Nilikatwa kizazi kwa kuwa na virusi vya Ukimwi

Wanawake waliofunika nyuso zao

Wanawake wanne wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) nchini Kenya wamelipwa dola 20,000 kila mmoja kama fidia kwa kufungwa kizazi bila ridhaa yao. Wamesimulia BBC yale waliyopitia katika safari yao ya kutafuta haki.

Wanawake hao walipigana vita vya kisheria vya miaka tisa - na majina yao halisi hayakutumika ili kulinda utambulisho wao, ambao haukufichuliwa hata wakati wa kesi katika Mahakama Kuu.

"Imeharibu maisha yangu," Penda aliambia BBC kuhusu upasuaji aliofanyiwa muda mfupi baada ya kupata pacha katika hospitali ya serikali ya Pumwani jijini, Nairobi.

Utaratibu huo unaitwa bilateral tubal ligation (BTL) (BTL) - wakati mirija ya uzazi ya mwanamke inakatwa, kufungwa, kuchomwa au sehemu yake kuondolewa, kuifunga ili kuzuia mimba.

Baba wa mapacha wake aliondoka kabla hawajazaliwa. Mumewe alikuwa amefariki miaka michache iliyopita kutokana na matatizo yanayohusiana na VVU. Anasikitika kwamba hatapata mpenzi mwingine: "Nani atanioa ikiwa tajua sina uwezo wa kuzaa?"

Penda alibaini kuwa ana VVU alipokuwa mjamzito hivyo alitafuta ushauri wa matibabu. Wakati huo, wajawazito wenye VVU walihimizwa kujifungua kwa njia ya upasuaji na kutowanyonyesha watoto wao ili kuzuia maambukizi ya virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hizi ni njia za gharama kubwa kwa idadi kubwa ya watu kutoka jamii maskini. Siku hizi huduma nyingi za uzazi nchini Kenya ni bure. Lakini haikuwa hivyo siku za nyuma.

Baada ya kujifungua, Penda anasema aliambiwa atumie maziwa ya unga pekee. Anasema alihakikishiwa kuwa ana haki ya kupata chakula cha bure kwa ajili yake na watoto wachanga, lakini ikiwa tu alionyesha uthibitisho kwamba alikuwa akitumia uzazi wa mpango.

"Kama mama asiye na mume, hilo lilinishangaza. Tayari nilikuwa nikipambana na unyanyapaa. Sikujua nifanye nini zaidi," anasema.

Ili kumsaidia Penda kupata uthibitisho huu, mtaalamu wa lishe hospitalini alimpeleka kwa mfanyakazi wa afya wa jamii ambaye alimwambia aripoti kwenye kliniki ambapo wafanyakazi kutoka Marie Stopes, shirika kubwa la afya ya uzazi nchini Kenya, liliendesha mradi wa uzazi wa mpango.

Hapa Penda alipewa fomu, ambayo alisaini, ili kufanyiwa BTL. Kwa vile hajui kusoma, anasema hakujua kuwa alikuwa ametoa kibali chake cha kufungwa kizazi.

Utaratibu wa kudumu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Neema alisimulia tukio kama hilo katika Pumwani, ambayo ni hospitali kubwa zaidi ya umma ya uzazi nchini Kenya.

Tayari alijua hali yake ya Ukimwi wakati alipokuwa anatarajia mtoto wake wa nne. Na alikuwa na hofu ya kumwambukiza virusi mtoto wake ambaye hajazaliwa.

Anasema aliambiwa na mtaalamu wa lishe katika hospitali hiyo kwamba asipokubali kufanyiwa BTL baada ya kujifungua, hatakuwa na sifa ya kupata sehemu ya uji wa mafuta ya kupikia na unga wa mahindi, na kwamba bili yake ya afya ya uzazi haitalipwa.

Siku ya kujifungua, kabla ya kupelekwa katka chumba cha upasuaji, Neema alisema muuguzi wa zamu alimshauri kuhusu haja ya kupanga familia yake kwa kuwa tayari alikuwa na watoto watatu.

Muuguzi alimwambia apitiwe BTL na akapewa kipande cha karatasi kutia sahihi akikubaliana na upasuaji na ligation ya neli.

"Sikujua maana yake. Nilidhani ulikuwa upangaji uzazi wa kawaida," Neema aliambia BBC.

"Kama wangenieleza utaratibu vizuri, nisingetia saini karatasi hiyo."

xx

Katika kisa kingine Furaha hakumbuki mazungumzo yoyote kuhusu ufungaji uzazi kabla ya kupata mtoto wake wa tatu katika Hospitali ya Wazazi ya Pumwani.

Anakumbuka tu kuridhiakufanyiwa upasuaji ili kumzuia kumwambukiza mtoto wake mchanga VVU - na kisha kuamka akiwa na maumivu ya ajabu.

Muuguzi mmoja alieleza kwamba pia alikuwa amepitia utaratibu wa kufunga uzazi.

"Niliogopa sana kumwambia mume wangu kilichotokea. Nilijificha," aliambia BBC.

"Alipojua, alijingiza kwenye ulevi. Alikufa baada ya kugongwa na gari lililokuwa likienda kwa mwend wa kasi. Mashirika haya yaliharibu nyumba yangu."

Mwanamke wa nne, Faraja, aliiambia BBC kwamba alikabiliwa na shinikizo la kufanyiwa pasuaji wa kufunga kizazi miezi miwili baada ya kujifungua mtoto wake wa tatu.

Kwa kuwa alikuwa na VVU, alikuwa ameonywa dhidi ya kumnyonyesha mtoto wake mchanga. Lakini bila uthibitisho kwamba alikuwa akitumia mbinu ya upangaji uzazi - kufungwa kizazi - hakuweza kupokea maziwa ya mtoto bila malipo.

"Nilikuwa nimekata tamaa. Mume wangu alikuwa ameondoka. Kodi ya nyumba inanisubiri. Ningefanya nini?" anauliza.

Faraja aliiambia Mahakama Kuu ya Kenya kwamba alihudhuria kliniki ambapo alifanyiwa upasuaji.

Alipewa fomu ya kutia sahihi, lakini anasema kwamba kwa sababu hajui kusoma, hakuelewa alichokuwa akisaini. Hakuna mtu aliyemweleza kwamba alikubali kufungwa kizazi, na anasema hakupewa mbinu mbadala ya upangaji uzazi.

Walishinda kesi yao kwa sababu wataalamu wa afya hawakueleza kwa uwazi kile ambacho walikuwa wamekubaliana nacho.

Haki za kimsingi

Mwezi Septemba Mahakama Kuu ya Kenya iliamua kwa hatua ya kuwafanyia upasuaji wa kukata kizazi bila idhini yao ikikiuka haki ya kimsingi ya wanawake hao ikiwa ni pamoja na haki ya kuendeleza familia.

Fidia wanayopaswa kupokea italipwa na Marie Stopes International, Hospitali kujifungulia watoto ya Pumwani na shirika la matibabu la Médecins Sans Frontières (MSF), ambalo lilitoa ushauri wa kupanga uzazi.

Allan Maleche, mkurugenzi mtendaji wa Kelin Kenya, kundi la kutetea haki za watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi ambalo liliwawakilisha, anasema hukumu hiyo ni muhimu sana kwa wanawake wenye VVU barani Afrika ambao wameshinikizwa kufunga kizazi.

"Kwa muda mrefu sana, kesi ambazo ziliwasilishwa nchini Afrika Kusini, Namibia, zilikuwa na ugumu wa kuhusisha mango wa kukata kizazi na hali ya Ukimwi ya mwanamke husika. Umuhimu wa kesi hii ni kwamba ilithibitisha wazi kwamba si sahihi," aliambia BBC.

Msemaji wa Marie Stopes nchini Kenya aliambia BBC kwa barua pepe kwamba kisa hicho kimekuw cha muda mrefu na kigumu kwa wote waliohusika.

"Tunakaribisha azimio baada ya takriban muongo mmoja. Idhini halali ya mhusika daima imekuwa muhimu kwa kila kitu tunachofanya.

"Kama mwanachama wa jumuiya ya kimataifa ya haki za uzazi, tunaelewa unyanyapaa ambao watu wanaoishi na VVU wanaendelea kukumbana nao. Tutaendelea kufanya mafunzo na ufuatiliaji wa kina ili kuhakikisha viwango vya juu vinazingatiwa, na kamwe hatutakubali kuzembea katika huduma tunayotoa."

Women with their faces covered

MSF Ufaransa inashikilia kuwa haijawahi kufanya upasuaji wala kufanya upasuaji wa kufungua uzazi kwa sasa nchini Kenya. Inasema ikiwa mgonjwa atachagua kufanyiwa upasuaji wa kufunga uzazi, jukumu lake ni kutoa ushauri nasaha, kuwajulisha na kuwaelekeza kwenye vituo vilivyochaguliwa kufanya utaratibu huo.

"Tunatambua sehemu ya jukumu la kile kilichotokea kwa wanawake hao na kama shirika la matibabu, tunakariri kujitolea kwetu kumhudumia mgonjwa," Dk Hajir Elyas, mratibu wa mradi wa MSF nchini Kenya, aliiambia BBC.

Hospitali ya Uzazi ya Pumwani haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni yao.

Hakuna data sahihi inayoonesha ni wanawake wangapi walio na VVU nchini Kenya wamekatwa uzazi bila ridhaa yao.

Hata hivyo, utafiti wa 2012 na Mpango wa Jinsia na Vyombo vya Habari Afrika - Robbed of Choice - uliangazia wanawake 40 ambao walikuwa wamelazimishwa kufunga uzazi. Kati ya hao, ni watano tu waliofanikiwa kuwasilisha kesi.

Bw Maleche anasema wanawake walichagua kuwasilisha malalamiko ya kikatiba, badala ya kesi za jinai, kwa sababu aina hii ya kesi ina athari kubwa.

"Kesi ya jinai unaweza kutumikia kifungo, kulipa faini na hakutakuwa na manufaa ambayo wangepata wanaotafuta kufidiwa," anasema.

Lakini wanawake hao wanasema kesi yao sio tu kuhusu fidia. Wanasema hukumu ya Mahakama Kuu imethibitisha kilio chao cha haki.

Wakili wao, Nyokabi Njogu, anaafikiana na hilo: "Unafidia vipi ukiukaji wa haki za binadamu wa hali ya juu?

"Walitaka tu kukiri kwamba hili lilitokea. Hawataki wanawake ambao wameteseka kama wao waendelee na mateso hayo."