WARIDI WA BBC: Ninaishi na Virusi vya Ukimwi na nimekuwa na wapenzi wasio na maambukizi

Na Anne Ngugi

BBC Swahili

Doreen

Chanzo cha picha, Doreen

Sio kawaida kwa mwathiriwa yeyote wa ugonjwa ambao ni sugu kujitokeza kuzungumzia hadharani kuhusu mahangaiko anayopitia, ila kwake Doreen Moraa mwanamke mwenye umri wa miaka 30 kutoka Kenya anayeishi na virusi vya HIV amepiga moyo konde na kuzungumzia waziwazi changamoto na maisha kwa macho ya anayeishi na virusi vya HIV vinavyosabaisha ugonjwa wa ukimwi.

Je anamudu vipi mahusiano ya kimapenzi?

Japo Doreen alifahamishwa kuhusiana na hali yake pindi alipohitimisha miaka 13, anasema kuwa safari imekuwa ndefu mno hasa kwa kuwa yeye ni miongoni mwa watoto wanaozaliwa na kuambukizwa na mama.

Kwa hiyo tafsiri yake ya mwanzo kuhusu virusi na mtazamo wa jamii kuhusiana na ugonjwa wa Ukimwi kwa ujumla ulikuwa unampa hofu mno hapo mwanzo.

Kwahiyo hata wakati anavunja ungo alikuwa na wasiwasi mwingi kuhusu jinsi maisha yake yatakavyokuwa.

Mojawapo wa sehemu katika maisha yake alikuwa ana wasiwasi nayo ilikuwa ni jinsi gani atamudu kuwa na mpenzi .

”Kando na kuwa nilikumbwa na unyanyapaa mwingi wakati jamaa zangu walifahamu kuhusu hali yangu , nilikuwa najiuliza basi itakuwa vipi wakati nitaingia ulimwengu wa mapenzi ” Doreen anasema.

Doreen

Chanzo cha picha, Doreen

Wakati mmoja anakumbuka alikutana na mwanaume mmoja ambaye walianza kufahamiana, mwanadada huyu tayari alikuwa amemfahamisha kuwa yeye alikuwa anaishi na virusi lakini mwanaume huyo alikataa kata kata na kumweleza kuwa hana muonekano wa mwanamke anayeishi na HIV.

Kilichofuata ni wao wawili kuelekea kituo cha kupima virusi vya HIV, na kama Doreen alivyotarajia matokeo yake yaliashiria HIV+ na matokeo ya rafiki wake yalikuwa ni HIV-.

Mwanadada huyu anakumbuka jinsi mambo yalivyobadilika ghafla kuanzia wakati huyo rafiki yake alimweleza kuwa alikuwa na shughuli nyingi sana na kuanzia wakati huo hakumtafuta tena.

Doreen

Chanzo cha picha, Doreen

Ila mwanadada huyu anakubali kuwa amekuwa kwenye mahusiano kadhaa ya kimapenzi na wanaume ambao hawana virusi, na kujamiana nao, Anaelezea kuwa kuna hatua ambazo wao wamekuwa wakichukua ili kuhakikisha Doreen hatawaambukiza virusi hivyo.

Nilipomuuliza ni vipi inawezekana kwamba huwaelezea wanaume kuwa ana virusi na bado wanakubali kuwa na uhusiano naye.

”Sio kitu cha kustaajabisha sana kusikia kuwa nimekuwa na urafiki na wanaume ambao hawana virusi, na mahusiano yamekuwa kama kawaida. kwangu mimi nadhani kuwa jamii haijaelemishwa vya kutosha kuhusiana na HIV na jinsi mtu anaweza kuambukizwa ”Doreem anasema.

Japo kwa wakati huu alitueleza kuwa hayuko kwenye mahusiano yoyote ila ana matumaini katika siku za usoni kufunga ndoa na kuwa na familia yake.

Changamoto za kuishi na HIV ni zipi kwa mujibu wa Doreen

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika Familia yake Doreen, ni yeye na mamake wanaoishi na virusi vya HIV.

Mwanadada huyu anasema kuwa baba yake hakuwa na virusi ilhali mama alipatikana na virusi hivyo, anaeleza kuwa mahangaiko kati ya mama na binti wake yalikuwa hasa ni jinsi gani watapona.

Doreen anakumbuka kuwa mara nyingi, waliandamana na mama yake katika maeneo tofauti kutafuta tiba, kwa mfano maombi, kutumia majani na bidhaa tofauti wakiwa na matumaini watapona .

”Nakumbuka wakati mmoja tulisafiri nchi jirani kupata tiba ya kienyeji, na mimi niliacha hata kutumia dawa zangu kwa miaka 2 nikiwa na matumaini kuwa nitapona , mwisho wa siku sikupona bali kinga ya mwili wangu ilidhoofika sana wakati huo ”anakumbuka Doreen.

Na kwa hayo anawasihi watu wanaoishi na virusi vya HIV kufuata maagizo ya kutoka hospitalini hasa kuhakikisha kuwa wanameza dawa kila siku. Kingine chochote ambacho hakijafanyiwa uchunguzi anapuuza na kusema kuwa watu wasihatarishe maisha yao.

Kwa sasa Doreen ni mwanaharakati nchini Kenya, akifanya kazi na vijana na watoto ambao wanazaliwa na virusi. Mwisho wa siku hawaelewi kinachofanyika kwa hiyo yeye huchukua jukumu la kutoa ushauri nasaha na jinsi vijana wanaweza kumudu maisha wakiwa wameathirika.