Kaburi la vyombo vya angani vya Urusi katika bahari ya Pasifiki

Katikati ya bahari ya Pasifiki ya Kusini, karibu kilomita 2,688 (maili 1,670) kutoka nchi kavu, ni sehemu yenye baridi kali, mawimbi makubwa na upepo mkali wa dhoruba.

"Bahari ya Kusini inaweza kuwa na mawimbi makubwa, inasisimua na inatisha kidogo," anasema Dee Caffari, baharia wa Uingereza aliyevunja rekodi ya kuwa mmoja wa watu wachache kwenye sayari hii kutembelea eneo hilo.

Katika eneo hili la mbali, kuna nafasi ndogo ya kuokolewa ikiwa utapata shida. Eneo hilo halitumiki kwa shughuli zozote za kibinadamu, kama vile meli au uvuvi. Ni sehemu iliyo na upweke, iliyotengwa na isiyo na uhai zaidi ya bahari. Hata sakafu ya bahari iko karibu futi 13,000 (maili 2.5) kutoka juu ya bahari.

Lakini kuna jambo jingine kuhusu mahali hapa; ni maarufu kama eneo la makaburi ya vyombo vya angani - ni dampo kubwa la mabaki kutoka angani.

Kati ya 1971 na 2018, mamlaka za anga za juu, ikiwa ni pamoja na ya Marekani, Urusi, Japan na Ulaya, ziliangusha zaidi ya vitu 263 vya anga katika eneo hilo lisilo na watu.

Orodha hiyo inajumuisha kituo cha anga za juu cha Mir cha enzi za Sovieti na vyombo sita kutoka katika mradi wa Salyut wa nchi hiyo, pamoja vifaa vingine ya Urusi, vyombo sita vya kusafirishia mizigo ya angani vya Japan, na vitano kutoka Shirika la Anga la Ulaya (Esa).

Hivi karibuni, dampo hili la baharini linadhaniwa kupokea sehemu ya roketi ya kapsuli ya SpaceX. Na kwa bahati mbaya, chombo cha ISS, kinatarajiwa kutua katika eneo hili miaka minane ijayo.

Taarifa zilizofichwa

Tarehe 23 Machi 2001, saa 2:59 asubuhi kwa saa za Moscow, kikundi cha wanaanga wa Urusi walitazama kutoka angani kisiwa cha Fiji katika Pasifiki ya Kusini. Hii ndiyo siku ambayo kituo cha anga za juu cha Mir "kilikufa", na kuhitimisha safari yake ya kilomita bilioni 1.9 (maili bilioni 1.2) kuzunguka ulimwengu.

Baada ya msururu wa kuchomwa kwa uangalifu, tani zote 134 za kituo cha kwanza cha anga za juu duniani zilirudi tena kwenye angahewa ya dunia na kuanguka katika eneo lisilo na watu la Bahari ya Pasifiki Kusini (SPOUA), eneo ambalo ni mara 34 ya ukubwa wa Ufaransa.

Hakuna mtu ambaye amewahi kurejesha chuma chakavu hata kimoja. Sehemu yote ya Mir ilimezwa na Bahari ya Pasifiki, na kubaki huko. Vipande vilivyobaki vimekaa kilomita kadhaa chini ya maji.

Vitu vinaposafiri kurudi kutoka anga za juu, hutembea kwa kasi ya 17,500 mph (28,164 kilomita 1 kwa saa), mabaki ya vyombo vya anga - husukuma hewa kwa nguvu kama hiyo, huvunjika na kuunda chaji ya umeme. Na kusababisha "kuungua."

"Mara nyingi mara vyombo vya angani vinapoingia tena kwenye angahewa ya dunia, hatima yao kwa kiasi kikubwa haijulikani. Tunafahamu tu vilipo, lakini hatuvioni. Hakuna mtu amekwenda chini ya bahari na chombo cha utafiti kuangalia hali ilivyo," anasema profesa wa anga kutoka chuo kikuu cha Flinders, Australia Alice Gorman.

Kuzagaa kwa uchafu

Makumbusho ya Esperance huko Australia ina kivutio chini ya maji. Kina mkusanyiko wa vitu vya kale - pikipiki kuukuu, behewa la treni la Karne ya 19, mashine mbalimbali za kilimo, kalamu ya chuma, tanki la maji lililokunjana lililoundwa kwa chuma, tufe ya ajabu ya titani na friza ya chuma.

Kitu kikubwa zaidi ni tanki ya oksijeni ya chuma, iliyofunikwa kwa plastiki yenye urefu wa futi 6 (mita 1.8). Hiki ni kipande kikubwa zaidi kuwahi kupatikana cha Skylab, kituo cha kwanza cha anga za juu cha Marekani .

Chombo hicho kilizinduliwa tarehe 14 Mei 1973 - na kurudi kwenye sayari ya dunia miaka sita tu baadaye. Nasa awali ilikuwa na matumaini kwamba Skylab inaweza kuendelea na kazi kwa muda mrefu, lakini kiliharibika mapema zaidi ya ilivyotarajiwa. Na mwanzoni mwa 1979 ikawa wazi kwamba kituo hiki cha tani 77 hakiwezi kubaki angani - iwe binadamu wanapenda au la.

Sawa na vituo vyote vikubwa vya angani, ilionekana ni muhimu kudhibiti mteremko wa Skylab, ili kiweze kutupwa baharini, mbali na shughuli za binadamu.

Lakini katika safari yake ya kurejea duniani. Katika siku yake ya mwisho, Skylab ilitakiwa idondoke katika Bahari ya Hindi kusini magharibi mwa Australia.

Mapema asubuhi tarehe 11 Julai 1979, kulikuwa na mabaki ya Skylab yaliyoanguka katikati mwa Australia. Kwa jumla, Nasa ilisema, angalau vipande 38 vyenye uzito wa zaidi ya 1,000lb (454kg) kila kimoja vilipatikana.

Sehemu kubwa ya mabaki yalianguka katika eneo la Shire of Esperance - eneo hilo likaomba sheria mpya ili Nasa itoe faini ya dola za kimarekani $400 (£329) kwa kutupa takataka, faini ambayo haijalipwa hadi leo.

Ukubwa wa Mabaki

Chombo cha Mir, ilitabiriwa kwamba kituo hiki kikubwa cha anga - ambacho kilikuwa karibu mita 13 urefu (futi43ft), na maabara tano. Kilitarajiwa kingegawanyika vipande 1,500.

Wataalamu walieleza kuwa sehemu kubwa zaidi inaweza kuwa na ukubwa wa gari ndogo. Vipande hivyo vikijumuisha matangi ya mafuta , betri, vichwa na masanduku ya kuhifadhi, na vyote viko chini ya bahari kwa sasa.

Chombo cha ISS kitakaposhuka kurudi duniani mwaka 2031, ni muhimu mabaki yadondokee kwenye eneo lisilo na watu kama vile baharini - kwani kina uzito wa takriban tani 400.

Nasa imetabiri ingawa baadhi ya sehemu za ISS zitateketea, sehemu zinazostahimili joto zinaweza kusalia. Hii inajumuisha mlolongo wa miundo ya chuma ambayo huunda uti wa mgongo wa kituo na inaweza kuwa hadi mita 18.3 (futi 60).

Kuna uwezekano kwa wanaakiolojia wa siku zijazo, kupata mabaki yaliyotupwa na wanadamu mamia au maelfu ya miaka iliyopita mara nyingi huyatumia kujifunza jinsi watu walivyoishi.