Wanasayansi wafanikiwa kwa mara ya kwanza kabisa kubaini neva za kisimi

Muda wa kusoma: Dakika 3

Wanasayansi wanatumaini kuwa utafiti huu mpya utakuwa "mwanzo wa sayansi ya kisimi".

Hatimaye wamefanikiwa kuchora ramani ya neva za kisimi, miaka mingi baada ya ramani ya neva za uume kuchorwa, kupitia utafiti mpya ambao bado haujapitiwa rasmi na wataalamu wengine wa kisayansi (peer review).

Watafiti kutoka chuo kikuu cha Amsterdam walitumia teknolojia maalumu za picha za X-ray kuunda ramani ya pande tatu (3D) ya neva za kisimi kwa wanawake wawili.

Kimsingi, mwandishi mkuu wa utafiti huo, Dr Ju Young Lee ambaye ni mtafiti katika idara ya uzazi na magonjwa ya wanawake ya Amsterdam alisema kuwa utafiti huu mpya unaweza kusaidia kuelewa vizuri jinsi kisimi kinavyofanya kazi.

"Kufahamu maumbile ni hatua ya msingi ili kuelewa jinsi yanavyofanya kazi," alisema Dr Ju Young Lee alipokuwa akizungumza na BBC Science Focus.

"Sasa kwa kuwa tuna uelewa mzuri zaidi wa anatomia yake, tunaweza kuanza kuuliza maswali zaidi kuhusu utendaji wake. Ndiyo maana utafiti huu unanivutia sana kama mwanasayansi."

Waandishi wa utafiti huo pia walisema kuwa utafiti huo unaweza kusaidia madaktari wa upasuaji kuepuka kuharibu kisimi wakati wa upasuaji wa nyonga (pelvic surgery), kwa mfano wakati wa kujifungua, upasuaji wa kuthibitisha jinsia (gender-affirming surgery), au urekebishaji baada ya ukeketaji wa wanawake.

Ramani hizo ziliundwa kutokana na picha maalumu zilizochukuliwa kutoka kwenye maeneo ya nyonga ya wanawake wawili waliokuwa wamejitolea miili itumike kwa tafiti katika chuo kikuu cha Amsterdam baada ya kufariki dunia.

Timu ya Lee ilitumia uchunguzi wa CT scan kupitisha miale ya X-ray yenye mwangaza mkubwa zaidi kupitia maeneo ya nyonga, jambo lililowaruhusu kufuatilia njia za neva za kisimi kwa usahihi ambao haujawahi kufikiwa hapo awali hadi sehemu ya elfu moja ya milimita (sawa na mara 25,000 ndogo zaidi kuliko inchi moja).

Kwa kufanya hivyo, waligundua kwamba neva kuu ya hisia, inayojulikana kitaalamu kama dorsal nerve of the clitoris (DNC), hugawanyika katika muundo unaofanana na matawi ya mti inapokaribia sehemu ya nje ya kisimi.

Hapo awali ilidhaniwa kuwa neva hii hupungua na kuishia tu, lakini utafiti huu unaonyesha tofauti. Wanasayansi hata waligundua kuwa neva hiyo inaendelea hadi kuelekea kwenye ngozi inayofunika kisimi na ngozi iliyo juu yake.

Hata hivyo, kwa kuwa utafiti huu mpya ulichunguza maumbile ya wanawake wawili tu waliokuwa wamefikia ukomo wa hedhi (postmenopausal), matokeo hayo huenda yasiwakilishe kwa usahihi neva za kila kisimi.

Utafiti huu unakuja baada ya tafiti nyingine ambazo kwa pamoja zinaendelea kubadilisha uelewa wetu kuhusu viungo vya uzazi vya mwanamke.

Kwa mfano, wanasayansi hivi karibuni waligundua kwamba kisimi kina ukubwa takriban mara mbili zaidi kuliko ilivyoonyeshwa kwenye vitabu vya anatomia, na kwamba msongamano wa neva zake unaweza kuwa mkubwa hadi mara 15 zaidi kuliko ule wa uume.

Dr Ju Young Lee alisema kuwa utafiti wake ni "mwanzo wa sayansi ya kisimi," na kwamba bado kuna mafumbo mengi ambayo hayajapataiwa majibu.

Hadi hivi karibuni, kisimi ni eneo ambalo limekuwa likipewa uangalifu mdogo sana katika utafiti wa kisayansi.

"Kuna tafiti za kisayansi takriban mara 20 zaidi kuhusu eneo lenye hisia kali kwenye uume kuliko kisimi," alisema Dr Ju Young Lee. Ni sehemu yenye hisia kali sana ya uume au kisimi, ikiwa na idadi kubwa ya miisho ya neva.

"Hii ni dalili nzuri ya jinsi ambavyo kisimi kimepewa uangalifu mdogo katika utafiti wa kisayansi." Aliongeza kuwa anatumai eneo la utafiti wa kisimi litakua zaidi.

Pia alisema anatarajia watu watachunguza miili yao wenyewe. "Ningependa pia wasomaji wachunguze miili yao," Lee aliendelea kusema. "Tofauti na uume ambao unaweza kuuona kwa kuangalia chini tu, unahitaji kioo ili kuiona vizuri kisimi. Ningependa kufanya hivyo ili kuona jinsi mwili wako ulivyo."