ambayo imekuwa ikisambazwa kwa miaka mingi kwenye majukwaa ya mtandaoni inashikilia kuwa Brigitte Macron alizaliwa mwanamume chini ya jina la Jean-Michel Trogneux, ambalo ni jina la kaka yake.
Owens ameeneza nadharia hii kwa hadhira yake kubwa, ambayo inajumuisha karibu wafuasi milioni saba kwenye X.
Mapema mwaka huu, alitoa msururu wa video unaoitwa Becoming Brigitte, ambao una maoni zaidi ya milioni 2.3 kwenye YouTube.
Uvumi usio na msingi kuhusu jinsia ya Brigitte Macron ulianza kuenea mnamo 2021 na umeshughulikiwa kwenye chaneli kadhaa za kihafidhina, kama vile podikasti zinazojulikana za Tucker Carlson na Joe Rogan.

Chanzo cha picha, Getty Images
Owens asisitiza msimamo wake
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Macrons walisema katika taarifa iliyotolewa na mawakili wao kwamba walimwomba Owens mara kwa mara kufutilia mbali taarifa hiyo lakini "hatimaye walihitimisha kuwa kwenda mahakamani ndio njia pekee inayowezekana ya kurekebisha."
"Kampeni chafu ya Owens ilianzishwa ili kutunyanyasa na kusababisha maumivu kwetu na familia zetu, ili kupata sifa mbaya," ilisema taarifa hiyo.
Na anaongeza: "Tulimpa kila fursa ya kufuta kauli hizi, lakini alikataa."
Kesi hiyo inadai kuwa Owens "alipuuza ushahidi wote wa kuaminika uliokanusha madai yake, lakini badala yake alitoa jukwaa kwa wananadharia wanaojulikana na watu wanaokashifu."
BBC iliwasiliana na Owens kwa maoni lakini bado haijapokea jibu.
Msemaji wa mshawishi huyo alidai katika taarifa kwamba kesi hiyo ni jaribio la kumtisha, na akasema kwamba Brigitte Macron alikuwa amekataa maombi ya mahojiano ya mara kwa mara.
"Hii ni serikali ya kigeni inayoshambulia haki ya mwandishi wa habari huru wa Marekani," alisema.
Na alitangaza kwamba "Candace Owens hatofunga mdomo wake."
Mshawishi mwenye nadharia
Rais wa Ufaransa na mkewe pia wanamtuhumu kwa madai ya uwongo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu na kwamba Emmanuel Macron aliwekwa madarakani kupitia njama ya siri ya CIA.

Chanzo cha picha, Getty Images
Owens alifanya kazi katika mashirika ya kihafidhina, ikijumuisha kikundi cha wanafunzi Turning Point na Daily Wire, kabla ya kuzindua podcast yake huru mnamo 2024.
Tangu wakati huo, ameeneza uvumi au kupendekeza kwamba kuna njama nyuma ya maswala kama vile chanjo ya COVID, Holocaust, na kutua kwa mwezi.
Katika kesi hiyo, ambayo pia inalenga kampuni zao za Delaware, Macrons wanatafuta kiasi kisichojulikana cha uharibifu.
Chini ya sheria za Marekani, watoa taarifa lazima wathibitishe "uovu halisi," kumaanisha kuwa mshtakiwa alijua habari hiyo ni ya uwongo lakini akaichapisha au kuisambaza kwa makusudi.
Mnamo Septemba mwaka jana, mahakama ya Ufaransa iliwapata wanawake wawili na hatia ya kukashifu kwa kueneza madai hayo ya uongo kuhusu Brigitte Macron, lakini uamuzi huo ulibatilishwa kwa kukata rufaa mapema mwezi huu, kwa mujibu wa AFP.
Candace Owens ameolewa na George Farmer, mfanyabiashara Mwingereza-M'marekani na mtoto wa Michael Farmer, mwanachama wa House of Lords ya Uingereza, pamoja na mweka hazina wa zamani wa Chama cha Conservative.
Farmer amejitenga na baadhi ya maoni ya Owens.












