BBC yafichua mbinu za matapeli wa Uganda wanaotumia mbwa kujipatia fedha kutoka kwa wapenda wanyama

Mbwa mwenye manyoya ya rangi ya kutu amelala kando ya barabara. Anaonekana mtulivu, lakini video ya TikTok inapoanza kuonyesha mwili wake wote kuanzia usoni hadi sehemu nyingine, majeraha makubwa kwenye sehemu ya miguu yake ya nyuma yanaonekana.
Mbwa huyo hapumziki. Anapumua kwa kasi, huenda alikuwa na maumivu.
Maandishi kwenye video ya sekunde 15 yanawaambia watazamaji kwamba mbwa huyu "alipata ajali" na kuwaomba "kuokoa maisha yake" kwa kutoa mchango kupitia chapisho mtandaoni.
Katika kipindi cha wiki tatu baada ya video hiyo kuchapishwa kwa mara ya kwanza tarehe 8 Januari mwaka jana, mbwa huyo alionyeshwa katika mamia ya kampeni nyingine za kuchangisha fedha, kupitia angalau akaunti kumi na mbili.
Mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii kutoka Uingereza alimpa mbwa huyo jina Russet, likiwa linaakisi rangi ya manyoya yake.
Maelfu ya dola zilikusanywa kwa ajili ya matibabu yake. Lakini hakuwahi kupona.
BBC imegundua kwamba mbwa huyu nchini Uganda alitumika katika vitendo vya utapeli wa kuomba michango kwa ajili ya wanyama wanaodaiwa kuwa katika hali ya mateso kama mkakati wa siri unaowanufaisha na ukatili huo.
Haiwezekani kuthibitisha kwa uhakika kilichosababisha majeraha kwa Russet, lakini waandishi waliweza kuunganisha baadhi ya vipande vya simulizi yake, vinavyoashiria kwamba alivumilia mateso ya muda mrefu, bila kujali chanzo chake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hadithi hii inaunganisha mji mmoja nchini Uganda na wapenzi wa wanyama walioko umbali wa takriban maili elfu.
Watu hawa hushawishiwa kutoa fedha zao kupitia picha za kusisimua hisia, uongo, na hadaa kwa mtazamo wa Kimagharibi kuhusu Afrika kama vile umaskini uliokithiri na kutojali ustawi wa wanyama.
Lakini ni mbwa kama Russet wanaotoza gharama kubwa zaidi.
Alirekodiwa katika mji wa Mityana, kituo cha biashara kilicho takriban kilomita 70 kutoka mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Mji huo umekuwa maarufu miongoni mwa wanaharakati wa haki za wanyama mtandaoni duniani kote kwa jambo moja la hadaa kuhusu makazi salama ya makazi ya mbwa.
Matapeli wa Uganda wamegundua jinsi mbwa wanavyopendwa sana barani Ulaya, Amerika Kaskazini na Australia, na jinsi ambavyo kupitia mitandao ya kijamii ni rahisi kutumia mbwa kuchangisha fedha.
"Kunao vijana wa kiume vijijini [Uganda] ambao daima wanatafuta chochote cha kufanya kwenye mtandao," anasema Bart Kakooza, mwenyekiti wa Uganda Society for the Protection and Care of Animals, akizungumza na BBC.
"Kwa upande mwingine, katika ulimwengu wa Magharibi, watu wanajali sana wanyama. Vijana hawa waligundua wanaweza kupata pesa iwapo watapata mbwa."
Haiwezekani kusema ni akaunti ngapi za mitandao ya kijamii zinaendeshwa kutoka Mityana.
Lakini kwa pamoja, zimejaa kwenye Instagram, TikTok, Facebook na YouTube kwa video za wanyama wanaoonekana kuwa na hali mbaya hasa mbwa na paka, lakini hata sungura wakiwa na maelezo ya kuomba michango ili kuwahifadhi, kuwalisha na kuwapatia matibabu.

Kwa kawaida Video hizo huonyesha mtu akionyesha mbwa kadhaa katika banda la muda, ikiambatana na ujumbe kama "mbwa wetu wana njaa" au "ni siku nyingine bila chakula katika makazi" na "tafadhali tusaidieni".
Video hizi mara nyingi hutumia kile ambacho watengenezaji wa maudhui wanaamini kitawagusa watazamaji kulingana na mitazamo yao ya awali kuhusu Afrika ikiionesha kama mahali penye uhaba wa chakula, ambapo vijana wanaopenda mbwa hulazimika kupambana na hali ngumu ili kuwalinda wanyama dhidi ya mateso katika kijamii na kutelekezwa.
Uchambuzi wa data uliofanywa na BBC Africa Eye unaonyesha kuwa video hizi zimekuwa na mafanikio katika kubadilisha watazamaji kuwa wafadhili.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, utafiti wetu umeonyesha kuwa zaidi ya dola 730,000 (£540,000) zimekusanywa kwa ajili ya makazi ya wanyama nchini Uganda kupitia mamia ya kampeni za kuchangisha fedha zilizochapishwa kwenye jukwaa la michango la GoFundMe.
Takriban asilimia 40 ya kampeni zote zilizochambuliwa na BBC zilihusishwa na Mityana.
Katika mji huo, biashara ya udanganyifu kuhusu makazi ya mbwa ni siri iliyo wazi. Wakazi kadhaa waliiambia BBC kuwa ni rahisi kuwatambua matapeli.
"Unapomwona kijana akiendesha Subaru [gari la hadhi katika eneo hili], unajua tu kwamba ni tapeli," anasema mmoja wao.
Mwingine anasema: "Matapeli ndio wanaoheshimiwa zaidi hapa Mityana."
Katika makazi hayo, waandishi wa habari wanapata mbwa wapatao 15 waliohifadhiwa kwenye boma moja, wakiwa wamelala kwenye kinyesi chao. Wengi wanaonekana kuwa na uzito mdogo na wachovu.
Lubajja anawaambia waandishi wa habari kwamba makazi hayo kimsingi yapo ili kupata fedha kutoka kwa watazamaji wa mitandao ya kijamii walioko nje ya nchi kwa udanganyifu. Anatoa ushauri kuhusu jinsi ya kuongeza mapato, na kushiriki baadhi ya mbinu, zikiwemo:
Kujifanya kwamba mwenye ardhi ametishia kuwafukuza, hivyo fedha zinahitajika kuhamisha makazi.
Kurekodi matibabu ya uongo ya mifugo, kwa mfano kuweka sindano juu ya manyoya ya mbwa badala ya kumpa sindano halisi.
Kupandisha bei ya chakula cha mbwa kwa zaidi ya mara 11.
"Mara tu unapopokea pesa za GoFundMe, unazitumia kununua gari au kujenga nyumba," anasema Lubajja huku akirekodiwa kwa siri.
"Ukishapata mfadhili mzungu, usimchukulie kama ndugu. Lazima umkamue [uchukue pesa zake]. Mmalize kabisa."
Hata hivyo, kadri shughuli hizi za uongo kama za Lubajja zilivyozidi kuenea mtandaoni, idadi inayoongezeka ya wafadhili iligundua kuwa walikuwa wamehujumiwa. Hatua mbalimbali zilianza kuchukuliwa ili kuzuia matapeli hawa.
Mbinu za wanaharakati ni pamoja na kuongeza uelewa kwa wanaoweza kuchangia, pamoja na kufichua na kuziweka hadharani akaunti zinazodhaniwa kuwa wahusika wakuu.
Wanaharakati wa mtandaoni pia wanasema kuwa zaidi ya uzembe unafanyika katika makazi ya Mityana ikiwemo kuwadhuru wanyama kwa makusudi.
Kampeni moja iliyopata nguvu kutokana na mtindo wake mkali ni We Won't Be Scammed, ambayo ina akaunti ya Instagram yenye takriban wafuasi 20,000.

Charles Lubajja huenda hakujua kwamba akaunti aliyokuwa akiwasiliana nayo ilisimamiwa na mwanamke mwenye umri wa miaka 49 anayeishi Yorkshire, kaskazini mwa Uingereza. Mwanamke huyo ni Nicola Baird, mwanzilishi wa We Won't Be Scammed, ambaye sasa amejitolea kupambana vikali na matapeli wa aina hiyo.
Baird anaeleza kuwa ana chuki kubwa dhidi ya matapeli hao, akiwaita mfano halisi wa uovu. Kama wanaharakati wengine wengi, yeye pia aliwahi kuwa mwathirika aliwahi kutuma fedha kwa mtu huko Mityana aliyedai mbwa wake alihitaji upasuaji baada ya ajali ya barabarani.
Hata hivyo, baada ya kupokea picha na video za kile kilichodaiwa kuwa matibabu, alianza kutilia shaka.
Madaktari wa mifugo aliowashirikisha walithibitisha kuwa picha hizo zilionyesha zaidi ukatili kuliko huduma ya tiba.
Tukio hilo lilimfanya atambue kuwa bila kujua alikuwa amechangia mateso ya mnyama, jambo lililomsukuma kuchukua hatua na kuanzisha mapambano dhidi ya udanganyifu na ukatili huo.
Uzoefu huo ulimfanya Nicola Baird kuamini kwamba majeraha ya wanyama yanayoonyeshwa kwenye video za mitandao ya kijamii ikiwemo kuchomwa, kukatwa na hata kupoteza viungo yanaweza kuwa yamesababishwa kwa makusudi.
Mtazamo huu pia unafanywa na makundi mengine ya wanaharakati wa mtandaoni yanayofuatilia akaunti zinazohusishwa na Mityana.
We Won't Be Scammed na wanaharakati wengine wa mtandaoni wanaamini kuwa Russet, mbwa aliyeonekana kando ya barabara na kutumika katika mamia ya video za kuchangisha fedha, huenda aliumizwa kwa makusudi, ikiwemo kuvunjwa miguu yake.
Wakati wa ufuatiliaji wa siri, Charles Lubajja anaonyeshwa video ya Russet na anamtambua kama mmoja wa mbwa wake. Anapoulizwa zaidi na waandishi wa habari, anadai kuwa mbwa huyo alipata ajali ya barabarani nje kidogo ya makazi hayo.
Hata hivyo, huenda hilo si kweli. Baada ya kuanza kuonekana mtandaoni, picha ya Russet ilianza kupakiwa kwenye akaunti tofauti tofauti, kana kwamba alikuwa akihamishwa kutoka kundi moja la matapeli hadi jingine.
Takriban wiki tatu baadaye, mfadhili mmoja kutoka Uingereza aliye kwenye mitandao ya kijamii ambaye hakutaka jina lake lijulikane aliweza kujadiliana na matapeli na kufanikisha kuachiliwa kwa Russet ili apelekwe katika kliniki ya mifugo jijini Kampala.
Isa Lutebemberwa alikwenda Mityana kumchukua mbwa huyo na kumpeleka kliniki yake kwa matibabu yaliyofadhiliwa na mfadhili huyo kutoka Uingereza.

Ikiwa mtu angekuwa na nia ya kuvunja mfupa, basi huo ndio mkao ambao angeuchagua kwa sababu ni dhaifu zaidi.
Lutebemberwa alimfanyia upasuaji Russet; ingawa alinusurika operesheni hiyo, alifariki siku chache baadaye. Alieleza kuwa ukimtazama usoni, ungeona wazi mateso makali aliyopitia, na kwamba hakustahili kufa baada ya yote aliyokuwa amepitia.
Zaidi ya hayo, Lutebemberwa alisema kuwa kisa cha Russet kilimfungua macho juu ya maumivu ambayo mbwa walioko mitaani wanaweza kuyapitia.
Alisisitiza kuwa mateso hayo ni makubwa na mara nyingi hayazingatiwi ipasavyo, jambo linaloibua maswali kuhusu ustawi wa wanyama katika mazingira kama hayo.
Shirika la BBC lilimwasiliana na Lubajja, aliyedaiwa kuwa mmiliki wa Russet, ili kutoa maoni yake kuhusu matokeo ya uchunguzi huo.
Alipoonyeshwa picha za mbwa huyo pamoja na tuhuma husika, alikana kumtambua na pia akakanusha kuwadhuru wanyama, ingawa alikiri kuwa watayarishaji wa maudhui hulipa ili kurekodi katika makazi yake.













