Mauaji ya wanawake Kenya: Kwa nini wanaume wanashindwa kukemea dhulma dhidi ya wanawake?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Wahiga Mwaura
- Nafasi, BBC Focus on Africa TV
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Saa chache kabla ya maandamano ya kitaifa nchini Kenya kupinga kuongezeka kwa visa vya mauaji ya wanawake na unyanyasaji mwingine dhidi ya wanawake - video ilitumwa kwenye mitandao ya kijamii:
Katika eneo moja katika mji mkuu, Nairobi, baadhi ya wanawake vijana walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya maandamano mwishoni mwa wiki iliyopita, wanaume wawili walirekodiwa wakibisha haja ya maandamano kama hayo.
"Wanaume wameteseka kwa sababu ya wanawake," mmoja wao analalamika na kuendelea kusema, “wanawake hutumia tu wanaume kwa pesa zao.”
Wakati majadiliano makali yakiendelea, mwenzake anaingia na wote wawili wanaielekea kamera na kupiga kelele kuwaambia wanawake: "Tutawaua."
Kipande hiki kilisambazwa na mwanaharakati maarufu wa Kenya Boniface Mwangi pamoja na maneno haya: "Kama mwanaume na baba, wanaume hawa hawazungumzi kwa niaba ya wanaume ninaowajua."
"Sisi kama wanaume wa Kenya tunapaswa kuzungumza kwa ujasiri, na kwa sauti kubwa," alisema kuhusu mauaji ya wanawake, wanaouwawa kwa sababu ya jinsia yao.
Kama anavyobainisha, ni ni kweli wanaume wachache sana nchini Kenya ndio wanajitokeza waziwazi kupinga mitazamo ya chuki.
Kauli yake inaungwa mkono na Felix Kiprono, mkuu wa masuala ya habari katika kampuni ya uchambuzi na uwasilishaji wa data ya Odipo Dev.
Hivi karibuni walichapisha ripoti kuhusu ongezeko la kutisha la mauaji ya wanawake nchini Kenya - nchi hiyo imekumbwa na takribani mauaji 10 ya wanawake yaliyoripotiwa katika mwezi wa kwanza wa mwaka pekee.
Tukio moja la kutisha lilihusisha mwanamke ambaye mabaki yake yalipatikana yakiwa kwenye mfuko wa plastiki katika nyumba ya kukodisha kwa muda mfupi.
Ripoti hiyo inayoitwa ‘Silencing Women, inalenga kutoa mwanga juu ya hali halisi ya maisha ya wanawake yalivyo hatarini. Ikitoa taarifa muhimu ya lawama dhidi ya waathiriwa, kesi kutoripotiwa na kuhamasisha hatua za maana."
Kuhamasisha Chuki

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kiprono ameshtushwa na matokeo ya utafiti huo, haswa kwenye mitandao ya kijamii ambapo inaeleza uwepo wa majukwaa ya mtandaoni ya kijamii yanayohamasisha uanaume mbaya na kupinga ufemenia nchini Kenya.
Aliiambia BBC, kuhamasishana huko ni kwenye majukwaa yote: "Sio tu kwenye Twitter bali hata kwenye TikTok, ambayo kwa kawaida hujulikana kama eneo salama."
Kwa kuwa ripoti hiyo sasa iko hadharani, yeye na timu yake wamekuwa wakipata maombi mengi ya mahojiano ya vyombo vya habari.
“Inavyoonekana, ni vigumu kupata wanaume kukubali kuzungumzia jambo hili hadharani,” alisema.
Pia inaonekana wanaume wana mwelekeo mdogo katika kushiriki mijadala mtandaoni kuhusu masuala ambayo ripoti inaangazia.
"Tuligundua, haswa kwenye Instagram na TikTok, takribani 90% ya watu ambao walikuwa wakishiriki ni wanawake," anasema Kiprono.
"Inaonekana kuna tofauti kubwa katika mitazamo ya wanaume dhidi ya wanawake kuhusu unyanyasaji wa kijinsia kwa ujumla."
Mwanaume mmoja ambaye amechagua kujieleza ni DJ wa Kenya, mtengeneza maudhui ya mtandaoni na mtangazaji wa TV, Moses Mathenge, maarufu kama "DJ Moz."
Wiki mbili zilizopita, alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kulaani mauaji ya wanawake, na kuchapisha video ndefu kwenye majukwaa yake ya mitandao ya kijamii.
"Tumepoteza wanawake wengi (wake, mama, binti, dada, marafiki, watoto) kwa kitendo hiki cha kutisha cha ukatili."
DJ Moz aliamua kwenda mbali zaidi na kuchunguza takwimu za kimataifa kuhusu mauaji ya wanawake - na alichokipata kilimshtua.
"Unajua jambo la ajabu ni kwamba Afrika ina idadi kubwa zaidi ya kesi za mauaji ya wanawake duniani. Hayo sio mambo ambayo tunapaswa kujivunia kama Waafrika," alisema.
Kulingana na UN Women, kupitia ripoti yao ya 2022, inaonyesha "Afrika ina idadi kubwa zaidi ya kesi za mauaji kwa wapenzi wa kike na mauaji yanayohusiana na familia na wastani wa waathiriwa ni 20,000."
Eneo linalofuatia ni Asia, kesi "18,400, Amerika kesi 7,900, Ulaya kesi 2,300 na nchi za Oceania kesi 200."
DJ Moz, ambaye amefanya kazi katika mashirika ya kidini, anaamini ni wakati wa taasisi za kidini kujitokeza na kupiga vita chuki dhidi ya wanawake katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi.
"Tunahitaji kuzungumza, kwa sababu wakati mwingine kanisani, tunawaambia wanawake, wabaki tu kwenye ndoa zao [ingawa] mwanamke huyu anapigwa na mumewe.
"Kisha anapouwawa, tunaanza kuzungumza juu ya tulivyojua suala hili lilikuwa linatokea."
Kiprono anaamini itachukua muda mrefu kuondoa chuki za wanaume katika jamii ya Wakenya. Mitazamo ya mfumo dume, inaathiri wanaume sana, na hata hatutambui ni kiasi gani unatuathiri.
Anasema kila wakati mwanamke anapotaka kuondoka nyumbani kwake, anapaswa kuzingatia njia za kuhakikisha anasalia salama - popote anapoelekea.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












