Rais Ruto azitaka Benki ya Dunia na IMF kuongeza muda wa msamaha wa madeni kwa mataifa yanayoendelea

Chanzo cha picha, Twitter
Rais William Ruto ametoa wito kwa mashirika ya fedha duniani kupanua msamaha wa deni la umma kwa nchi zinazoendelea katika hotuba yake ya kwanza kama mkuu wa nchi katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Akitoa hotuba yake mbele ya viongozi mbalimbali kote duniani, Kiongozi huyo alibainisha kuwa nchi nyingi bado zinaendelea kupata afueni kutokana na athari mbaya za janga la Covid-19 na msamaha wa madeni utasaidia sana kufanikisha miradi ya maendeleo ambayo tayari imeanzishwa na nchi hizo.
Ruto, ambaye amekuwa ofisini kwa muda wa wiki moja, alisema kuwa Kenya, kama nchi nyingine za kipato cha kati, bado inakabiliana na kushuka kwa uchumi na shinikizo la mfumuko wa bei hivyo basi haja ya kurekebisha mipango ya ulipaji wa mkopo.
"Kwa niaba ya Kenya, ninaungana na viongozi wengine kutoa wito kwa Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa na wakopeshaji wengine wa kimataifa kupanua misamaha ya madeni yanayohusiana na janga kwa nchi zilizoathiriwa zaidi, haswa zile zilizoathiriwa na mchanganyiko mbaya wa migogoro , mabadiliko ya hali ya hewa na Covid-19," Dkt Ruto alinukuliwa na gzeti la Nation Daily akisema.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Kenya
Kulingana na Daily Nation, Ruto Pia ametoa wito kwa nchi nyingine kushirikiana na nchi zinazoendelea kusaidia katika kukabiliana na janga hili.
"Kenya na Afrika nzima, kama nchi nyingine zinazoendelea, zinahitaji ushirikiano wa kimataifa ili kuepusha mzozo wa kiuchumi kutokana na janga hili," alinukuliwa na gazeti la Nation akiongezea.
Alisisitiza kuwa wito huo ukizingatiwa utasaidia nchi za kipato cha kati kuanza ajenda zao za maendeleo na kuepusha mzozo wa kiuchumi.
Maoni yake yanajiri miezi michache baada ya Hazina ya Kitaifa kufichua kuwa deni la Kenya lilikuwa Ksh8.6 trilioni. Kulingana na mchanganuo wa Hazina, deni la nje ni Ksh4.1 trilioni, huku deni la ndani likiwa Ksh3.9 trilioni.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Rais Kenya
Rais pia alihimiza mataifa ya G20 kupanua mfumo wa pamoja wa kusimamisha au kupanga upya ulipaji wa deni miongoni mwa nchi za kipato cha kati wakati wa kipindicha kujiponya dhidi ya janga la corona.
Dkt. Ruto alisema nchi zinazoendelea zimelemewa sana na ulipaji wa madeni hali inayohatarisha maendeleo kutokana na mshtuko unaosababishwa na janga hilo.
"Ninatoa wito kwa taasisi za fedha za kimataifa na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na kutoa vyombo vyote vya kifedha vilivyopo na kutoa ukwasi wa kifedha unaohitajika na kupata nafasi bora ya kifedha kwa nchi zinazoendelea kama Kenya," alinukuliwa na Daily Nation akisema.

Chanzo cha picha, Twitter/William Ruto












