Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump asema majibu ya Iran kuhusu kumaliza vita 'hayakubaliki kabisa'

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, hakuzungumzia moja kwa moja pendekezo hilo, lakini alisema Jumapili: “Hatutanyenyekea mbele ya adui. Mazungumzo au diplomasia havimaanishi kujisalimisha au kurudi nyuma.”

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Beijing yathibitisha ziara ya Rais wa Marekani Donald Trump nchini China

    Beijing imethibitisha kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, atazuru China kuanzia Mei 13 hadi 15, ambapo anatarajiwa kujadili vita vya Iran pamoja na masuala ya biashara na mwenyeji wake, Rais wa China Xi Jinping.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema: “Kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping, Rais wa Marekani Donald Trump atafanya ziara rasmi nchini China kuanzia Mei 13 hadi 15.”

    Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, pia alifanya ziara nchini China.

    Hii itakuwa ziara ya kwanza ya rais wa Marekani nchini China katika kipindi cha karibu miaka tisa.

    Awali, safari ya Trump ilikuwa imepangwa kufanyika mwezi Machi, lakini ikaahirishwa kutokana na mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati.

    Mapema, China ilikuwa imesema kuwa Mlango wa Hormuz ni njia muhimu sana kwa biashara ya dunia, na kwamba kuufunga si uamuzi sahihi.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Israel yaonya mashambulizi zaidi kusini mwa Lebanon, yaamuru wakazi kuhama eneo

    Msemaji wa jeshi la Israel kwa lugha ya Kiarabu, Avichai Adraee, ametoa onyo jipya kwa wakazi wa kusini mwa Lebanon, akiwataka watu wa maeneo tisa kuhama kabla ya mashambulizi yanayotarajiwa ya Israel.

    Mapema leo asubuhi, Israel ilithibitisha kifo cha mwanajeshi wake mmoja kusini mwa Lebanon, huku pia kukiripotiwa mashambulizi ya kurushiana makombora kati ya Hezbollah na majeshi ya Israel katika maeneo mbalimbali ya mpakani.

    Jeshi la Israel lilithibitisha kifo cha mwanajeshi wake katika mapigano yaliyotokea karibu na mpaka wa Lebanon.

    Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, mwanajeshi huyo, Alexander Galvanov mwenye umri wa miaka 47, alikuwa dereva wa gari la kijeshi na aliuawa Jumapili.

    Soma pia:

  3. Waziri Mkuu wa India Narendra Modi awahimiza raia wake kupunguza ununuzi wa dhahabu

    Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, amewataka wananchi wa India kurejea kufanya kazi wakiwa nyumbani, kupunguza ununuzi wa dhahabu na kupunguza safari za nje ya nchi ili kukabiliana na ongezeko la bei ya nishati duniani linalosababishwa na mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.

    Modi alisema hatua hizo za kubana matumizi, zinazofanana na zile za kipindi cha COVID 19, zitasaidia kupunguza matumizi ya mafuta nchini India na kuhifadhi fedha za kigeni.

    India huagiza takriban asilimia 90 ya mafuta yake kutoka nje, na gharama zake za mafuta ghafi zimepanda kwa mabilioni ya dola kufuatia vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, huku Mlango wa Hormuz, njia nyembamba ya usafirishaji mafuta katika Ghuba, ukiwa umefungwa kwa zaidi ya miezi miwili na nusu.

    Wachambuzi wamesema wito wa Modi, uliotolewa katika hafla ya hadhara mjini Hyderabad kusini mwa India Jumapili, ni miongoni mwa hatua kali zaidi alizowahi kupendekeza.

    “Uzalendo si tu kujitolea maisha mpakani. Katika nyakati hizi, ni kuishi kwa uwajibikaji na kutimiza wajibu wetu kwa taifa katika maisha ya kila siku,” alisema Modi.

    “Katika hali ya sasa, lazima tuweke msisitizo mkubwa katika kuhifadhi fedha za kigeni,” aliongeza.

    Akihimiza matumizi ya usafiri wa umma kama metro, Modi alipendekeza watu washirikiane kutumia magari ili kuokoa mafuta. Pia aliwaomba wakulima kupunguza matumizi ya mbolea kwa nusu.

    Athari za kauli hizo zilionekana katika masoko ya India Jumatatu, ambapo wachambuzi wanasema maneno ya Modi yalichangia kushuka kwa zaidi ya pointi 1,000 kwa faharasa kuu ya Sensex katika biashara za mapema, kutokana na hofu ya kudorora kwa uchumi kwa muda mrefu.

    Soma zaidi:

  4. Joe McCann, mchumba wa Ashley Robinson aliyeaga dunia Zanzibar, arejea Marekani

    Wakili wa Joe McCann amethibitisha kuwa mteja wake amerudi nchini Marekani na anaendelea kuomboleza kifo cha Ashley Robinson, mwanamitandao ambaye alifariki Zanzibar wakati wa likizo yake ya kuzaliwa.

    Katika taarifa yake, wakili huyo amesema McCann amepata afueni ya kurejea nyumbani ambako anapewa muda wa kuomboleza Ashley, ambaye amemtaja kuwa mapenzi ya maisha yake. Pia ameishukuru mamlaka za Zanzibar pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa ushirikiano waliotoa katika kipindi chote cha tukio hilo.

    Ashley Janae, jina lake halisi Ashley Robinson, alikuwa Zanzibar akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa akiwa na McCann, ambaye pia alimposa wakati wa safari hiyo.

    Picha zilizowekwa mitandaoni zilionyesha wawili hao wakifurahia likizo yao, huku familia ya marehemu ikieleza kuwa alionekana kuwa na furaha katika mawasiliano yao ya mwisho naye.

    Hata hivyo, mamlaka nchini Tanzania zilitoa taarifa ya awali ikieleza kuwa kifo hicho huenda kilihusishwa na kujiua, kabla ya baadaye kusema kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo halisi cha kifo hicho.

    Hadi sasa, ripoti kamili ya uchunguzi bado haijatolewa, hali inayoendelea kuiacha familia katika sintofahamu na kusubiri majibu rasmi. Familia imeeleza kutoridhishwa na ukosefu wa taarifa za wazi kutoka kwa mamlaka.

    Ashley Robinson alizikwa wiki iliyopita nchini Marekani, wakati uchunguzi kuhusu kifo chake ukiendelea.

    Soma zaidi:

  5. Bilionea wa Afrika Aliko Dangote apendekeza kiwanda cha mafuta kijengwe Kenya - FT

    Mmoja wa matajiri wakubwa barani Afrika, Aliko Dangote, ameonesha nia ya kuanzisha kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta nchini Kenya, katika mradi unaokadiriwa kuwa na uwezo wa kuchakata mapipa 650,000 kwa siku, kulingana na ripoti ya Financial Times.

    Dangote amesema katika mahojiano kuwa mpango huo sasa unaelekea zaidi Mombasa, akibainisha kuwa mji huo una bandari kubwa na yenye kina kirefu ikilinganishwa na maeneo mengine yaliyopendekezwa awali.

    Hata hivyo, mpango huo unakuja kufuatia mjadala mkali wa kikanda, baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kueleza kutoridhishwa kwake na mpango wa awali wa kujenga kiwanda hicho katika pwani ya Tanzania. Alisema hakushirikishwa ipasavyo kabla ya tangazo la mradi huo katika mkutano wa miundombinu uliopita.

    Dangote alisema Mombasa ni chaguo lenye mantiki kutokana na ukubwa wa uchumi wa Kenya na kiwango kikubwa cha matumizi ya mafuta. Alikadiria gharama ya ujenzi wa kiwanda hicho kuwa kati ya dola bilioni 15 na 17 za Marekani.

    Alifafanua kuwa mafuta ghafi yanaweza kusafirishwa kwa njia ya baharini, hivyo kiwanda hakilazimiki kuwekwa karibu na bomba la mafuta linalopangwa kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi pwani ya Tanga, Tanzania, kwa umbali wa takriban kilomita 1,500.

    “Kenya hutumia mafuta zaidi. Ni uchumi mkubwa zaidi,” alisema, akiongeza kuwa hatma ya mradi huo sasa iko mikononi mwa Rais wa Kenya, William Ruto.

    “Kile Rais Ruto atakachosema ndicho nitakachofanya,” alisema.

    Mpango huo unajiri baada ya kukamilika kwa kiwanda kikubwa cha Dangote nchini Nigeria chenye thamani ya dola bilioni 20, huku dunia ikikabiliwa na changamoto za usambazaji wa nishati kutokana na athari za migogoro ya kimataifa, ikiwemo vita nchini Iran.

    Dangote alisema ili mradi wa Afrika Mashariki uanze, atahitaji ardhi, ufadhili wa kikanda na, muhimu zaidi, ulinzi dhidi ya mafuta ya bei nafuu yanayoingia sokoni kutoka nchi kama Russia na India.

    “Hakuna kiwanda cha kusafisha mafuta duniani kinachoweza kuhimili bila ulinzi huo,” alisema. “Kama makubaliano yatapatikana, tunaweza kuanza mwaka huu.”

    Soma zaidi:

  6. Bei ya mafuta yapaa kufuatia mvutano wa Marekani na Iran

    Kauli kali za Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Iran pamoja na majibu ya nchi hiyo zimeathiri kwa haraka masoko ya mafuta barani Asia Jumatatu asubuhi, na kusababisha kupanda kwa bei kwa takriban asilimia 3.

    Mafuta ghafi ya Brent ya Bahari ya Kaskazini yalifikia dola 104.09 kwa pipa katika biashara za mapema Jumatatu asubuhi.

    Soma pia:

  7. Abiria wa MV Hondius waendelea kurejeshwa makwao baada ya mlipuko wa hantavirus

    Makundi ya abiria na wafanyakazi wa meli ya kitalii iliyokumbwa na mlipuko hatari wa hantavirus yaliondoka melini Jumapili ili kusafirishwa kurejea katika mataifa yao, ambako watawekwa karantini kwa mujibu wa taratibu za afya za kila nchi ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

    Ndege za serikali zilizowabeba raia wa Hispania na Ufaransa zilitua Madrid na Paris Jumapili alasiri, huku abiria hao wakipelekwa hospitalini kwa mujibu wa serikali za mataifa hayo mawili.

    Mmoja kati ya abiria watano wa Ufaransa alionyesha dalili za ugonjwa huo akiwa ndani ya ndege ya kurejeshwa nyumbani, Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sebastien Lecornu, alisema kupitia mtandao wa X.

    Ndege kuelekea Canada, Uholanzi, Uturuki, Uingereza, Ireland na Marekani zilitarajiwa kuondoka kufikia saa 2:30 usiku kwa saa za eneo hilo Jumapili, huku safari za mwisho zikitarajiwa kuondoka Jumatatu kufikia saa moja usiku.

    Abiria hao watafanyiwa vipimo mara watakapowasili katika nchi zao, kabla ya kupelekwa hospitali za eneo husika, vituo vya karantini au kurejeshwa majumbani kwa ajili ya kujitenga.

    Shirika la Afya duniani - WHO - imependekeza karantini ya siku 42 kwa abiria wote waliokuwa ndani ya meli hiyo kuanzia Jumapili, kulingana na kauli ya mkurugenzi wa usimamizi wa magonjwa ya mlipuko na janga duniani, Maria Van Kerkhove, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

    Pia unaweza kusoma:

  8. El- Classico: Barcelona yailaza Real Madrid

    Marcus Rashford alifunga mkwaju wa fauli na kuwasaidia Barcelona kuwalaza wapinzani wao Real Madrid na kufanikiwa kunyakua taji lao la 29 la La Liga huku zikiwa zimesalia mechi tatu kumalizika kwa msimu.

    Mshambuliaji huyo wa Uingereza aliwaweka wenyeji mbele kabla ya Ferran Torres kufunga bao la pili kwa umaliziaji mzuri wakati kikosi cha Hansi Flick kikishinda mechi ya El Clasico kwenye Uwanja wa Nou Camp.

    Wachezaji wote wawili walimkimbilia kocha wao mkuu walipofunga baada ya babake kuaga dunia wikendi.

    Barcelona sasa wako nyuma ya Real madrid kwa mataji baada ya kunyakua ligi kuu ya Uhispania kwa misimu miwili mfululizo.

    Wameshinda mechi 11 kwenye La Liga hadi kutwaa ubingwa na kuwaongoza wapinzani wao kwa pointi 14 zisizoweza kuepukika.

    Kiwango kizuri cha Barcelona nyumbani kimewasaidia kutwaa ubingwa, kwani huo ulikuwa ushindi wao wa 18 kati ya michezo 18 waliyocheza mbele ya mashabiki wao.

    Mshambuliaji wa Manchester United anayecheza kwa mkopo Rashford alianza vyema wakati alipopiga mpira wa adhabu wa mapema hadi kwenye kona ya juu na kumpita kipa wa Real Thibaut Courtois, ambaye mguso wake hafifu haukuweza kuuzuia mpira nje.

    Na baadaye kunako dakika ya 18 mchezo mzuri wa Dani Olmo aliyemtengenezea Torres pasi nzuri na kufunga goli la pili.

    Aurelien Tchouameni alianzishwa katika mechi hiyo kwa upande wa Real Madrid siku chache baada ya kugombana na mchezaji mwenzake Federico Valverde, ambaye alichanganyikiwa wakati wa mabishano na kukosa mchezo.

    Meneja wa Real aliye na shinikizo la chini, Alvaro Arbeloa hakuweza kuitia moyo timu yake, huku Gonzalo Garcia akishindwa kufunga moja ya nafasi chache walizopata kwenye kipindi cha kwanza.

    Sauti za "Mabingwa" zilisikika karibu na Nou Camp iliyoboreshwa huku saa zikiyoyoma kuthibitisha kwamba wenyeji walikuwa wamehifadhi taji lao la La Liga, huku Robert Lewandowski akikaribia kufanya matokeo kuwa 3-0.

    Soma zaidi:

  9. Trump asema majibu ya Iran kuhusu kumaliza vita 'hayakubaliki kabisa'

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameyakataa vikali majibu ya Iran kwa mapendekezo ya Marekani ya kumaliza vita, akiyataja kuwa “hayakubaliki kabisa”.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim la Iran, Tehran iliwasilisha mapendekezo yake kupitia Pakistan, ambayo imekuwa ikipatanisha pande hizo.

    Pendekezo hilo lilitaka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika maeneo yote, kuondolewa kwa mzingiro wa majini uliowekwa na Marekani pamoja na dhamana kwamba hakutakuwa na mashambulizi mengine dhidi ya Iran.

    Usitishaji mapigano uliolenga kufungua njia ya mazungumzo ya kumaliza vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel mwezi Februari umeendelea kuheshimiwa kwa kiasi kikubwa, licha ya mashambulizi ya hapa na pale yaliyoripotiwa.

    Mapema wiki hii, Trump alisema tena kuwa vita nchini Iran “vitamalizika haraka”.

    Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema akiba ya Iran ya urani iliyorutubishwa lazima iondolewe kabisa kabla ya vita kutangazwa kumalizika.

    “Bado kuna vituo vya kurutubisha urani vinavyopaswa kusambaratishwa,” Netanyahu alisema katika mahojiano na kipindi cha 60 Minutes cha CBS.

    Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, hakuzungumzia moja kwa moja pendekezo hilo, lakini alisema Jumapili: “Hatutainamisha vichwa vyetu mbele ya adui. Mazungumzo au diplomasia havimaanishi kujisalimisha au kurudi nyuma.”

    Kupitia mtandao wake wa Truth Social, Trump aliandika: “Nimesoma majibu kutoka kwa wanaojiita ‘wawakilishi’ wa Iran. Siyakubali kabisa.”

    Chombo cha habari cha Marekani cha Axios kiliripoti kuwa waraka wa Marekani wenye vipengele 14 unajumuisha masharti ya kusitishwa kwa urutubishaji wa nyuklia wa Iran, kuondolewa kwa vikwazo pamoja na kurejeshwa kwa uhuru wa usafiri wa majini katika Mlango wa Hormuz.

    Ripoti hiyo ilinukuu maafisa wawili wa Marekani pamoja na vyanzo vingine viwili visivyotajwa majina vikisema kuwa utekelezaji wa masharti mengi unategemea kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho.

    Iran imeendelea kuzuia njia ya Hormuz, hatua iliyochangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

    Kwa upande wake, Marekani imeendelea kuweka mzingiro katika bandari za Iran ili kuishinikiza Tehran kukubali masharti yake, jambo ambalo limeongeza hasira nchini Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 11 Mei 2026.