Wasiwasi waongezeka juu ya udhibiti wa madini ya uranium ya Niger baada ya mapinduzi

Na Yusuf Akinpelu

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Mapinduzi ya hivi karibuni nchini Niger yamesababisha hofu juu ya mustakabali wa nchi hiyo tajiri ya usambazaji wa madini ya uranium, na chuma cha mionzi kinachotengeneza mafuta ya kiwanda cha nyuklia.

Niger ni nchi ya hivi karibuni katika kanda wa Sahel barani Afrika kuchukuliwa na utawala wa kijeshi, kufuatia mapinduzi kama hayo katika nchi jirani za Bukina Faso na Mali.

Hali ya kisiasa nchini humo imezua wasiwasi wa kiuchumi na kiusalama.

Niger ni nchi ya saba kwa uzalishaji mkubwa wa madini ya uranium duniani. Ingawa ni kwa asilimia nne tu ya uzalishaji wa kimataifa, ni muuzaji muhimu. Katika 2022, 25% uranium iliyoagizwa na Umoja wa Ulaya ilitoka Niger, kulingana na shirika la nyuklia la Muungano wa Ulaya (EU), Euratom.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ni Kazakhstan tu, nchi iliyopakana na Urusi na China, iliyosafirisha uranium zaidi nchini Ufaransa kuliko Niger.

Mapinduzi ya mwezi uliopita yameweka ugavi huu mashakani. Kuna hofu kwamba serikali mpya inaweza kupunguza utoaji wa madini ya uranium kulingana na vikwazo vya Ulaya na kususia misaada, ingawa hawajasema watafanya hivyo.

Ikiwa hii ilitokea, Euratom inasema kuna vifaa vya kutosha vya uranium katika soko la dunia kukidhi mahitaji ya EU kwa miaka mitatu, ikimaanisha hakuna tishio la haraka kwa uzalishaji wa umeme.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kampuni ya mafuta ya nyuklia ya Ufaransa Orano, ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama Areva, ambayo inaendesha mgodi katika mji wa kaskazini magharibi mwa Niger wa Airlit, pia imesema operesheni zake zitaendelea, licha ya jeshi kuchukua madaraka.

Katika miaka ya hivi karibuni, Ufaransa imepunguza usambazaji wake wa madini ya uranium ili kujumuisha uagizaji kutoka nchi nyingine kadhaa, ambazo wataalamu wanasema zinaweza kusaidia kuziba pengo hilo ikiwa kuna upungufu wa usambazaji kutoka Niger.

Lakini wataalamu wa masoko wanasema kuwa vituo hivyo vinaangukia katika eneo la udhibiti wa Urusi na China.

Ikiwa Niger itaondoa Wafaransa na kuhamia Urusi au Uchina, itafanya soko kuwa gumu kwa mahitaji ya Magharibi, Ben Godwin, mtaalam wa usimamizi wa hatari za kisiasa, aliiambia DW News.

Kazakhstan, ambayo inadhibiti karibu 40% ya uzalishaji wa uranium duniani, hivi karibuni iliuza hisa ya 50% katika moja ya migodi yake kubwa ya uranium kwa Urusi. China pia imekuwa ikiwekeza sana katika nchi hiyo ya Asia ya Kati.

Shirika la kitaifa la nyuklia la China tayari limeingiza karibu dola milioni 480 nchini Niger kwa ajili ya utafutaji wa madini ya uranium, kwa mujibu wa Wizara ya Biashara ya China, wakati ikitafuta kushikilia hisa zaidi katika udhibiti wa rasilimali za dunia.

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Umoja wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, unaangalia kuondoa utegemezi wa madini ya uranium ya Urusi. Wakati Umoja wa Ulaya ulipopitisha vikwazo dhidi ya mafuta na gesi ya Urusi, iliacha madini ya uranium, Urusi inaonekana kuendelea hivyo. Tishio lolote la usambazaji nchini Niger au mahali pengine popote linamaanisha kuwa uranium ya Urusi itaendelea kuwa na umuhimu, Bwana Godwin alisema.

Wakati huo huo, kupunguzwa kwa usambazaji kunaweza kuwa gharama kubwa kwa Niger pia. Kwanza, Niger italazimika kujitahidi kupata mshirika mwingine wa mgodi na kuuza uranium yake.

Pili, pia itamaanisha mapato kidogo kutokana na mauzo ya uranium kwa nchi hiyo maskini isiyo na bandari ambapo misaada ya kigeni huchukua asilimia tisa ya Pato la Taifa na karibu 40% ya bajeti ya serikali.

Baadhi ya washirika wa mataifa ya magharibi wameashiria kuwa huenda wakafuata mkondo wa Marekani katika kutoa misaada ya aina fulani kwa Niger, ambayo inaweza kusababisha kushuka kwa uchumi wa watu milioni 25 wa Niger, ambao tayari asilimia 40 kati yao wanaishi katika umasikini.

Nchi hiyo inashika nafasi ya chini kabisa katika orodha ya maendeleo ya binadamu ya Umoja wa Mataifa, ikishika nafasi ya 189 kati ya nchi 191.

Ikiwa Niger itapoteza Ufaransa kama mnunuzi wa madini yake ya uranium, uongozi wake mpya wa kijeshi unaweza kugeuka China badala yake. China kwa sasa ni mwekezaji wa pili mkubwa wa kigeni wa Niger baada ya koloni lake la zamani Ufaransa.

Wakati hakuna uthibitisho wa uhakika wa kuhusika kwa Urusi katika mapinduzi hayo, wachambuzi wanaounga mkono serikali ya Niger wamesifu waziwazi hatua hiyo.

Sasa kuna wasiwasi kwamba mamluki wa Urusi wa Wagner wanaweza kutumia hali hiyo ili kupata fursa ya madini ya uranium na rasilimali nyingine za asili kama almasi, dhahabu na mafuta.

Ushawishi wa Urusi pia unaongeza wasiwasi wa usalama. Katika nchi jirani ya Mali, maelfu ya wapiganaji wa Wagner walifurika nchini humo baada ya uvamizi kama huo wa kijeshi. Tangu wakati huo, Mali imeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya vurugu yanayofanywa na wanamgambo wenye itikadi kali.

Hivi sasa Marekani na Ufaransa zinaendesha kambi za kijeshi nchini Niger ili kukabiliana na shughuli za jihadi nchini humo na eneo pana.

Hata hivyo, mustakabali wa kambi hizi sasa hauna uhakika na kuna wasiwasi kwamba waasi watatumia fursa ya ukosefu wa utulivu wa kisiasa kueneza uwezo wao.

Hii inaelezea kwa nini jumuiya ya kiuchumi ya kikanda, Ecowas, na washirika wao wa Magharibi wanashinikiza kurejesha utaratibu wa kikatiba nchini Niger.

Wanahofia kuwa taifa dhaifu linaweza kusababisha madini ya urani ya Niger - yanayotumiwa katika mazingira ya kiraia na kijeshi - kuanguka katika mikono isiyo sahihi katika eneo ambalo wanamgambo wa Kiislamu wanaendesha shughuli zao, na Urusi na kundi la Wagner wanapanua ushawishi wao.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mataifa mengine kadhaa wameelezea kuunga mkono kikamilifu Ecowas katika juhudi zake za kurejesha utaratibu wa kikatiba nchini Niger.

Ecowas imewapa viongozi wa mapinduzi katika mji mkuu wa Niger, Niamey, muda wa siku saba wa kuachia madaraka au kukabiliana na uingiliaji wa kijeshi. Hii ilimalizika siku ya Jumapili.

Tangu wakati huo, Ecowas imetangaza kuwa itafanya mkutano wa kilele katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Alhamisi kujadili hali ya kisiasa na usalama inayoendelea.

Hadi wakati huo, hali ya wasiwasi inaning'inia juu ya Niger na eneo pana.