Waziri Mkuu wa India azindua hekalu kuu la mungu lililochukua nafasi ya msikiti

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amezindua hekalu kuu la mungu wa Kihindu Ram katika mji wa Ayodhya.
Alisema ni hatua ya kutangaza "zama mpya" kwa India - hekalu hilo litachukua nafasi ya msikiti wa Karne ya 16 uliobomolewa na makundi ya Wahindu mwaka 1992, na kusababisha ghasia ambapo karibu watu 2,000 walifariki.
Wachezaji nyota wa filamu na wacheza kriketi walikuwa miongoni mwa wageni katika hafla hiyo huko Ayodhya.
Lakini baadhi ya watu kutoka upinzani walisusia tukio hilo, wakisema Bw Modi alikuwa akitekeleza hilo kwa manufaa ya kisiasa.
Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika nchini India miezi michache ijayo na wapinzani wa Bw Modi wa kisiasa wanasema chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) kitatafuta kura kwa jina la hekalu hilo katika nchi ambayo asilimia 80 ya wakazi ni Wahindu.
Wakosoaji pia wameishutumu serikali kwa kutumia sherehe za kidini katika nchi ambayo - kulingana na katiba yake - haina dini.
Kwa Waislamu, walio wachache zaidi nchini India, tukio hilo lilizua hofu na kumbukumbu zenye uchungu, wanachama wa jumuiya ya Ayodhya waliambia BBC katika maandalizi ya sherehe za Jumatatu.
Televisheni zilionyesha Bw Modi akifanya matambiko ya kidini ndani ya hekalu pamoja na makasisi na Mohan Bhagwat, mkuu wa Rashtriya Swayamsevak Sangh (RSS) - kiongozi wa itikadi kali wa vyama vya kitaifa vya Kihindu.
"Tarehe ya leo itakuwa katika historia," Bw Modi alisema baada ya hafla hiyo. "Baada ya miaka mingi ya mapambano na kujitolea mhanga, Bwana Ram amewasili [nyumbani]. Ninataka kumpongeza kila raia wa nchi kwa tukio hili la kihistoria."
Hekalu hilo limejengwa kwa gharama ya $217m (£170m), lililofadhiliwa na michango ya kibinafsi. Ghorofa ya chini tu ndiyo iliyofunguliwa - iliyobaki inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka. Kazi ya ujenzi ni sehemu ya urekebishaji wa jiji, unaokadiriwa kugharimu zaidi ya $3bn.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jengo la hekalu la Ram huko Ayodhya linatimiza ahadi ya utaifa ya miongo mingi. Wahindu wengi wanaamini kuwa msikiti wa Babri ulijengwa na wavamizi Waislamu kwenye magofu ya hekalu ambalo mungu wa Kihindu alizaliwa.
Harakati za kujenga hekalu zilisaidia kukuza chama cha BJP katika umaarufu wa kisiasa katika miaka ya 1990.
Kulikuwa na sherehe huku makumi ya maelfu ya waumini wa Kihindu waliokuwa wakiimba wakipeperusha bendera na kupiga ngoma - helikopta za kijeshi zikimimina petali za maua kwenye hekalu.
Kulikuwa na bendera za zafarani zenye picha za barabara za Lord Ram pamoja na mabango yenye nyuso za Bw Modi na Waziri Mkuu wa Uttar Pradesh Yogi Adityanath.
Baadhi ya watu mashuhuri wakubwa wa India, akiwemo nyota wa Bollywood Amitabh Bachchan na mwanakriketi Sachin Tendulkar, walihudhuria.
Katika miji mingine mingi ya kaskazini Wahindu waliwasha taa na bendera za zafarani zilizobeba picha za Ram zikipepea juu ya paa za nyumba, ikiwa ni pamoja na katika vitongoji kadhaa vya Delhi.
Tukio hilo lilionekana moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii huku skrini kubwa zikisambaza picha kutoka kwa Ayodhya hadi viwanja vya mijini na vitongoji vya makazi.
Vituo kadhaa vya runinga vya ndani ya nchi vilijikita kando ya mto Saryu, kijito cha Ganges, nyuma kidogo ya hekalu, na kupeperusha matangazo ya moja kwa moja.
Mnamo 2019, Mahakama ya Juu Zaidi iliwapa Wahindu ardhi hiyo iliyozozaniwa baada ya mabishano ya muda mrefu ya kisheria kufuatia kubomolewa kwa msikiti huo. Waislamu walipewa kiwanja nje ya mji kwa ajili ya msikiti lakini bado hawajajenga.
Mwanachama mmoja wa jumuiya ambayo BBC ilizungumza naye huko Ayodhya kabla ya uzinduzi wa Jumatatu alikubali kwamba Wahindu wana haki ya kujenga hekalu baada ya Mahakama ya Juu Zaidi kuwapa eneo hilo.
"Hatukukubali tu uamuzi huo , lakini hatuna cha kufanya," alisema. Mtu mwingine alisema anafurahi Wahindu wanajenga hekalu - "lakini pia tunasikitika kwa sababu lilijengwa baada ya kuharibu msikiti".
Hekalu hilo jipya la orofa tatu - lililotengenezwa kwa mchanga wa waridi - linaenea katika ekari 7.2 katika eneo la ekari 70.
Sanamu ya inchi 51 (futi 4.25) ya mungu huyo, iliyowekwa maalum kwa ajili ya hekalu, ilizinduliwa wiki iliyopita. Sanamu hiyo imewekwa juu ya msingi wa marumaru katika eneo linalochukuliwa kuwa patakatifu.
Jinsi eneo hilo lilivyobadilika kutoka msikiti wa Babri 1989 hadi Hekalu la Ram 2024

Maelfu ya polisi walitumwa kwa hafla hiyo ya Jumatatu, licha ya Bw Modi kuwataka mahujaji kutofika na kutazama hafla hiyo kwenye runinga. Katika majimbo yanayotawaliwa na BJP likizo ya siku nzima au nusu ilitangazwa huku shule, vyuo na soko la hisa vikifungwa.
Lakini baadhi walikosoa hatua hiyo wakisema kwamba kwa vile hekalu lilikuwa bado halijakamilika, ni kinyume cha Uhindu kufanya matambiko huko, na viongozi wengi wa upinzani waliamua kutojihusisha na tukio hilo.
Mamlaka inasema wanatarajia zaidi ya wageni 150,000 kwa siku mara tu hekalu la Ayodhya litakapokamilika.
Ili kushughulikia haraka idadi kubwa ya watu inayotarajiwa eneo hilo, hoteli mpya zinajengwa na zilizopo zimekarabatiwa kama sehemu ya mabadiliko makubwa na katika wiki za hivi karibuni, uwanja mpya wa ndege na kituo cha reli vimefunguliwa.
Maafisa wanasema wanajenga "mji wa hadhi ya kimataifa ambapo watu huja kama mahujaji na watalii", lakini watu wengi wa eneo hilo wameambia BBC kwamba nyumba zao, maduka na "miundo ya kidini" imebomolewa kabisa au kwa kiasi fulani ili kupanua barabara na kuanzishwa kwa vituo vingine.
Imefasiriwa na Asha Juma














