Tunachokijua kuhusu mradi wa Trump wa "Project Freedom" katika mlango bahari wa Hormuz

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa watakuwa wanatoa mwongozo kwa meli ambazo zimekwama, baada ya Iran kufunga mlango bahari wa Hormuz.
Mlango huo wa bahari umesalia kufungwa baada ya mashambulizi ya Marekani na Israel kuanza dhidi ya Iran.
Siku moja tu baada ya tangazo la Trump, mapigano yanaonekana yamerejea, Marekani ikishambulia boti ndogo za Iran, huku Iran ikitekeleza mashambulizi katika mataifa ya Ghuba.
Trump alitangaza kuwa wameanza mradi wa "Project Freedom". Je hii inamaanisha nini, na itachochea mashambulizi mapya?
Trump alisema nini?
Rais Trump alisema ameomba mataifa kutoka kote duniani kuwasaidia kupitisha meli ambazo zimekwama katika mlango bahari wa Hormuz na hazina hatia.
Aliongezea kuwa Marekani itaelekeza meli zilizokwama kutoka maeneo yaliyozuiliwa hadi maeneo salama ili ziendelee na safari zao.
"Harakati ya meli ni kwa ajili ya kuwaachia huru watu, kampuni, na nchi ambazo hazijafanya kosa lolote wao ni wahanga wa vita hivi," Trump alisema katika chapisho lake kwenye Truth Social.
Iran imejibu nini?
Tishio la Trump limeonekana kutokua na ukali kama vitisho vingine alivyotoa awali.
Ilionekana ni kama Iran pia inashiriki katika oparesheni hiyo, baada ya Rais Trump kusema kuwa "Project Freedom" inahusisha Iran pia.
Ila Iran haina mtazamo saw ana rais Trump.
Taarifa kutoka kwa kamanda kuu ya kijeshi ya Iran ilisema kuwa "jeshi lolote la kigeni" ambayo itajaribu kukaribia mlango bahari wa Hormuz itashambuliwa.
Meja Jenerali Ali Abdollahi alisema kuwa kupita salama kwa meli katika mlango huo wa bahari lazima uwe katika ushirikiano na Iran wakati wote.
Jeshi la Marekani, linatekeleza vipi mpango wake Iran?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Meli 2000, na mabaharia 200,000 wamekwama eneo la ghuba tangu kuanza kwa vita nchini Iran, hii ni kulingana na shirika la kimataifa la bahari (IMO) ambayo hudhibiti safari za meli.
Kumekuwa na hofu kuhusu mabaharia hawa kukosa bidhaa muhimu, ambayo inaaathiri afya yao kimwili na kisaikolojia.
"Wakati Iran ilichagua kushambulia meli za kibiashara zisizo na hatia, Marekani imejitolea kwa niaba ya jumuiya ya kimataifa ili kulinda biashara ya kimataifa na kuelekeza meli zilizokwama zipite salama katika mlango wa bahari wa Hormuz," alisema Olivia Wales, msemaji wa Ikulu ya White House.
"Marekani inaendelea kuchukua hatua za ujasiri kwa manufaa ya dunia nzima"
Hata hivyo, Trump hakueleza jinsi meli hizo zitaweza kuondoka baada ya kuzuiwa huku akitishia kutumia nguvu.
Kituo kikuu cha kuendesha oparesheni za kijeshi za Marekani (Centcom) ilitangaza kuwa "manowari za kivita zenye makombora, zaidi ya ndege 100 za ardhini na baharini, mifumo isiyo na rubani ya nyanja mbalimbali, na wanajeshi 15,000" watatumika katika operesheni hiyo.
Katika mkutano na waandishi wa habari, kamanda wa Centcom, Admiral Brad Cooper, alisema baadhi ya helikopta za kivita zilitumika kuzamisha boti sita ndogo za Iran zilizokuwa zikilenga meli za kiraia.
Admiral Cooper aliongeza kuwa "tutafyatua risasi" dhidi ya vyombo vyovyote vya Iran vitakavyoonekana vinaingilia juhudi za kusaidia meli kupita katika eneo hilo.
Iwapo Marekani itatoa ulinzi wa kijeshi kwa meli zilizoathirika, hilo linaweza kuchochea mvutano wakijeshi na Iran.
Mick Mulroy, aliyewahi kuwa naibu msaidizi wa waziri wa ulinzi wa Marekani eneo la Mashariki ya Kati na pia mwanajeshi wa Marine aliambia BBC kuwa, anaamini mradi huo utalenga zaidi kutoa ulinzi wa anga na kujihami dhidi ya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani badala ya kusindikiza moja kwa moja meli hizo kupitia Mlango bahari wa Hormuz.
Hata hivyo, Mulroy alisema hakuna uhakika kuwa juhudi hiyo itafanikiwa kurejesha uhuru wa usafiri na biashara katika mlango huo wa bahari.
"Swali ni kama meli zitaamini uwezo wao wa kupita bila kushambuliwa, na muhimu zaidi, ni kampuni za bima," alisema.
Je, meli zinapita katika Mlango wa Hormuz?
Jeshi la Marekani linasema linaendelea kutekeleza mpango wa Trump.
Kituo kikuu cha kuendesha oparesheni za kijeshi za Marekani (Centcom) ilisema kuwa manowari za Jeshi la Wanamaji la Marekani zenye makombora zilikuwa zikifanya operesheni eneo la Ghuba "baada ya kuvuka Mlango wa Hormuz kuunga katika mradi "Project Freedom."
"Kama hatua ya kwanza, meli 2 za kibiashara zenye bendera ya Marekani zimefanikiwa kuvuka Mlango wa Hormuz na sasa zinaendelea na safari yao," Centcom ilisema. Hata hivyo, hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu utambulisho wa meli hizo za kibiashara.
Shirika la BBC halikuweza mara moja kuona meli zozote zinazoendana na maelezo ya Marekani kwenye tovuti ya ufuatiliaji wa meli ya MarineTraffic. Pia inawezekana kuwa meli hizo zilizima mifumo yao ya kutuma taarifa za eneo zilizopo au hata kutoa taarifa zisizo sahihi.
Jeshi la Iran la Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) lilikanusha taarifa hiyo ya kuwa kuna meli ambazo zimepita katika Mlango huo wa bahari.
"Kauli za Marekani hazina msingi na si za kweli kabisa," na kuonya kuwa harakati zozote zinazokiuka maelekezo ya Jeshi la Wanamaji la IRGC "zitakabiliwa vikali."
Je, Iran imeshambulia manowari za Marekani na meli nyingine?
Saa chache baada ya operesheni ya Marekani kuanza, jeshi la Iran lilisema "manowari za adui na wayahudi zimezuiwa kuingia mlango bahari wa Hormuz"
Kwa mujibu wa Centcom, Iran ilirusha makombora dhidi ya manowari za Marekani pamoja na meli za kibiashara zenye bendera ya Marekani, huku ndege zisizo na rubani na boti ndogo zikitumika kushambulia meli za kibiashara.
Katika chapisho kwenye Truth Social, Trump aliishutumu Iran kwa "kushambulia mataifa yasiyohusika," jambo lililosababisha Marekani kujibu kwa kushambulia boti ndogo za Marekani.
Falme za Kiarabu (UAE) mshirika wa Marekani eneo la Ghuba, ambayo mara nyingi imekuwa ikishambuliwa na Iran wakati wa vita ilisema kuwa meli ya mafuta inayohusishwa na kampuni ya taifa ya mafuta, Adnoc, ililengwa na ndege mbili zisizo na rubani wakati ikipita katika Mlango wa Hormuz.
Hakuna mtu aliyejeruhiwa, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema katika taarifa. Pia, makombora matatu yaliripotiwa kuzuiwa angani.













