Je William Ruto ametimiza ahadi zake za kampeni katika uteuzi wa baraza la mawaziri?
Na Asha Juma

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Kenya William Ruto hapo jana ametangaza baraza lake la mawaziri.
Bwana Ruto ameteua wanasiasa mbalimbali na kujaribu kuangalia namna atakavyoweza kusawazisha nafasi zilizopo kwa wanasiasa waliojitoa kimasomaso kusimama naye katika kipindi cha kampeni na uchaguzi uliokamilika.
Wakati wa kampeni zake, miongoni mwa ahadi alizotoa ilikuwa ni pamoja na kuunda nafasi ya uongozi ya Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri.
Bw Ruto ametimiza hilo kwa kuunda nyadhifa ya Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri, iliyopewa kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi.
Nafasi hiyo imeonekana kuwa karibu sana na Rais. Lakini je, tofauti yake na wadhifa wa Makamu Rais unaoshikiliwa na Rigathi Gachagua ni ipi?
Makamu Rais
- Mwakilishi wa rais katika utekelezaji wa majukumu ya rais
- Mwenyekiti wa kamati za baraza la mawaziri
- Kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya baraza la mawaziri katika wizara zote na idara za serikali
- Kuratibu uhusiano katika ya Serikali Kuu na serikali za Kaunti ikiwemo kusimamia Bajeti ya Serikali na Baraza la Kichumi
- Kushirikiana na tume za katiba na ofisi huru katika masuala yanayohitaji ushirikiano wa serikali kama bajeti, uundaji wa sera na utekelezaji wa mapendekezo yake
- Uratibu wa mipango na usimamizi wa utekelezaji wa miradi na mipango ya maendeleo
- Usimamizi wa mabadiliko katika sekta ya umma
- Na utekelezaji wa majukumu yoyote yale ambayo utapewa na Rais
Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri
- Kumsaidia Rais na Makamu Rais katika uratibu na usimamizi wa wizara na idara za serikali
- Kwa ushirikiano na Wizara ya mambo ya ndani na utawala wa kitaifa, kusimamia utekelezaji wa sera za serikali ya kitaifa, mipango na miradi
- Kusimamia na kuratibu ajenda za utungaji sheria katika serikali ya kitaifa kwenye wizara zote na idara kwa kushauriana na viongozi wa vyama bungeni
- Kusimamia na kuratibu miradi na mipango ya wizara
- Uratibu na usimamizi wa thathmini ya sera za serikali, miradi na mipango katika wizara zote
- Na kutekeleza majukumu yoyote yale ambayo unaweza kupewa na Rais
Je ahadi ya usawa wa kijinsia katika uteuzi wa baraza la mawaziri, imetimia?
Wanawake 7 wameteuliwa katika baraza jipya la mawaziri nchini Kenya kati ya nafasi 22 zilizopo kikatiba.
Susan Wafula amechukuwa nafasi ya (Waziri wa Afya), Florence Bore ameteuliwa kuwa (Waziri wa Ajira), Penina Malonza (Waziri wa Utalii), Soipan Tuya (Waziri wa Mazingira), Aisha Jumwa (Waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia), Rebecca Miano (Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki) na Alice Wahome (Waziri wa maji).
Hata hivyo, licha ya uteuzi huo ambapo majina hayo sasa yatasubiri kuidhinishwa na bunge, je, Bw Ruto alifanikiwa kutimiza ahadi yake ya kuteua kwa usawa wa kijinsia nafasi za uongozi?
Kulingana na katiba ya Kenya, nafasi zilizopo katika baraza la mawaziri sio zaidi ya 22.
Lakini anayonafasi ya kuchagua wanawake wengi zaidi hasa ikizingatiwa kuwa kuna nafasi za Makatibu Wakuu wa Wizara ambazo bado hazijatangazwa.
Kuregesha fadhila
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati wa kipindi cha kampeni kama kwingine kokote, kuna matukio mengi yaliyojitokeza.
Wanasiasa walikuwa wakipima kwa macho na mizani na kutathmini namna ya kucheza karata zao vizuri kwenye safari yao hiyo.
Tuanze kwa kuangalia waliojihini ili kupiga jeki siasa za Rais William Ruto.
Aliyekuwa spika wa bunge la kitaifa Justus Muturi ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya.
Wakati wa kampeni, Bw. Muturi alipewa uongozi wa chama cha Democratic Party cha aliyekuwa Rais Mwai Kibaki na kutangaza kwamba atawania urais.
Wakati fulani alitangaza kuwa chama hicho hakitaingia katika makubaliano na muungano wowote kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo, miezi michache baadaye, alifungia macho aliyosema na kutangaza kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na William Ruto.
Mwingine aliyeonekana kuchukua wadhifa wa juu ni aliyekuwa seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki.
Ndiye atakaye chukua nafasi ya Dr. Fred Matiang’i ya Waziri wa Mambo ya Ndani na mratibu wa Serikali ya Kitaifa.
Aisha Jumwa ameteuliwa kama Waziri wa Utumishi wa Umma na Jinsia.
Katika kipindi cha kampeni, alijitolea kufa kupona kumuunga mkono Rais William Ruto na yeye mwenyewe akawa anawania nafasi ya gavana katika kaunti ya Kilifi.
Hata hivyo aliangushwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Ugatuzi Gideon Mung'aro.
Mwingine anayeelekea kuweka historia ya kufanyakazi katika serikali zote zilizotangulia iwapo jina lake litaidhinishwa na bunge ni – aliyekuwa mbunge wa Nyaribari Masaba Ezekiel Machogu.
Amepewa nafasi ya waziri wa elimu iliyoshikiliwa na Profesa George Magoha.
Bw Machogu anasimamia Wizara ya Elimu wakati kuna sintofahamu nyingi kuhusu mtaala wa sasa wa elimu ya (CBC).
Rais William Ruto katika hotuba yake wakati anaapishwa rasmi, alihakikishia wazazi nchini Kenya kwamba ataanzisha jopo kazi la mageuzi ya elimu litakalosimamia ushirikishwaji wa umma unaolenga kupitia tena Mtaala wa Elimu ya (CBC).
Ezekiel Machogu amezawadiwa nafasi hiyo ya waziri baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu alipokuwa akitafuta kuwa gavana wa kaunti ya Kisii lakini akapigwa chini na Simba Arati.
Tofauti iliyojitokeza na teuzi za serikali iliyotangulia
Katika uteuzi huo wa mawaziri uliofanywa na Rais William Ruto, picha iliyojitokeza tofauti na uteuzi wa serikali ya awali, ni kwamba serikali ya sasa imejumuisha wanasiasa katika baraza la mawaziri.
Katika utawala uliotangulia, nyadhifa hizi ziliegemea zaidi ujuzi na stadi wa mtu kwendana na wizara husika na ambaye hakuwa mwanasiasa.
Wanasiasa Kipchumba Murkomen ambaye ni Seneta wa Elgeyo Marakwet, amepewa Wizara ya Usafirishaji na Barabara huku mbunge wa eneo la Garissa mjini Aden Duale akiteuliwa katika wizara muhimu ya Usalama.
Mbunge wa eneo la Kandara Alice Wahome, amepewa wizara ya Maji na Usafi.
Wote hao walikuwa wamechaguliwa na wananchi kama wawakilishi wao kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022 ikiwa ni pamoja na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula.
Hivyo basi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), itaanza mchakato wa kuandaa chaguzi ndogo katika maeneo yao ili wananchi wapate fursa ya kuchagua viongozi wengine watakao wawakilisha.
Hatua hii itaanza rasmi kutekelezwa baada ya wahusika kuwasilisha barua zao za kujiuzulu.












