Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mabilionea wanavyotoa pesa zao kuboresha maisha ulimwenguni
Na Dinah Gahamanyi
BBC News Swahili
Miaka sita iliyopita, Warren Buffett na Bill Gates walianzisha kampeni inayoitwa TheGive Pledge ambapo mabilionea hujitolea kutoa angalau nusu ya utajiri wao kwa hisani.
Tangu wakati huo, karibu mabilionea 200 wameahidi kutoa fedha zao kwa njia ya wakfu na misaada badala ya kuwapatia watoto wao.
Hawa hapa ni mabilionea 10 miongoni mwao ambao hadhithi zao zinavutia:
Mark Zuckerberg
Zuckerberg, mwanzilishi wa Facebook (FB) ni mtu anayeamini na kuipenda sana elimu.
Alitoa pesa kudhamini mfumo wa shule ya umma ya Newark $ 100 milioni mnamo 2010 kabla ya kutoa michango miwili tofauti ya jumla ya karibu $ 1.5 bilioni kwa wakfu wa Silicon Valley Community mnamo 2013.
Huduma za ruzuku za Silicon Valley Community Foundation ni pamoja na elimu, pamoja na usalama wa kiuchumi, uhamiaji, na ujenzi wa jamii.
Mwishoni mwa mwaka 2015 na kuambatana na kuzaliwa kwa mtoto wake wa kwanza, Zuckerberg na mkewe waliahidi kutoa mchango wao wote katika Facebook kwa mpango wa Chan Zuckerberg.
Mchango huu, zaidi ya miaka mitatu, ni sawa na 99% ya hisa za Zuckerberg za Facebook, ambazo ni takribani $ 45 bilioni.
Mpango wa Chan Zuckerberg una lengo la kuongeza uwezo wa binadamu na kukuza usawa katika maeneo kama vile afya, elimu, utafiti wa kisayansi, na nishati.”
Bill Gates
Huenda Bwana Gates ndiye mhisani anayejulikana zaidi kwenye orodha hii.
Kuanzia mwaka 1997, Gates alianza kuuza na kutoa hisa zake za Microsoft (MSFT) ili kufadhili kile kinachoitwa Bill &Melinda Gates Foundation.
Taasisi hiyo inachukuliwa kuwa tajiri zaidi duniani na inalenga kutatua matatizo ambayo ni ya haraka lakini yasiyo kipaumbele kwa serikali, mambo kama malaria, polio na usafi wa mazingira.
Mbali na kutatua matatizo yanayoikumba dunia, wakfu wa Bill & Melinda Gates pia umedhamiria kumaliza umaskini, kukuza elimu na kuboresha afya duniani kote.
Wakfu wa Bill & Melinda Gates ni taasisi kubwa zaidi ya binafsi duniani ikiwa na thamani ya dola bilioni 44.
Taasisi hiyo ina ufanisi mkubwa kwa fedha zake kiasi kwamba Warren Buffett ameahidi kiasi kikubwa cha fedha zake kwa wakfu wa Bill & Melinda Gates badala ya yeye mwenyewe, kwa kuwa anahisi kuwa fedha hizo zitatumika kwa ufanisi zaidi mikononi mwa Bill Gates.
Paulo Allen
Mtaalamu mwenzake wa Microsoft Allen ametoa pesa zake kwa ajili ya utafiti wa matibabu hususan ubongo, Allen ameanzisha Taasisi ya Sayansi ya Ubongo na Taasisi ya Huduma ya Akili Mnemba (AI) .
Taasisi hizo kwa sasa zinafanya kazi ya kujifunza jinsi ubongo unavyofanya kazi na kuendeleza akili ya kisasa ya bandia.
Michango ya marehemu Allen katika utafiti wa matibabu pia inaambatana na michango ya kupambana na Ebola, pamoja na kulinda dunia na kukuza elimu.
Warren Buffett
Buffett, anayefahamika kama Mwekezaji Mkuu Zaidi Aliyewahi Kuishi, ameahidi kutoa 99% ya pesa zake wakati wote wa maisha yake au wakati wa kifo kwa ajili ya hisani.
Buffett ambaye ni rafiki wa Gates, ameupatia jukumu wakfu wa Bill & Melinda Gates wa kuwa mpokeaji mkuu wa mabilioni yake.
Vinginevyo, Buffett anahusika katika Wakfu wa Susan Thomson Buffet , shirika ambalo lilianzishwa mwaka wa 1964. Leo, shirika hilo linahusika sana katika kukuza elimu, kutoa udhamini na kutoa tuzo kwa walimu.
Elon Musk
Musk anatumia mabilioni yake katika uendeshaji wa Wakfu wake Musk Foundation unaofadhili mipango ya nishati mbadala, uvumbuzi wa binadamu wa anga za juu, utafiti katika afya ya watoto na elimu ya sayansi.
Musk pia amejulikana kutoa huduma za pesa na nishati kutoa usaidizi katika hali za maafa.
Sara Blakely
Blakely, mwanamke pekee katika orodha hii, ni mvumbuzi wa Spanx, bidhaa ambayo ilimfanya kuwa bilionea mdogo zaidi aliyejitengenezea utajiri wake.
Leo, Blakely anasimamia wakfu wa Sara Blakely Foundation , shirika ambalo husaidia wajasiriamali wanawake na elimu na mafunzo.
Zaidi ya hayo, Blakely ametoa kiasi kikubwa cha fedha kwa Chuo cha Uongozi cha Oprah Winfrey na shule yake kwa wasichana barani Afrika.
Ted Turner
Turner ambaye ni mtu mashuhuri na maarufu katika burudani ni muasisi mwenza wa mpango wa kupambana na nyuklia ulioanzishwa mwaka 2001.
Lengo kuu la wakfu huo ni kukuza usalama wa silaha za nyuklia na kibiolojia.
Turner pia ametoa dola bilioni 1 kwa Umoja wa Mataifa kuunda wakfu wa Umoja wa Mataifa.
Wakfu huo ulianzishwa kama njia ya kukubali michango ya kusaidia Umoja wa Mataifa kukuza shughuli zake katika afya, uendelevu na kibinadamu.
Larry Ellison
Akiwa mwanzilishi wa Oracle Corp (ORCL), Ellison, ni mfadhili wa kimya kimya.
Mbali na kuwekeza fedha zake, Ellison ameanzisha wakfu wake, Elison Medical Foundation ambao unatoa fedha kwa ajili ya utafiti wa matibabu ili kupambana na magonjwa yanayohusiana na umri pamoja na Lawrence Ellison Foundation ambayo inalinda wanyamapori.
Michael Bloomberg
Bloomberg Philanthropies ni taasisi iliyoanzishwa na Bloomberg. Shirika hilo lina maeneo makuu kama : mazingira, ambayo likitoa fedha ili kukuza uendelevu na nishati safi; afya, ambapo fedha zimetumika kupambana na matumizi ya tumbaku na kuendeleza afya ya wanawake; sanaa, huku Bloomberg Philanthropies ikitoa fedha kwa mashirika ya sanaa na kwa ajili ya makumbusho; mageuzi ya serikali; na kwa elimu.
Richard Branson
Naye Sir Branson, ambaye ni mwanzilishi wa Virgin Group, ameahidi kutoa mabilioni yake katika juhudi za kibinadamu na kuwasaidia watu kufuata nyayo zake za biashara.
Ametoa fedha na muda wake kusaidia kuzuia ongezeko la joto duniani na ni mwanaharakati wa kupambana na ujangili.
Virgin Group ina msingi usio wa faida unaoitwa Virgin Unite, kampuni ambayo inalenga kuboresha uongozi, utetezi, kufundisha ujasiriamali na fedha, na uvumbuzi wa biashara.
Mabilionea hawa kumi husaidia kuokoa dunia na kuondoa matatizo yanayohusiana na umaskini.
Ingawa elimu na huduma za afya ni maeneo maarufu zaidi ya mchango wao , mabilionea wengine wanalenga maeneo yasiyofadhiliwa ya ulimwengu, kama usalama wa kemikali ya kibaiolojia na utafutaji katika anga za juu.
Bila kujali hisia za umma kwa watu hawa kumi, wanaboresha hali ya maisha ya ulimwengu, kwa ajili ya wakazi bilioni moja kwa wakati mmoja.
Imeandikwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Lizzy Masinga.