Ujumbe uliohifadhiwa kwenye chupa kwa miaka 135 wapatikana kwenye sakafu ya mbao

Fundi mmoja hakuamini macho yake alipotoboa shimo kwenye sakafu ya mbao katika nyumba moja huko Edinburgh na kukuta chupa iliyokuwa na ujumbe wa miaka 135.

Peter Allan, 50, alipotoboa tu sakafu ndipo ahali ambapo chupa ya whisky ilikuwa imeachwa ikiwa na karatasi ndani yenye ujumbe huo.

Alishuka chini haraka kwenda kumwambia mwenye nyumba eneo la Morningside. Eilidh Stimpson alilazimika kuivunja chupa ili kusoma karatasi (barua) hiyo - na akasema watoto wake wawili walifurahishwa na kupatikana kwa chupa hiyo yenye ujumbe.

Bw Allan aliiambia BBC Scotland kuwa haamini kabisa bahati yake ya kutoboa sakafu na kukutana moja kwa moja na chupa.

"Chumba ni futi 10 kwa futi 15 na nimekata kabisa sakafu kuzunguka eneo la chupa bila kujua kwamba kulikuwa na chupa. Siwezi kuamini kabisa," alisema.

"Nilikuwa nikisogeza bomba na kukata tundu bila mpangilio kutafuta bomba na hapo ndipo nilipotoboa, sijui nini kilitokea. "Niliipeleka kwa yule mwanamke pale chini na kusema 'Angalia kile nimepata chini ya sakafu yako'."

Bw Allan, mmiliki wa kampuni ya WF Wightman Plumbing, alisema iligunduliwa chini ya kile ambacho kingekuwa chumba cha mjakazi wakati nyumba hiyo ilipojengwa kwa mara ya kwanza.

Sasa mama wa watoto wawili Eilidh Stimpson, daktari wa Edinburgh, anaishi huko na mume wake. Aliamua kungoja hadi watoto wake wa miaka minane na 10 warudi nyumbani kutoka shuleni kabla ya kujaribu kuitoa barua kutoka kwenye chupa.

Aliiambia BBC Scotland: "Nilipowachukua niliwaambia nina jambo la kufurahisha sana la kuwaambia. "Walikuwa na makisio machache zaidi na kisha nikawaambia kuna ujumbe kwenye chupa umepatikana nyumbani kwetu na walifurahi sana walijua labda ni mali (fedha)."

Walipofika nyumbani walijaribu sana kuitoa ile karatasi kwa kutumia vifaa mbalimbali, lakini ilianza kupasuka kidogo. Kwa hivyo alichukua nyundo na kuvunja chupa. Alisema: "Sote tulikuwa tukisongamana huku tukielekezea tochi zetu kujaribu kuisoma, ilisisimua sana."

Barua hiyo ilitiwa saini na kuandikwa tarehe na wafanyakazi wawili wa kiume na ilisomeka: "James Ritchie na John Grieve waliweka sakafu hii, lakini hawakunywa whisky. Oktoba 6, 1887. "Yeyote anayepata chupa hii anaweza kufikiria namna vumbi letu linavuma barabarani."

Utunzaji wa ujumbe

"Ninajisikia vibaya sana kuivunja chupa yenye umri wa miaka 135 lakini ilikuwa njia pekee ya kuufikia ujumbe. Nimeweka vipande vyote vya chupa kwenye beseni la Tupperware."

Tangu kupatikana kwa chupa siku ya Jumatatu rafiki wa familia aliangalia sensa ya 1881 na akapata majina ya wanaume wanaoishi maili chache tu katika eneo la Newington la Edinburgh.

Msimamizi katika Maktaba ya Kitaifa ya Scotland tangu wakati huo amewataka familia hiyo kwamba wahifadhi karatasi hiyo kwenye mfuko usio na kemikali.

Eilidh alisema: "Nimeagiza mifuko kuhifadhi kwa sababu ni jambo la kufurahisha na la kupendeza kuwa nalo."

Alisema wangeweza weka chupa, pamoja na karatasi mpya kutoka kwa familia pamoja na maandishi yaliyopatikana, na kurudisha kwenye shimo la sakafu ilipopatikana kabla ya kufunikwa tena.

"Fikiria ilikuwa pale wakati huo wote na inaweza kuwa huko milele ni ajabu. Sio tu kutoka miaka ya 70 au kitu kama hicho, ni cha zamani sana, na ni baridi sana', alisema.