‘Baada ya kuwekewa kifaa hicho, nilianza kuvuja damu na kupatwa na maumivu ya kichwa na mgongo’

Baada ya kupata mtoto wake wa nne, Kelli Patrícia da Luz mwenye umri wa miaka 43 alikuwa akingojea kwa zaidi ya miaka miwili kuunganishwa kwa mirija ya kufunga uzazi wa kudumu alipopokea simu kutoka kwa hospitali ya umma huko Brasília, mji mkuu wa Brazili.

Njia mbadala ya mpango wa uzazi aliyofahamishwa Kelli ilionekana kupendeza.

"Madaktari walinialika kwenye mazungumzo na kuniambia kuhusu kifaa ‘Essure’. Walielezea kama njia ya mapinduzi, isiyo na maumivu bila kukatwa popote, ambayo haihitaji kutatiza muda wa kazi au shughuli za kila siku. Nilikubali haraka kuwa ni chaguo bora zaidi kwa mpango wa uzazi," anasema Kelli.

Kulikuwa na kasoro moja, hata hivyo: Ikiwa angejuta kutumia kifaa hicho baadaye, utaratibu huo haungeweza kutenduliwa, aliambiwa.

Kuondolewa kwa kifaa hicho kutahitaji tumbo la uzazi liondolewe kabisa.

Alitia saini kuashiria kuwa amekubali.

Essure iliingizwa kupitia utaratibu unaotumika kuchunguza sehemu ya ndani ya tumbo la uzazi kwa kutumia kifaa chembamba kinachofanana na kalamu.

Kawaida, madaktari huingiza kifaa kupitia mlango wa kizazi ili kutazama sehemu ya ndani ya tumbo la uzazi na upande wa ndani uliowazi wa mirija ya uzazi ambapo Essure inafaa kuwekwa.

Hapa ndipo changamoto ya kwanza ilipojitokeza, anaeleza Carlos Politano, mjumbe wa Kamati ya Uzazi wa mpango ya Shirikisho la Brazil la Vyama vya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi.

“Mtaalamu anatakiwa kuweka kifaa hicho kwenye mianya ya mirija ya uzazi kwa tahadhari kubwa ili kuepuka kutoboka,” anasema.

Kulingana na Bayer, kampuni inayotengeneza kifaa Essure, mwili hutengeneza mmenyuko wa uponyaji wa kikaboni ambao hufunga mrija wa uzazi kabisa kwa takriban miezi mitatu baada ya utaratibu na kuzuia kukutana kwa manii na yai.

Madhara ya kudumu

Hata hivyo, Kelli alianza kupata maumivu mara tu baada ya kuwekewa kifaa hicho.

"Baada ya upasuaji nilikuwa na matatizo ya tumbo, maumivu ya nyonga, kutokwa na damu, maumivu ya viungo, na kipandauso kikubwa. Zaidi ya hayo, nilipatwa na maumivu makali ya kiuno, ambayo yalinizuia kutembea," anasema.

Mnamo mwaka wa 2017, ripoti za athari mbaya zinazowapata wanawake katika nchi mbalimbali baada ya kuwekwa kifaa hicho zilijitokeza. Huu uliashiria mwanzo wa kusitishwa kwa matumizi ya kifaa Essure duniani kote.

Nchi kama vile Brazili, Canada na Muungano wa Ulaya zilisitisha matumizi ya kifaa hicho haraka.

Nchini Marekani, Mamlaka ya Chakula na Dawa (FDA) ilianza kutoa onyo dhidi ya matumizi ya kifaa hicho kupitia "kisanduku cheusi", ikionyesha kwamba inaweza kuwa na madhara makubwa, ambayo baadhi yake yanaweza "kuhatarisha maisha".

Kwa kupungua kwa mauzo kwa 70%, mtengenezaji aliondoa kifaa hicho kwenye soko la Marekani mnamo mwaka 2018 na baadaye akafanya vivyo hivyo katika nchi zingine.

Leo, Essure haiuzwi tena popote duniani.

Marufuku hiyo, hata hivyo, haikubadilisha chochote katika maisha ya kila siku ya wanawake ambao tayari walikuwa wameweka kifaa hicho.

"Kwa wale ambao waliendana vizuri na kifaa Essure, hakukuwa na dalili ya mabadiliko yoyote," anasema Politano.

Lakini kwa idadi kubwa ya watumiaji, utasa wa kudumu ulikuja na athari zingine za milele.

"Nilikuwa mwanamke mwenye shughuli nyingi na maisha ya kawaida katika jamii, lakini nilianza kupata maumivu makali ya nyonga na tumbo, kutokwa na damu, maumivu ya matiti na mguu, na maumivu ya kichwa yanayodhoofisha," anasema Liliane Feitosa, 44, kutoka Brasília.

Anaeleza kuwa pia alipata mzio wa nikeli - nyenzo iliyo kwenye kifaa hicho - ambayo iliathiri ubora wa maisha yake kwa kiasi kikubwa, na kusababisha mwili kuwasha, maumivu na kutoa harufu mbaya ambayo ilimfanya ajisikie kutengwa.

"Tulihadaiwa. Huwezi kufikiria jinsi maisha yanavyokuwa magumu kwa mwanamke ambaye amepandikizwa kifaa hiki," analalamika.

Mamlaka ya afya inayohusika na Hospitali ya Mama na Mtoto ya Brasília ambako Kelli aliwekewa Essure aliiambia BBC News Brasil kwamba wakati wa kuingizwa, kifaa cha Essure kilikuwa kimeidhinishwa na wakala wa udhibiti wa afya wa Brazili na tayari kilikuwa kinatumika duniani kote.

Idara hiyo pia ilisema kuwa wagonjwa ambao walikuwa na kifaa cha Essure kilichopandikizwa wanafuatiliwa katika mtandao wa afya ya umma.

Mwongozo maalum uliundwa kwa wataalamu wa afya katika eneo hilo kufuatilia wagonjwa hawa, ambao wana haki ya kuondolewa kizazi ikiwa wanataka.

Watengenezaji wa Essure, Bayer pia walitetea bidhaa yake wakisema ni salama.

"Usalama wa Essure unaungwa mkono na kundi kubwa la tafiti za kisayansi," Bayer aliiambia BBC News Brasil katika taarifa yake.

"Takwimu hizi ni pamoja na matokeo ya tafiti 10 za kimatibabu na zaidi ya tafiti 70 za uchunguzi wa ulimwengu halisi zilizofanywa na kampuni na watafiti huru katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, zikihusisha zaidi ya wanawake 270,000," kampuni hiyo ilisema.

Shely Frazão, 40, alifanyiwa upasuaji wa kuondoa kizazi kabisa, ambao ulijumuisha kuondolewa kwa tumbo la uzazi, mlango wa uzazi, mirija ya uzazi, na kutoa kifaa cha Essure mapema mwaka wa 2023.

"Ilikuwa ni upasuaji wa tumbo usio wa kawaida sawa na upasuaji mwingine. Wakati wa kupona kwangu, nilianza kutokewa na mistari ya makovu ya kidonda inayojitengeneza ndani ya tumbo ambayo 'inashikamana' viungo na tishu pamoja ambavyo vilisababisha maumivu makali. Ilinibidi kufanyiwa upasuaji mwingine," anasema.

Liliane alikuwa karibu kufanyiwa utaratibu uleule kutoa Essure mwilini, lakini aligundua kwamna ana kidonda cha daraja la tatu kwenye mfuko wa uzazi ambacho kingehitaji kutibiwa kwanza.

Kelli alitaka kuondoa kifaa hicho bila kupoteza tumbo la uzazi, lakini akakabiliwa na matatizo zaidi na ilimbidi afanyiwe upasuaji wa kuondoa tumbo la uzazi kabisa.

Wanawake wote watatu wanakusudia kushtaki kampuni ya Bayer, kufuatia kesi kama hizo huko Marekani, Uingereza na Australia.

Mnamo Agosti 2020, Bayer ililipa $1.6 bilioni kutatua zaidi ya kesi 39,000 za kifaa Essure nchini Marekani.

Nchini Uingereza, wanawake mia mbili ambao wanadai waliachwa na maumivu baada ya kuwekewa kifaa Essure, wanajiandaa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni ya Bayer.

Na huko Australia, zaidi ya wanawake elfu moja walifungua kesi mwaka huu, wakidai kwamba kifaa hicho kilisababisha maumivu, kuteseka, na kuvuja damu nyingi.

Katika taarifa yake kwa BBC News Brasil, Bayer ilitetea bidhaa yake na kusema kuwa makubaliano ya kisheria nchini Marekani yaliakisi uamuzi wa kibiashara pekee.

"Katika kesi zilizotatuliwa nchini Marekani, hakukuwa na kukiri kosa, mapungufu yoyote, au kuwajibika kwa upande wa Bayer," Bayer alisema.