Kukimbia na ulemavu wa macho kumebadili maisha yangu baada ya kukanyaga bomu Afghanistan

Chanzo cha picha, Wali Noori
Wali Noori alikuwa akifanya kazi ya ukalimani wa Jeshi la Uingereza nchini Afghanistan mwaka 2009 alipokanyaga bomu.
Mlipuko huo ulimfanya kuwa mlemavu wa macho akiwa na umri wa miaka 20.
Alipokuwa mdogo, alipenda kukimbia katika milima ya Kabul, lakini baada ya tukio hilo alifikiri hataweza tena kukimbia.
Kwa maneno yake mwenyewe, anaelezea jinsi kuhamia Uingereza kulivyobadilisha maishayake.
Kujiunga na jeshi

Chanzo cha picha, Wali Noori
Nilikulia Kabul, nilikuwa bondia mzuri sana na nilikuwa nakimbia ili kujiweka sawa. Nilimaliza masomo yangu na nilitaka kwenda chuo kikuu, lakini familia yangu ilikuwa maskini sana na nilitaka kuwasaidia.
Walikuwa masikini, baba yangu hakuwa na kazi na nina ndugu wa kike watano na wakiume wanne.
Nilipokuwa na umri wa miaka 18 nilijiunga na Jeshi la Uingereza nikiwa mfasiri na mshauri wa kitamaduni.
Nilisoma Kiingereza shuleni na nilikuwa nakijua vizuri. Kazi yangu ilikuwa ni kulisaidia Jeshi la Uingereza, vikosi vya Afghanistan na raia wa ndani katika kuwasiliana.
Niliulizwa ikiwa nitakwenda Mkoa wa Helmand, nikasema ndiyo, licha ya kujua hatari zilizoko. Watu walikuwa wakifa kila siku huko lakini sikuogopa.
Nilikaa Helmand kwa miaka miwili, hadi siku nilipokanyaga bomu nikiwa kwenye doria. Nilirushwa hewani na kurudi chini. Uso wangu wote ulikuwa umejaa vipande vya bomu na nilipoteza meno yangu yote 28.
Nilikuwa sipumui lakini nilipeleka mkono kwenye koo langu na kuchomoa kipande kimoja. Sikuweza kuona chochote. Nilisafirishwa kwa helikopta, na kukaa wiki mbili bila fahamu katika hospitali ya jeshi huko Kabul.
'Nilidhani maisha yangu yamekwisha'

Chanzo cha picha, Wali Noori
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Madaktari hawakudhani ningepona. Nilipozinduka sikuweza kuzungumza, ikabidi niwaandikie jina langu ili wampigie simu rafiki yangu ambaye aliiambia familia yangu kilichotokea.
Mama na baba walipokuja kwa mara ya kwanza, ilikuwa wakati mgumu sana kwao. Nilifanikiwa kukaa kitako ili hali isionekane ni mbaya sana, nikajaribu kutabasamu kwa ajili yao, lakini bado sikuweza kuzungumza.
Nilipelekwa katika Hospitali ya Bagram, ambapo Wamarekani walitibu majeraha yangu ya uso na mivunjiko. Nilikuwa nikipumua kupitia mrija kutoka shingoni mwangu.
Nilikaa huko kwa mwezi mmoja kabla ya kwenda kwenye hospitali za India na Pakistani ili kuona kama zingeweza kuokoa macho yangu, lakini haikuwezekana.
Nilikuwa napenda kukimbia lakini niliona siku zangu za kukimbia zimeisha. Nilikuwa kapera na nikarudi kuishi na familia yangu huko Afghanistan.
Mwaka 2012, nilifunga ndoa iliyopangwa. Tangu siku hiyo mke wangu amekuwa msaidizi wangu mkubwa.
Aliweka kando fimbo yangu nyeupe na akasema "Mimi ni fimbo yako." Ni mkarimu sana na kila ninapohuzunika huniambia "usihuzunike, niko hapa." Kwa sasa tuna watoto watatu.
Kukutana na Prince Harry

Chanzo cha picha, Getty Images
Sikuweza kufanya kazi nilipokuwa nikiishi Afghanistan, ingawa nilitaka. Jeshi la Uingereza lilinipa mshahara wa mwaka mmoja lakini nilikuwa nikipata tabu hasa kwa vile ni mlemavu.
Mwaka 2014, niliambiwa na Serikali ya Uingereza kwamba nastahili kuja Uingereza na familia yangu. Ilichukua miaka miwili kukamilisha hilo na kisha tukahamia Colchester.
Napapenda sana hapa. Ni mahali pazuri na nimepata marafiki wema, hasa katika klabu yangu ya mbio, Colchester Harriers. Na tuko salama.
Niligundua ninaweza kuanza kukimbia tena, kwa sababu wana wakimbiaji elekezi, na hii imenirudishia uhuru wangu na afya yangu ya akili.
Nilikuwa nikipata maumivu makali ya kichwa kutokana na majeraha yangu lakini sasa natoka na kwenda kukimbia na maumivu ya kichwa yamekata.
Nilingoja kwa miaka mitano kabla ya kuchaguliwa katika mashindano ya Invictus na nilifurahi kuiwakilisha Uingereza mwezi Septemba uliopita.
Nilishinda medali nne za dhahabu, katika mbio za mita 100, 200, 400 na 1500. Nilikutana na Prince Harry na Meghan na walikuwa wakarimu na wenye upendo.
Harry alinishika mkono, sikumjua ni nani. Nikauliza "huyu ni nani?" akasema "mimi ni Prince Harry" tukacheka na kuzungumza. Ulikuwa ni wakati wa furaha katika maisha yangu.
'Siwezi kamwe kubweteka'

Chanzo cha picha, Getty Images
Sasa nimeshinda medali 21 za kukimbia na tatu za kuogelea. Siku zote nataka kusonga mbele katika maisha yangu na sitaangalia nyuma.
Ndoto yangu ni kushindana kwenye michezo ya Olimpiki ya Walemavu (Paralympic). Nimekidhi vigezo kwa jinsi ninavyo kimbia haraka, lakini mwaka huu nilichelewa kutuma maombi. Ila nitafika huko siku moja.
Ningependa pia kukimbia mbio kuu sita za marathoni, baada ya kukimbia London 2019.
Nimeadika kitabu kuhusu maisha yangu na kitachapishwa tarehe 12 Septemba, itakuwa sawa na miaka 15 tangu kupoteza macho yangu.
Ninakwenda shuleni na vyuoni na katika vikundi vya wanajeshi wa zamani ili kutoa hadithi yangu na hivi karibuni nilizungumza na maveterani ambao waliojeruhiwa nchini Ukraine. Nikipata pesa katika hotuba hizi nazirudisha Afghanistan kusaidia wajane na mayatima.

Chanzo cha picha, Wali Noori
Sijuti kamwe kujiandikisha kufanya kazi na Jeshi la Uingereza na kile kilichonipata. Maisha yalikuwa magumu sana kwangu kabla ya hapo, lakini maisha yananiendea vyema sasa.
Sitasalimu amri kwa kukosa kuona. Nataka kuendelea kuhamasisha watu na kuonyesha kuwa ulemavu sio lazima ukuzuie kufikia mambo makubwa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












