Tunachokifahamu kuhusu Rais wa zamani wa Korea Kusini aliyehukumiwa kifungo cha maisha

Yoon Suk Yeol

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Mahakama nchini Korea Kusini juma hili ilimhukumu kifungo cha maisha jela Rais wa zamani wa nchi hiyo Yoon Suk Yeol, kwa kufanya uasi alipojaribu kuidhinisha utawala wa kijeshi mwaka mmoja uliopita.

Amri yake iliyodumu kwa muda mfupi, iliibua hisia mseto iliyoigawanya taifa hilo, na kuipa nafasi upinzani kushinda uchaguzi uliofanyika miezi sita baadaye.

Yoon mwenye umri wa miaka 65, tayari alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kutumia mamlaka yake vibaya, na kuzuia kukamatwa kwake. Bado ana mashataka mengine mawili ya kujibu.

Uamuzi wa siku ya Alhamisi dhidi yake ulihusisha shitaka kubwa zaidi la uasi.

Uasi ni nini?

Uasi ni hatua ya kujaribu kuipindua au kuipindua serikali iliyopo madarakani kwa kutumia nguvu.

Chini ya sheria ya Korea Kusini, rais aliye madarakani hawezi kufunguliwa mashtaka ya uhalifu isipokuwa kosa la uasi au uhaini.

Siku ya Alhamisi, mahakama moja mjini Seoul, ilisema kuwa matendo ya Yoon ya tarehe 3 mwezi Disemba 2024, ya kuwatuma wanajeshi kufunga bunge la kitaifa na kuwakamata viongozi wa kisiasa, zilikuwa hatua zinazokandamiza katiba ya taifa hilo

"Mahakama imebaini kuwa alikuwa na nia ya kulemaza bunge kwa muda usiojulikana" Jaji Ji Gwi-yeon alisema.

Waendesha mashtaka walitaka Yoon ahukumiwe kunyongwa wakisema kuwa "sio mtu wa kusamehewa." Waendesha mashataka walisema akipewa adhabu ndogo haitatoa funzo kwa wale watakaotaka kujaribu au kurudia alichokifanya.

Yoon alisema awali kuwa aliweka sheria hiyo ya kijeshi ili kuilinda taifa hilo kutoka kwa "wanaoipinga serikali" haswa wale wanaoiunga mkono Korea Kaskazini.

Ila wiki zilizofuata ilibainika kuwa alikuwa akikumbwa na changamoto tofauti za kisiasa,alikuwa anakumbwa na kashfa tofauti, ushawishi wake ulikuwa umepungua, na upinzani ulikuwa umetishia kuchunguza mkewe kwa madai ya ufisadi.

Ila wakati wa kesi yake, aliendelea kutetea uamuzi wake wa kuidhinisha utawala wa kijeshi akisema ilikuwa njia ya 'kulinda uhuru wa watu na taifa hilo pamoja na katiba"

Waandamanaji wanaompinga Yoon, wakiandamana mjini Seoul Mwezi Machi 2025.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa Korea Kusini kufungwa jela kwa kufanya uasi.

Chun Doo-hwan, ambaye aliongoza Korea Kusini miaka ya 1980 kama kiongozi wa kijeshi, alipewa kifungo cha kunyongwa kwa kutenda uasi, ila baadaye alipunguziwa adhabu hiyo na kupewa kifungo cha maisha. Mrithi wake Roh Tae-woo alipewa kifungo kirefu ila baadaye wote walisamehewa.

Waendesha mashtaka walisema hatua ya Yoon mwaka wa 2024 ya kujaribu kuweka sheria ya kijeshi iliharibu mno heshima ya taifa hilo ikilinganishwa na mapinduzi yaliyofanywa na Chun na Roh mwaka wa 1979.

Lim Ji-bong, Professa wa sheria aliambia BBC kuwa hakuwa anatarajia Yoon kupewa kifungo cha kunyongwa, kwani ingekuwa na athari za kisiasa na kuleta vurugu nchini humo haswa miongoni mwa wafuasi wake.

Hata kama angepewa kifungo cha maisha, kifungo hicho hakingetekelezwa kikamilifu, kwani Korea Kusini haijamnyonga mtu tangu mwaka wa 1997 alisema Lim.

Christopher Jumin Lee, wakili anayeishi Marekani anasema anaamini Yoon atasemehewa baadaye kama Chun na Roh walivyopewa msamaha.

"Ni desturi katika siasa za Korea, hukumu aliyopewa ni kudhihirisha tu kosa alilotenda ni baya" Alisema Lee.

Kuzuia kukamwatwa

Mwezi Januari, Yoon alipatikana na hatia ya kukwepa kukamatwa, kutumia mamlaka vibaya ,kuitisha mktano na mawaziri kabla ya kuidhinisha sheria ya utawala wa kijeshi na kughushi stakabadhi muhimu.

Waendesha mashtaka walimshtumu kwa kutumia taasisi za serikali kwa manufaa yake kibinafsi na kukwepa kuwajibika kisheria.

Mwezi Januari mwaka uliopita, polisi 3000 walijaribu mara mbili ili kufanikiwa kumkamata Yoon na kumzuilia.

Yoon alikuwa ameweka kikosi kikubwa cha walinzi kuizingira boma lake, na kuzuia jaribio la kumkamata.

Maelfu ya polisi katika makaziya Yoon wakijaribu kumkamata

Chanzo cha picha, Reuters

Kusaidia adui

Waendesha mashtaka pia walidai kuwa Yoon alijaribu kuichokoza Korea Kaskazini kwa kutekeleza shambulio kusini mwa taifa hilo ili kutetea hatua yake ya kuidhinisha sheria ya kijeshi.

Kesi hii iliyofunguliwa mwezi Januari, itachunguza iwapo Yoon aliamrisha droni kutumwa Korea Kaskazini ili kuchochea vita kati ya mataifa hayo mawili.

Waziri wa ulinzi wa zamani katika utawala wa Yoon, Kim Yong-hyun, pia anakabiliwa na shtaka hilo.

Mashtaka mengine

Yoon pia anakabiliwa na shitaka la kusema uwongo, baada ya kutoa ushahidi usio wa kweli kwa kesi ya waziri mkuu wa zamani wa taifa hilo Han Duck-soo's, ambapo alikuwa anakumbwa na shitaka la kusaidia uasi wa Yoon.

Yoon pia ni miongoni mwa watu 33, wanaokabiliwa na shitaka la kuzuia uchunguzi wa kifo cha askari mmoja wa jeshi la maji mwaka wa 2023.

Pia anakumbwa na shitaka la kuingilia uchaguzi wa urais wa mwaka 2022 na kutoa semi za uongo wakati wa kampeni.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula