WARIDI WA BBC: 'Sijamsamehe baba wa kambo kwa kunidhulumu kingono"

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Victoria Itenyo ni mama na mwanaharakati wa haki za watoto na pia anatoa ushauri nasaha juu ya masuala yanayohusu watoto na vijana nchini Kenya.

Hatua hii ya kushughulikia afya ya akili kwa watoto na vijana ilimjia baada ya kuishi na machungu na kero kwa miaka mingi kwa kile anachosema ni tukio la kunajisiwa na baba wa kambo wakati akiwa na umri wa miaka 11.

"Kukua kwangu ilikuwa ni mimi na mama yangu pekee, mama alikuwa na kazi na alihakikisha kuwa ninaishi maisha mazuri, hadi pale alipoanza uhusiano na baba wa kambo ndipo maisha yangu yalipochukua mkondo tofauti, " anakumbuka Victoria.

Alipotimiza miaka 7, Victoria anasema kuwa mama yake alipatana na mwanamume mmoja ambaye walianza uhusiano wa kimapenzi naye na muda si muda, mwanamume huyo alihamia kwao na wakaanza kuishi naye kama baba wa kambo.

Victoria anasema kuwa uhusiano kati ya mama yake na baba wa kambo, ilipelekea kuzaliwa kwa kaka yake mdogo wakati akiwa na miaka 8.

"Nakumbuka pindi tu kaka yangu mdogo alipozaliwa maisha yalinibadilikia kwani baba wa kambo alianza kuwa mbaya kwangu, hakuficha hisia zake kwangu kuonyesha kuwa ananipenda, na hilo halikuwa siri kwa wale tuliokuwa tunaishi nao," Victoria anasema.

Baba wa kambo alivyoninyanyasa kimapenzi

Victoria anasimulia kisa hicho kana kwamba kilifanyika jana, kuanzia mavazi aliovalia baba wa kambo hadi jinsi siku hiyo ilivyoanza. Yote bado yamejikita akilini mwake.

Anaendelea kusema licha ya kuwa miaka mingi imesonga tukio hilo lingali katika moyo wake na imekuwa vigumu kulisahau licha ya kuwa amepitia matibabu ya kisaikoloji, ya afya ya akili na mengineo.

Victoria anakumbuka siku hiyo alikuwa ameamka mapema kama kawaida na kwenda shuleni, lakini hakuwa amelipiwa karo ya shule hivyo basi, waliamriwa kurejea nyumbani hadi ada itakapolipwa.

Mwanamke huyo anasema aliporudi nyumbani aliamua kukaa ndani kwani mchana hakukuwa na watoto wenzake wa kucheza naye.

"Kipindi ambacho baba yangu wakambo alininajisi tulikuwa tunaishi na rafiki wa mama yangu, ni nyumba iliyokuwa na vyumba vitatu na sisi tulikuwa tumepewa chumba kimoja ambacho tuliishi mimi, mama na baba wa kambo aliyekuwa amehamia pale pale kwa nyumba ya rafiki wa mama yangu," Anakumbuka Victoria.

Victoria anasema alikuwa amekaa chumbani pale baba wa kambo alipomuita na kumweleza kuwa alitaka kumfundisha densi moja maalum. Mwanadada huyo anakumbuka kuwa mtu huyo alikuwa amejifunga kikoi.

Aidha Victoria aliitikia mwito wa baba wa kambo na wakaanza kucheza densi lakini ghafla bin vuu mwanamume huyo aligeuka na kuwa mchungaji mla kondoo wake na papo hapo Victoria anasema, baba wa kambo alimnajisi.

Baada ya tukio hilo baba wa kambo aliingia bafuni na kuoga na kisha akaondoka.

Tukio la dhulma lilivyofichwa

Wakati tukio hilo lilipokuwa linafanyika, rafiki ya mama yake Victoria alikuwepo na anasema kwamba kuwa akilini mwake alifahamu kitendo kilichofanyika hakikuwa kizuri.

Victoria anasema kuwa baba wa kambo alimshurutisha aende kuoga kwa mara nyingine tena, na mwanamume huyo akaondoka baada ya kitendo hicho.

"Rafiki wa mama ambaye pia tulikuwa tunaishi na yeye, alikutana na mimi nikitoka bafuni akaniuliza ni nani niliyekuwa nina zungumza na yeye. Na mimi nikamueleza kuwa kuwa ni baba wa kambo na ameninyanyasa king’ono. Mama huyo alinituliza na kuniambia tusubiri mama yangu arejee ili nimueleze kilichotokea".

Mama yake Victoria alipofika nyumbani alielezwa yaliomkuta binti wake Victoria na anasema kuwa mama yake alimuuliza ikiwa alikuwa amezungumza na watu wengine na papo hapo akamkanya dhidi ya kuzungumzia tukio hilo.

Vile vile mwanadada huyo anasema kuwa baba wa kambo alipoulizwa alisema kuwa maneno ya Victoria hayakuwa ya kweli na kwamba alikuwa anatoa taarifa za uwongo.

Victoria anasema kuwa mama yake alishindwa kumchukulia hatua baba wa kambo na kama haitoshi akawa ni mwenye kumkinga licha ya dhulma alizopata mwanawe mikononi mwa mwanamume huyo.

Kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, maisha yalianza kuwa magumu kwake na kwa kiasi fulani Victoria alianza kuyaona kuwa kero na machungu yalimzonga na akaanza kuona siku zikiwa ndefu na maisha kukosa ladha.

Msamaha baina ya binti na mama

Wakati Victoria alipofikisha miaka 16, anakumbuka mama yake alimwalika kwa chakula cha mchana ambapo mama alifungua roho kuhusu matukio mengi yaliyotokea.

Victoria anasema kuwa mama yake alihuzunika baada ya kugundua kuwa hakuweza kumkinga binti yake dhidi ya tukio la kunajisiwa na baba wa kambo ila alikubali kuwa wakati huo alishindwa ni hatua ipi angemchukulia mwanamume huyo.

"Mama alinifungukia na kuomba msamaha kwa kushindwa kunilinda wakati nilipomuhitaji zaidi na ingawa mama yangu alifariki, niliamua kumsamehe," Victoria anasema.

Ila kwa upande wa baba wa kambo, Victoria anasema imekuwa vigumu sana kumsamehe ikiwa ni zaidi ya miaka ishirini tangu tukio hilo kufanyika.

"Sijamsamehe baba wa kambo kwa kunidhulumu kingono."

Lakini pia tangu mama yake alipofariki, yeye na baba yake wa kando hawajaonana kwa miaka mingi.

Jinsi Victoria alivyobadilisha machungu ya dhulma kuwa faida

Baadaye Victoria alipata mchumba na kuolewa na kujaaliwa mtoto wa kike ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 12. Na licha ya kuwa ndoa yake haikufaulu Victoria amejitolea kuhakikisha kuwa anawakilisha watoto ambao wanajipata katika dhulma za king’ono.

Victoria amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kuhusu mateso ambayo watoto hupitia mikononi mwa watu ambao wanafaa kuwaamini na kuwalinda.

Hivyo basi, anatoa ushauri nasaha na kuwashika mkono watoto au wanarika ambao wamedhulumiwa katika jamii na wamekosa haki.

Hali kadhalika mwanadada huyo anasema kuwa tangu alipodhulumiwa aliwachwa na makovu mengi hasa ya kihisia na kisaikolojia. Katika ukuaji wake, alikuwa msichana aliyeogopa mno kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kwasababu "nilihisi kwa ujumla, ninawaogopa wanaume."

Anasema imekuwa safari ndefu ya kuponya vidonda ndani ya moyo wake, na kwa kila hatua aliyopiga, tukio hilo la kunyanyaswa king’ono wakati akiwa mtoto limekuwa likipungua nguvu.