Je, kuna hatari ya Israel kuishambulia Uturuki?

Picha ya Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan na Benjamin Netanyahu

Chanzo cha picha, BBC/Getty Images

Maelezo ya picha, Picha ya Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan na Benjamin Netanyahu
Muda wa kusoma: Dakika 3

Mataifa ya Israel na Uturuki yamekuwa na uhusiano wa kidiplomasia ambao umedorora katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, na sasa imefikia hatua ya uwezekano wa vita kuanza.

Viongozi wa mataifa hayo wamekuwa wakijibizana huku kukihofiwa kuwa mataifa hayo mawili yanaweza kushambuliana.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kupitia mtandao wa kijamii tarehe 11 mwezi Aprili, alimshtumu rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kwa kuunga mkono "utawala wa kigaidi" wa Iran na kuwauwa raia wake wa Kikurdi.

Tarehe 15 mwezi Aprili, rais Erdogan katika hotuba yake alisema kuwa "bila hata kuangazia vifo vya wakazi wa Gaza 73,000, wamejitokeza kuingilia taifa letu kupitia ndugu zetu Wakurdi"

Wachambuzi waliozungumza na BBC Turkish wanasema uwezekano wa mzozo kuzuka kati ya Uturuki na Israel uko juu sana, ila pande zote zinafanya juhudi ya kuzuia mashambulizi.

"Badala ya amani, tunaona ushindani"

Mvutano wa kisiasa kati ya Uturuki na Israel umeongezeka baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7 mwaka wa 2023, na oparesheni ya kijeshi ya Israel eneo la Gaza.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mataifa hayo yamekuwa yakinyoosheana vidole vya lawama, hadi Uturuki ikatangaza kusitisha kufanya biashara na Israel.

Profesa Tugce Ersoy kutoka Idara ya diplomasia katika Chuo Kikuu cha İzmir Katip Çelebi anaelezea mchakato kati ya nchi hizo mbili kama "siasa za ndani zinazoshikilia mateka sera za kimataifa."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Hali hii ya kila upande kuwa na misimamo mikali,mivutano, na matamshi makali inatumika kuchochea siasa za ndani ya taifa katika mataifa yote mawili"Alisema Ersoy

"Netanyahu anajaribu kuimarisha nafasi yake ya kisiasa nchini mwake"

Ersoy, ambaye amekiandika kitabu cha "Conflicting Identities in Israel: Palestinians and Jews," anasema Uturuki na Israel kila mmoja anamwona mwenzake kama "mhusika anayeyumbisha hali ya utulivu wa kikanda," na kuongezea kuwa "Tulikuwa tukielezea mahusiano ya Uturuki na Israel kama 'amani baridi' sasa imegeuka kuwa 'ushindani baridi.'"

Balozi wa zamani wa Israel Alon Pinkas anasema kwamba kauli za Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu zinaionesha Uturuki kama "mpinzani hatari."

"Matamshi ya Netanyahu na Erdogan yanaongeza hatari ya mgogoro kuzuka,"anasema.

Profesa Amnon Aran mhadhiri wa diplomasia katika Chuo Kikuu cha City St. George's London pia anasema kuwa mivutano ya kisiasa inaelekezwa zaidi kwenye siasa za ndani ya taifa.

"Kwa Uturuki na Rais Erdoğan, matamshi haya yanalenga msingi wa kiitikadi wa uungwaji mkono wa chama cha AKP. Waziri Mkuu Netanyahu pia hutumia matamshi yakuwaunga mkono wafuasi wake wa mrengo wa kulia."

Syria, Cyprus na Mashariki ya Mediterania

Tugce Ersoy anasema "Hatari ya mzozo kati ya Uturuki na Israel iko juu zaidi kuliko ilivyowahi kuwa hapo awali."

Ersoy anaeleza kuwa uwezekano wa vita vya moja kwa moja kuzuka ni mdogo, lakini ushindani unaongezeka kutoka , Syria, Cyprus, na Mashariki ya Mediterania.

"Hapa tunaona jitihada za kuanzisha mhimili wa pande zote mbili. Tunaweza kusema kwamba nchi hizo mbili zinajaribu kuunda kinga ya kijiografia dhidi ya kila moja."

"Kwenye hati za mikakati za Israel, Uturuki sasa imehamishwa na kuwekwa katika kundi la adui"

.

Chanzo cha picha, Global Sumud Flotilla/Anadolu Ajansı/Getty Images

Hotuba ya "Iran Mpya"

Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Naftali Bennett alidai katika taarifa aliyotoa tarehe 17 mwezi Februari, kuwa Uturuki ni "Iran mpya".

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia alishutumu Uturuki kwa kuiunga mkono Iran katika taarifa aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Uturuki Hakan Fidan katika mahojiano aliyofanya na Shirika la habari la Anadolu tarehe 13 mwezi Aprili, alisema kuwa

"Baada ya Iran, Israel haiwezi kuishi bila adui, lazima iunde kauli na simulizi ya uhasama. Tunaona kwamba si tu utawala wa Netanyahu, bali pia baadhi ya wapinzani wake wanajaribu kuitangaza Uturuki kuwa adui mpya kupitia lugha ya kisiasa."