Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kelele za barabarani husababisha shinikizo la juu la damu - utafiti
Sauti za injini, honi na ving'ora vinavyoungurumana na kuwafikia watu wanaoishi karibu na barabara zenye magari mengi zinaweza kusababisha shinikizo lao la damu (presha) kuongezeka, watafiti wanasema.
Watafiti wa Chuo Kikuu cha Leicester wamegundua kuwepo kwa uhusiano kati ya msongamano wa magari yenye kelele barabarani na hatari ya kuongezeka kwa shinikizo la damu.
Uchunguzi wa awali haukuweka wazi kwa namna gani kelele au uchafuzi wa hewa unaathiri shinikizo la damu.
Hata hivyo, watafiti wanasema utafiti huo mpya unaweza "kubadilisha mambo" ambao unaweza kuathiri sera zijazo za mazingira.
Hatua za afya ya umma
Samuel Y Cai, mhadhiri wa magonjwa ya mazingira katika Kituo cha Leicester cha Afya ya Mazingira na Uendelevu, alisimamia utafiti huo.
Alisema: "Huu ni uchunguzi wa kwanza Uingereza ambao ulichunguza moja kwa moja athari za kuwepo kwa kelele za muda mrefu kwenye foleni na misongamano ya barabarani na tishio la matukio ya shinikizo la damu katika kipindi cha ufuatiliaji wa miaka minane.
"Labda ni utafiti mkubwa zaidi na wa kina zaidi wa mtu binafsi ulimwenguni.
"Kulikuwa na tafiti nyingi hapo awali ambazo zilitoa uhusiano kwa muhtasari kati ya kelele za msongamano wa magari karibu na nyumba na hali ya shinikizo la damu kwa watu.
"Hata hivyo, hakuna utafiti uliokuwa na ubora wa kutosha kusogeza mbele ajenda ya sera."
Alisema ushahidi unaonyesha kuna uwezekano wa uhusiano kati ya kelele za msongamano barabarani na shinikizo la damu, uchafuzi wa hewa na sababu zingine za hatari.
"Hili ni jambo linalokwenda 'kubadilisha mchezo' linapokuja suala la kuzuia shinikizo la damu kwa mtu binafsi na kwa jamii," alisema.
"Ingawa ushahidi zaidi unahitajika, hii haipaswi kuchelewesha hatua ili kutambua kwamba kelele za magari ni sababu ya hatari ya shinikizo la damu, na magonjwa ya moyo na kwa ujumla katika maendeleo ya mwongozo wa afya na sera za mazingira."
Mwandishi mkuu wa utafiti huo alikuwa Jing Huang, profesa msaidizi katika Idara ya Sayansi ya Afya Kazini na Mazingira katika Shule ya Afya ya Umma katika Chuo Kikuu cha Peking huko Beijing, China.
"Tulishangaa kidogo kwamba uhusiano kati ya kelele za barabarani na shinikizo la damu ulikuwa madhubuti na thabiti hata baada ya uchafuzi wa hewa kurekebishwa," alisema.
Watafiti walichambua data kutoka kwa zaidi ya watu 240,000, wenye umri wa kati ya miaka 40 hadi 69 ambao walianza kufuatiliwa wakiwa hawana shinikizo la damu au presha.
Kwa kutumia takwimu na data waliwafuatilia kwa wastani wa miaka 8 na mwezi mmoja, waliangalia ni watu wangapi walipata shinikizo la damu.
Waligundua watu wanaoishi karibu na kelele za barabarani walikuwa na kwenye hatari kubwa ya kupata shinikizo la damu, lakini pia hatari hiyo iliongezeka kila "makekele yalipozidi na kuwa mengi.
Hata hivyo, watu ambao walikuwa karibu zaidi na kelele za barabarani na kwenye uchafuzi wa hewa walikuwa na hatari kubwa zaidi ya kupata shinikizo la damu, hii ni kuonyesha kuwa uchafuzi wa hewa una jukumu pia.
Watafiti walisema matokeo hayo yanaweza kusaidia hatua za afya ya umma kama vile kuweka miongozo mikali dhidi ya kelele za barabarani na kuboresha teknolojia kwenye magari ili yasipige kelele na kuimarisha muundo ya maeneo ya mijini.