Kwanini Canada inaongoza kwa wizi wa magari?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Vyuma vya kuzuia wizi wa gari
    • Author, Nadine Yousif
    • Nafasi, BBC

Logan LaFarniere aliamka asubuhi moja ya Oktoba 2022 na kukuta gari lake halipo. Lori lake aina ya Ram Rebel, alikuwa amelinunua mwaka mmoja na nusu uliopita.

Kamera ya usalama ilinasa wanaume wawili waliovalia kofia, wakati wa usiku waliingia kwenye gari hilo nje ya nyumba yake Milton, Ontario, na kuliendesha na kutoweka nalo.

Miezi michache baadaye, lori hilo hilo lilionekana kwenye tovuti ya magari yanayouzwa nchini Ghana, umbali wa kilomita 8,500.

Pia unaweza kusoma

Takwimu zinasemaje?

Mkasa wa LaFarniere si mkasa pekee. Mwaka 2022, zaidi ya magari 105,000 yaliibiwa nchini Canada - gari moja huibiwa kila dakika tano.

Miongoni mwa waathiriwa ni waziri wa sheria wa Canada, gari lake la serikali, Toyota Highlander XLE liliibiwa mara mbili na wezi.

Mapema msimu huu wa kiangazi, Interpol iliiorodhesha Canada miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa wizi wa magari kati ya nchi 137.

“Ni jambo la kushangaza,” anasema msemaji wa Interpol, kwani nchi hiyo ilianza kuunganisha taarifa zake na shirika hilo la kimataifa mwezi Februari tu.

Mamlaka zinasema magari yanapoibiwa, hutumika kutekeleza uhalifu, kuuzwa ndani ya nchi kwa Wakanada wengine, au kusafirishwa nje ya nchi ili kuuzwa tena.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Interpol imegundua zaidi ya magari 1,500 duniani kote ambayo yameibiwa kutoka Canada tangu Februari, na mengine zaidi ya 200 yanaendelea kufuatiliwa kila wiki, katika bandari za nchi nyingine.

Wizi wa magari ni janga lililotangazwa kuwa "tatizo la kitaifa" na Ofisi ya Bima ya Canada, ambayo inasema watoa bima wamelazimika kulipa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 1 katika matukio ya wizi wa magari mwaka jana.

Tatizo hilo limezilazimisha mamlaka za polisi kote nchini kutoa taarifa kwa umma kuhusu namna ya kulinda magari dhidi ya wizi.

Mbali na hilo, baadhi ya Wacanada wanafanya juhudi zao binafsi kwa kuweka vifuatiliaji vya GPS kwenye magari yao, na kuweka walinzi binafsi katika vitongoji.

Na wanaoweza kumudu, wameweka vizuizi vya vyuma katika maegesho yao - sawa na vizuizi katika benki na balozi - ili kujaribu kuzuia wezi.

“Kuenea kwa wizi wa magari nchini Canada ni jambo la kushangaza kutokana na idadi ya watu nchini humo ilivyo ndogo ikilinganishwa na Marekani na Uingereza - nchi nyingine zenye viwango vya juu vya uhalifu huo,” anasema Alexis Piquero, Mkurugenzi wa Ofisi ya Justice Statistics, Marekani.

"(Canada) pia haina miji mingi ya bandari kama Marekani," anasema Piquero.

Marekani, Canada na Uingereza zote zina tatizo kubwa la wizi wa magari tangu janga la Covid-19. Kiwango cha wizi nchini Canada ni mara 262.5 kwa kila watu 100,000.

Ni kiwango kikubwa kuliko nchini Uingereza na Wales, ambako ni magari 220 kwa kila watu 100,000, kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka kila nchi.

Takwimu za Canada, ziko karibu na zile za Marekani, kuna wizi wa magari 300 kwa kila watu 100,000, kulingana na takwimu za 2022.

Sababu za wizi Canada

df

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha, Magari yanayoibiwa Canada mara nyingi husafirishwa nje ya nchi kupitia bandari kama ya Montreal

Kuongezeka kwa wizi katika miaka ya hivi karibuni ni kwa sababu ya uhaba wa magari uliosababishwa na covid. Janga hilo limeongeza mahitaji ya magari yaliyotumika na mapya.

“Pia kuna soko la kimataifa linalokua la magari, na kufanya wizi wa magari kuwa mzalishaji mkuu wa mapato kwa vikundi vya uhalifu,” anasema Elliott Silverstein, mkurugenzi wa mahusiano ya serikali katika Chama cha Magari cha Canada.

Silverstein anasema, jinsi bandari za Canada zinavyofanya kazi zinakuwa hatarini zaidi kwa aina hii ya wizi kuliko nchi nyingine.

"Katika mfumo wa bandari, uwangalizi mkubwa hufanywa kwa kile kinachoingia, kuliko kile kinachotoka nchini," anasema, akiongeza, “magari yanapopakiwa kwenye makontena ya meli inakuwa vigumu kuyakagua.”

Mwezi Oktoba, Polisi wa Toronto walitangaza uchunguzi wa miezi 11 ambapo walipata magari 1,080 yenye thamani ya karibu dola za Canada milioni 60. Na zaidi ya mashtaka 550 yalifunguliwa.

Katikati ya Disemba na mwisho wa Machi, maafisa wa mipakani na polisi, walipata karibu magari 600 ya wizi, kwenye Bandari ya Montreal baada ya kukagua kontena 400 za usafirishaji.

“Operesheni za aina hii, hata hivyo, zinaweza kuwa ngumu kutokana na wingi wa bidhaa zinazopita kwenye bandari hiyo,” wataalamu wanasema.

Takribani kontena milioni 1.7 zilisafirishwa kupitia Bandari ya Montreal mwaka 2023 pekee.

Wafanyakazi wa bandari mara nyingi hawana mamlaka ya kukagua makontena, na katika maeneo yanayodhibitiwa na forodha ni maofisa wa mpakani pekee ndio wanaweza kufungua kontena bila kibali.

Shirika la Mipaka ya Canada (CBSA), limekumbwa na ukosefu wa wafanyakazi, kulingana na ripoti iliyowasilishwa na chama chake kwa serikali mwezi Aprili.

Teknolojia ya kizamani ni tatizo

Patrick Brown, meya wa Brampton - jiji lingine la Ontario lililoathiriwa sana na wizi wa magari - hivi karibuni alitembelea Kituo cha Makontena cha Bandari ya Newark huko New Jersey, ili kulinganisha mbinu za ukaguzi kati ya Marekani na Canada.

Aliliambia gazeti la National Post, mamlaka za Marekani "zinatumia skena. Wanapima uzito. Wanafanya kazi kwa ukaribu na wasimamizi wa sheria wa eneo hilo.”

"Haya ni mambo ambayo hatufanyi nchini Canada," alisema.

Mwezi Mei, serikali ya Canada ilisema itawekeza mamilioni ili kuimarisha uwezo wa maafisa wa kufatilia makontena ya usafirishaji. Polisi pia watapata pesa za ziada ili kukabiliana na wizi wa magari katika jamii zao.

Lakini Silverstein anaamini, kipande cha fumbo kinachokosekana ni watengenezaji wa magari wenyewe.

"Kila mtu anazungumzia namna ya kuipata gari yako baada ya kuibiwa, lakini kwa nini hatufanyi iwe vigumu kwa magari kuibiwa .”

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah