Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashambulizi ya Kharkiv: Jeshi la Ukraine lakomboa mara tatu ya maeneo yaliotekwa na Urusi
Jeshi la Ukraine linasema kuwa vikosi vyake vimekomba zaidi ya kilomita 3000 mraba (maili za mraba 1,158) wakati wa mashambulizi ya haraka mashariki mwa Ukraine.
Mafanikio hayo ya ajabu, yakithibitishwa, yanamaanisha kuwa vikosi vya Ukraine vimeongeza mara tatu mafanikio waliyoyapata katika muda wa saa 48.
Siku ya Alhamisi jioni, Rais Zelensky aliweka takwimu katika kilomita za mraba 1,000, na kisha kilomita za mraba 2,000 Jumamosi jioni.
BBC haiwezi kuthibitisha takwimu za Ukraine, na waandishi wa habari wamenyimwa kufika mstari wam bele wa vita hivyo.
Siku ya Jumamosi, mashambulizi ya mashariki yalishuhudia wanajeshi wa Ukraine wakiingia katika miji muhimu inayoshikiliwa na Urusi ya Izyum na Kupiansk.
Lakini maafisa wa ulinzi wa Uingereza wameonya kwamba mapigano yameendelea nje ya miji hiyo. Na maafisa wa Kyiv walisema vikosi vya Ukraine bado vinapambana kupata udhibiti wa makazi kadhaa karibu na Izyum.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilithibitisha kuondoka kwa vikosi vyake kutoka Izyum yenyewe na Kupiansk, ambayo ilisema itaruhusu vikosi vyake "kujipanga upya" katika eneo linaloshikiliwa na watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Moscow.
Wizara ya Urusi pia ilithibitisha kuondolewa kwa wanajeshi kutoka mji wa tatu muhimu, Balaklyia, ili "kuimarisha juhudi" katika eneo la Donetsk. Vikosi vya Ukraine viliingia katika mji huo siku ya Ijumaa.
Wakati huo huo, mkuu wa utawala uliowekwa na Urusi katika eneo la Kharkiv alipendekeza kwamba watu wake wahamie Urusi "kuokoa maisha".
Picha ambazo hazijathibitishwa kwenye mitandao ya kijamii zilionekana kuonyesha misururu mirefu ya msongamano wa magari kwenye vivuko vya mpaka. Gavana wa eneo la mpaka wa Belgorod nchini Urusi, Vyacheslav Gladkov, alisema "maelfu" ya watu walikuwa wamevuka na kuingia nchini humo.
Wakati huo huo, Jenerali Valerii Zaluzhnyi, kamanda wa jeshi la Ukraine, alisema vikosi vyake vimesonga mbele hadi umbali wa kilomita 50 (maili 31) kutoka mpaka wa Urusi.
Kasi ya mashambulizi imewashika Warusi, na kiongozi wa Chechnya Ramzan Kadyrov - mfuasi mkubwa wa Rais Vladimir Putin - alionekana kutilia shaka kurudi nyuma kwa Urusi.
Katika ujumbe aliotuma kwa Telegram, Bw Kadyrov alisema ikiwa hakutakuwa na mabadiliko katika vita hivyo , atalazimika kuhoji uongozi wa nchi hiyo ili kuelezea hali hiyo.
Na Bw Kadyrov mwenyewe alisisitiza "Urusi itashinda" na "silaha za Nato" "zitapondwa".
Katika mahojiano na gazeti la Financial Times, waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov alipongeza wanajeshi wake, lakini alionya juu ya uwezekano wa kutokea kwa shambulio la kivita la Urusi.
"Mashambulizi ya kukabiliana na mashambulizi hukomboa eneo na baada ya hapo unapaswa kudhibiti na kuwa tayari kulitetea," Bw Reznikov alisema. "Kwa kweli, tunapaswa kuwa na wasiwasi, vita hivi vimetutia wasiwasi kwa miaka mingi."
Hatua zilizopigwa na Ukraine Kivita - ikiwa yataendelea - yatakuwa mabadiliko muhimu zaidi ya mstari wa mbele wa vita tangu Urusi kujiondoa kutoka maeneo karibu na Kyiv mnamo Aprili.
Kupiansk ilitumika kama kitovu kikuu cha usambazaji wa bidhaa za mashariki mwa Urusi na upotezaji wa Izyum - ambayo Moscow ilitumia zaidi ya mwezi mmoja kujaribu kuichukua mwanzoni mwa vita - ingeonekana kama fedheha kubwa kwa Rais Vladimir Putin.
Kulingana na mtaalam mmoja wa kijeshi, hatua hizo zinaashiria mara ya kwanza tangu Vita vya Pili vya Ulimwengu kwamba vitengo vyote vya Urusi vimepotea.
Mafanikio hayo pia yataonekana kama ishara kwamba jeshi la Ukraine lina uwezo wa kutwaa tena eneo lililokaliwa kwa mabavu - muhimu wakati Kyiv ikiendelea kuomba washirika wa Magharibi walio na shinikizo kubwa kwa msaada wa kijeshi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alisema maendeleo ya hivi punde yanaonyesha kuwa vikosi vyake vinaweza kumaliza vita haraka kwa kutumia silaha nyingi za Magharibi.
Ukraine ilianzisha mashambulizi yake ya kukabiliana na mashambulizi mashariki mapema wiki hii, wakati tahadhari ya kimataifa ililenga katika maendeleo yaliyotarajiwa karibu na mji wa kusini wa Kherson.
Wachambuzi wanaamini kuwa Urusi ilielekeza upya baadhi ya wanajeshi wake wenye uzoefu zaidi kuulinda mji huo.
Lakini pamoja na kupata mafanikio katika eneo la mashariki, Ukraine pia inapata mafanikio katika eneo la kusini, afisa mmoja alisema.
Nataliya Gumenyuk, msemaji wa kamandi ya kusini ya jeshi la Ukraine, alisema walikuwa wamepiga hatua za kilomita kadhaa katika mstari wa mbele wa vita .
Lakini vikosi vya Urusi vinavyopigana katika eneo la kusini vinasemekana kujichimbia katika maeneo ya ulinzi, na wanajeshi wa Ukraine wamekabiliwa na upinzani mkubwa tangu kuanza kwa mashambulizi hayo.
Na huko Kharkiv kwenyewe, mtu mmoja aliuawa na nyumba kadhaa kuharibiwa siku ya Jumamosi wakati roketi za Urusi zilipiga mji huo, kulingana na maafisa wa eneo hilo.
Kwingineko, mdhibiti wa nishati wa Ukraine, Energoatom, anasema kinu cha mwisho katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachokaliwa na Urusi kimefungwa, na hakizalishi umeme.
KInu hicho kilikuwa kikizalisha nishati kwa mmea yenyewe kwa siku tatu - kilizimwa wakati nguvu za nje zilirejeshwa.