Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mali: Kipi kifuatacho kwa nchi inayotegemea Wagner kwa usalama wake?
Wakati Mali inapambana na wapiganaji wa Kiislamu na makundi ya wanaotaka kujitenga, nchi hiyo imewageukia mamluki wa Wagner kwa usalama. Lakini kiongozi wa kundi hilo amekufa, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaondoka na Mali inakabiliwa na mgogoro.
Mwandishi wa BBC Feras Kilani alisafiri hadi eneo hatari la jangwa kaskazini - kukutana na watu waliokumbwa na machafuko.
Ilikuwa jioni tuliweka kambi, tukawasha moto ili kupika chakula cha jioni na kuweka blanketi zetu na kulala chini ya anga ya wazi. Ghafla ukimya wa usiku wa jangwa lenye joto kali ukavunjwa na muungurumo wa pikipiki.
Kisha tulisikia watu wakikoki silaha zao mfululizo. Tulikuwa na kikundi cha watu wanaotaka kujitenga wa Tuareg ambao walimwambia mtu aliyekuwa kwenye pikipiki aendelee na safari yake.
Mara tu alipoondoka, wenyeji wetu walituambia tunapaswa kuondoka pia. Ilikuwa ni hatari sana kukaa mahali hapo kwani mtu huyo alikuwa skauti wa kikundi cha wenyeji kinachoshirikiana na al-Qaeda.
Tulikuwa waangalifu, tulivua jinzi zetu na kuvaa majoho ya kitamaduni na vilemba vya Tuareg, kama angegundua kuna wageni angeweza kuwaongoza wanamgambo na wangetuteka nyara.
Tulipakia vitu upesi na tukaenda kwenye eneo lenye giza totoro bila taa za gari wala mienge ili tusifuatwe.
Sehemu hii ya kaskazini mwa Mali iko nje ya udhibiti wa serikali na inaendeshwa na vikundi vya watu wanaotaka kujitenga wa Tuareg na waislamu wenye itikadi kali wenye uhusiano na al-Qaeda - hawaelewani lakini wamefikia maelewano ya kutosumbuana.
Serikali imejitenga na vikosi vya kimataifa vya kulinda amani, ikitegemea kundi la Wagner la Urusi kwa usalama. Lakini sasa kiongozi wao Yevgeny Prigozhin, ameaga dunia katika ajali ya ndege, na kuacha maswali juu ya operesheni zao Mali.
Kuwakimbia IS
Katika upande wa mashariki, kundi la Islamic State limejiimarisha na linajaribu kuongeza eneo linalodhibiti. Tulitaka kukutana na raia wa huko.
Kwa hivyo tuliendesha gari zaidi ya kilomita 1,000 (maili 650) katika jangwa hadi jiji la Kidal mashariki mwa Mali. Tulipofika, tuliona kambi za maelfu ya wakimbizi wanaishi baada ya kukimbia makazi yao.
"Dola ya Kiislamu ilitulazimisha kuja hapa," Fatima alituambia, akiwa ameketi kwenye hema ya muda. Ana umri wa miaka 60 na hapa ni nyumbani kwake, binti yake na wajukuu zake wawili wako kando yake.
Mumewe na mkwewe waliuawa wakati IS iliposhambulia kijiji walichokuwa wakiishi. "Waliwaua wanaume wetu wote na kuchoma vyakula na wanyama wetu wote," aliongeza.
Wengine walitusimulia hadithi kama hizo za jinsi mali zao za nafaka, kondoo na ngamia zilivyoharibiwa, na kuwaacha bila chochote. Watoto wengi wadogo tuliowaona hawakuwa na nguo wala viatu.
Fatima, na mabaki ya familia yake, walitembea mamia ya kilomita kufika Kidal kutoka nyumbani katika jimbo la Menaka mashariki mwa Mali.
Kama tulivyojionea wenyewe, kusafiri katika jangwa ni vigumu. Hakuna barabara za lami, njia ni mbaya. Utaona alama kwenye tu mchanga ya magari ambayo yamepitia hapo awali. Utaona mchanga tu hadi ukomo wa macho yako kuona.
Hakuna mengi kwa watu wa Kidal, lakini angalau wanaweza kuishi. "Tulipata maji na makazi, kwa hivyo tukabaki," Fatima alisema. Watu katika kambi hizi wanapata usaidizi kutoka kwa mashirika ya ndani lakini msaada huo hautoshi.
Pia tulikutana na Musa Ag Taher, mmoja wa wanaume wachache kambini. Wapiganaji wa Islamic State walishambulia nyumba yake pia.
“IS ilipoingia mjini tulijizika hadi walipoondoka ndipo nilipofanikiwa kutoroka na familia yangu,” alisema.
Alieleza jinsi alivyochimba shimo la kina kifupi ardhini na kujifunika kwa mchanga ili kujificha. Alifanikiwa kutoroka na watoto wake wanne.
Ingawa Kidal ni salama zaidi kuliko maeneo ambayo Fatima na Musa walitoka, lakini kuna hofu kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
Kuwageukia Wagner
Mwaka 2012, jeshi lilifanya mapinduzi, wakati waasi na wapiganaji wa Kiislamu walipochukua udhibiti wa kaskazini, na kutangaza taifa huru katika eneo hilo.
Serikali mpya ya mpito iliwaomba wanajeshi wa Ufaransa kuja kupambana na wana itikadi kali za Kiislamu. Miezi michache baada ya kuwasili kwao mwaka 2013, Umoja wa Mataifa ulituma kikosi cha kimataifa kiitwacho Minusma kulinda amani.
Viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo walichukua tena madaraka mwaka 2020 - tangu wakati huo serikali ya kijeshi imejitenga na Ufaransa, mkoloni wa zamani, na wanajeshi wa Ufaransa wamerudishwa nyumbani.
2021 serikali iliwa alika Wagner nchini Mali kusaidia usalama na hivi karibuni kundi la mamluki la Urusi litakuwa jeshi pekee la nje kutoa msaada wa kijeshi Mali. Serikali imewaambia walinda amani 12,000 wa Umoja wa Mataifa kuondoka - sasa wako katika harakati za kujiondoa.
Tulitembelea kituo cha Umoja wa Mataifa huko Kidal ambacho kinatarajiwa kufungwa mwezi Novemba. Mifuko mikubwa ya mchanga pamoja na waya vimewekwa karibu na geti kwa ajili ya usalama. Zaidi ya hayo, tuliweza kuona watu waliovalia helmeti za bluu na safu za magari meupe yenye alama za Umoja wa Mataifa.
Mlinzi wa getini aliita mtu kwenye redio yake na watu watatu wakatokea. Walituomba tuache kurekodi kwa kamera na wakaeleza kuwa kwa sababu wanajiandaa kuondoka hawataweza kufanya mahojiano.
Makundi ya ndani yana wasiwasi kwamba wakati vikosi hivi vya Umoja wa Mataifa vikiondoka, vitaacha ombwe la mamlaka kwa IS, wanamgambo wanaohusishwa na al-Qaeda na wanaotaka kujitenga wote wanaopigania udhibiti.
Inaaminika kuwa kuna takriban wanajeshi 1,000 wa Wagner nchini Mali - chini ya theluthi moja ya ukubwa wa kikosi cha Umoja wa Mataifa na kuna hofu kwamba watakuwa na ufanisi mdogo katika kukabiliana na makundi ya kijihadi.
Mapema mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulishutumu Wagner kwa kufanya ukatili pamoja na jeshi la Mali, ikielezea "simulizi za kutisha za mauaji, makaburi ya pamoja, vitendo vya mateso, ubakaji na unyanyasaji wa kingono" katika eneo la Mopti.
Pia ilieleza jinsi wanajeshi wa Mali, wakisimamiwa na wapiganaji wa Wagner, walivyowaua takriban watu 500 wengi wao wakiwa raia wasio na silaha katika kijiji kimoja. Serikali ya Mali ilikana kufanya makosa yoyote.
Katika kambi ya jirani tulikutana na kundi la watu wanaotaka kujitenga kutoka kabila la Tuareg ambao wanadhibiti Kidal. Wana wasiwasi kwamba serikali ya kijeshi ya Mali, ambayo inadhibiti eneo la kusini mwa nchi hiyo, huenda ikajaribu kuteka eneo lililosalia la kambi ya Umoja wa Mataifa wakati jeshi la kimataifa litakapoondoka. Anasema hii inaweza kusababisha mapigano mapya.
"Kama kambi hizi zitakabidhiwa kwa jeshi la Mali, Minusma itawajibika kwa kile kitakachofuata," Bilal Ag Sharif, kiongozi wa eneo la Tuareg, alituambia.
"Serikali ya Mali pia itawajibika kwa sababu inadai kitu ambacho si haki yake, na hatutakubali," aliongeza, akiweka wazi kundi lake halitaacha udhibiti wa eneo hilo bila kupigana.
Pamoja na kutoa usalama, vituo 12 vya Umoja wa Mataifa kote nchini Mali pia vinasaidia takriban ajira 10,000 za ndani. Wanaajiri watafsiri, madereva, watu wa kusambaza chakula na kutoa huduma kama vile taa za barabarani na huduma za kimsingi za afya.
"Itawaacha watu hawa bila kazi yoyote bila matumaini yoyote, bila chanzo chochote [cha mapato] kulisha familia zao," Sharif alituambia. Ana wasiwasi kuwa vikundi vya wapiganaji wa Kiislamu vitaingilia kati na kufaidika.
"Hii itayapa makundi yenye msimamo mkali fursa mpya za kuajiri vijana," alisema.
Katika kambi ya wakimbizi tuliona safu za watoto wakiwa wamekaa kwenye uwanja wa shule ya muda kwa ajili ya kujifunza. Mwalimu alikuwa akiwapiga vichwa vyao kwa fimbo walipokuwa wakisoma aya za Quran.
Wazazi wao wameuawa na IS na inaonekana jinsi ilivyo rahisi kulengwa na kuandikishwa na makundi ya wapiganaji wakati wakiendelea kukua.
Maslahi ya Urusi
Motisha ya kundi la Wagner katika eneo hilo inatiliwa shaka. Serikali ya Marekani inawashutumua Wagner kwa kuendesha migodi ya dhahabu na almasi katika mataifa mengine ya Afrika, ikisema kuwa ni "wavurugaji", wenye nia ya kufaidika na maliasili.
Siku chache kabla ya ajali ya ndege nchini Urusi, Yevgeny Prigozhin alionekana kwenye video ambayo inaelezwa alikuwa Afrika.
BBC haijaweza kuthibitisha ni wapi video hiyo ilirekodiwa, lakini Prigozhin alisema kundi hilo litaiweka Afrika "huru zaidi" na kwamba Wagner wanachimba madini na pia kupambana na wanamgambo wa Kiislamu na wahalifu wengine.
Nje kidogo ya Kidal, tulitembelea mojawapo ya viwanda vingi vya kuchakata dhahabu nchini Mali. Ni kiwanda kidogo, na mashine ndogo na sehemu kubwa ya kuyeyusha hufanywa kwa mkono.
Kwa mamia ya maeneo kama haya nchini kote, Mali huzalisha zaidi ya tani 60 za dhahabu kwa mwaka, na kuifanya kuwa miongoni mwa wauzaji watano wakuu barani Afrika wa madini hayo ya thamani.
Vikundi vya Tuareg vina wasiwasi kuwa wanajeshi wa Wagner wanaweza kujaribu kutwaa udhibiti rasilimali ya dhahabu na maeneo kama haya. Wakifanya hivyo, Sharif anaonya kwamba kutatokea umwagaji damu.
Tishio la Kikanda
Umoja wa Mataifa umeonya kwamba tishio kutoka kwa makundi ya kijihadi limeongezeka kote Mali, Niger na Burkina Faso katika mwaka uliopita.
Nchi zote tatu zimekumbwa na mapinduzi ya kijeshi, huku serikali za kiraia zikiondolewa madarakani nchini Burkina Faso mwaka 2022 na nchini Niger mwezi Julai mwaka huu.
Na kwa kuwa mustakabali wa Wagner sasa haujulikani, haijulikani ni kwa kiasi gani Mali inaweza kutegemea kundi hilo kwa usalama.