Kuna hatari gani za kuwa baba ukiwa na umri mkubwa?

Muigizaji Al Pacino ana mtoto akiwa na miaka zaidi ya themanini. Je! Sayansi inasema nini juu ya athari za kuwa baba ukiwa na umri wa juu , kupoteza mimba na hatari ya ugonjwa?
Inaonekana akina baba wanazeeka. Katika baadhi ya matukio, kwa kiasi kidogo kabisa.
Wiki hii, wawakilishi wa mwigizaji Al Pacino, mwenye umri wa miaka 83, walithibitisha kuwa ana mtoto na mpenzi wake mwenye umri wa miaka 29 Noor Alfallah. Atajiunga na klabu ya waliopata watoto baadaye maishani kama nyota mwenzake na baba wa mara kwa mara Robert De Niro, ambaye mwezi uliopita alithibitisha kuwa ana mtoto wake wa saba akiwa na umri wa miaka 79
Wawili hao kwa hakika si baba wa kwanza wazee: waigizaji wengine kadhaa wa kiume, wanamuziki, na hata marais wa Marekani wamepata watoto baadaye maishani wakiwa na umri wa juu. Na umri wa wastani wa baba wapya kwa ujumla umekuwa ukiongezeka kwa miaka mingi. Kati ya 1972 na 2015, uliongezeka kwa miaka 3.5 : wastani wa baba nchini Marekani ana umri wa miaka 30.9, na 9% ya baba walikuwa na umri wa miaka 40 wakati mtoto wao anazaliwa.
Baba mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kutokea, angalau kulingana na Guinness World Records , alikuwa na umri wa miaka 92 - ingawa madai yasiyo rasmi kuhusu hata wanaume wazee zaidi ya hapo mara kwa mara huibuka.
Hata hivyo, kuwa baba mkubwa hubeba hatari fulani.
Mnamo Desemba 2022, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Utah na taasisi nyingine walichapisha mapitio ya kina ya "umri wa kina baba" na athari zake kwa uzazi, matatizo katika ujauzito na afya ya utotoni.
Ingawa tafiti nyingi hazingejumuisha wanaume wengi wa umri wa Pacino, kutokana na jinsi walivyo nadra, ushahidi unaonyesha kwamba mbegu za kiume za miaka arobaini na hamsini tayari zina ubora wa chini katika suala la kiasi, hesabu na mabadiliko . .
Mabadiliko haya yanamaanisha kwamba umri mkubwa wa uzazi "unahusishwa sana na hatari kubwa ya sio tu kuwa na utasa lakini pia kupoteza mimba baada ya mimba ya asili", watafiti wanaandika. Tafiti nyingi, zinasema, zimeonyesha kuwa baba wa umri mkubwa huongeza hatari ya kuharibika kwa mimba.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kisha kuna hatari ya ugonjwa baada ya kuzaliwa. Imejulikana tangu miaka ya 1950 kwamba baba wa umri wa juu wana uwezekano mkubwa wa kupata watoto walio na ugonjwa wa jeni achondroplasia . Lakini tangu wakati huo, uhusiano na hali zingine tofauti umeibuka.
"Imezidi kudhihirika kuwa umri mkubwa wa uzazi, unahusishwa na…madhara duni ya kiafya kwa watoto," watafiti wa Utah wanaandika.
Watafiti katika Chuo Kikuu cha Stanford, kwa mfano, waligundua baba wa umri mkubwa walihusishwa na hatari za kuzaliwa kwa uzito mdogo na kifafa kwa watoto wachanga. Umri wa uzazi wa juu pia unahusishwa na viwango vya kuongezeka kwa kansa mbalimbali za utoto, pamoja na kasoro za moyo za kuzaliwa.
Inafaa kukumbuka, hata hivyo, kwamba kama tafiti nyingi zinazochunguza uhusiano kati ya afya na sababu zinazowezekana, njia hazieleweki. Kuna uwezekano wa kuwepo mambo mengine magumu ambayo huchukua jukumu, kama vile mtindo wa maisha ya wazazi na uchafuzi wa mazingira .
Hata hivyo, watafiti wamegundua kwamba kadiri wanaume wanavyozeeka, wanaweza kupata mabadiliko na uharibifu wa DNA katika chembe zinazounda mbegu ambazo zinaweza kupitishwa kwa kizazi kijacho .
Masomo kama haya yanasababisha mabadiliko katika njia ambayo madaktari na wanasayansi wanafikiria juu ya uzazi kwa ujumla zaidi. Kihistoria, kumekuwa na tabia ya kuzingatia mwanamke na umri wake wakati wanandoa wana matatizo ya kushika mimba. Hakika, utafiti mwingi umezingatia uzazi wa wanawake . Lakini sasa inakuwa wazi kwamba ingawa uzazi wa kiume unaweza kupungua polepole zaidi, na baadaye maishani kuliko wanawake, umri wa baba bado ni muhimu.
Kwa sasa, kesi za Pacino na De Niro - na wanaume wengine katika miaka ya sabini, themanini na tisini - zimesalia kuwa nadra.
Tangu miaka ya 1970, idadi ya akina baba wa Marekani wenye umri wa chini ya miaka 30 imepungua kwa 27%, wakati idadi ya baba wenye umri wa miaka 45-49 iliongezeka hadi 52%.
Ikiwa mwelekeo wa sasa utaendelea, tiba - ikiwemo pia mitazamo ya kijamii - bila shaka italazimika kubadilika.












