Utafiti: Kwa nini nusu ya watu wote duniani kuwa wanene?

Muda wa kusoma: Dakika 3

Zaidi ya nusu ya watu wazima wote na theluthi moja ya watoto, vijana, duniani wanatarajiwa kuwa na uzito mkubwa au unene kupita kiasi ifikapo mwaka 2050.

Matokeo haya yanatokana na utafiti mpya wa takwimu za kimataifa uliochapishwa katika jarida la The Lancet, likihusisha zaidi ya nchi 200.

Watafiti wanatahadharisha kwamba viwango vya unene vinatarajiwa kuongezeka kwa kasi kubwa katika kipindi kilichosalia cha muongo huu, hasa katika nchi za kipato cha chini.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kwamba ikiwa serikali zitachukua hatua za dharura sasa, bado kuna muda wa kuzuia kile wanachokiita "janga kubwa".

Kwa mwaka 2021, karibu nusu ya idadi ya watu wazima duniani—milioni moja ya wanaume na milioni 1.11 ya wanawake wenye umri wa miaka 25 au zaidi—walikuwa na uzito mkubwa au unene kupita kiasi.

Idadi ya wanaume na wanawake wanaoishi na hali hii imeongezeka mara mbili tangu mwaka 1990.

Ikiwa mwelekeo utaendelea hivi, viwango vya watu wazima wenye uzito mkubwa na unene kupita kiasi duniani vinatarajiwa kufikia takriban 57.4% kwa wanaume na 60.3% kwa wanawake ifikapo mwaka 2050.

Kwa idadi halisi, China (milioni 627), India (milioni 450) na Marekani (milioni 214) zitakuwa nchi zenye idadi kubwa ya watu wenye uzito mkubwa au unene kupita kiasi ifikapo mwaka 2050.

Hata hivyo, ukuaji wa idadi ya watu unamaanisha kwamba wataalamu wanatarajia idadi katika Afrika ya Kusini mwa Sahara itaongezeka kwa zaidi ya 250% na kufikia milioni 522.

Nigeria, hasa, inajitokeza, na idadi inayotarajiwa inakadiriwa kuongezeka zaidi ya mara tatu—kutoka milioni 36.6 mwaka 2021 hadi milioni 141 mwaka 2050.

Hii itaifanya iwe nchi ya nne yenye idadi kubwa ya watu wazima wenye uzito mkubwa au unene kupita kiasi.

Waandishi wanatambua kuwa utafiti huu hauzingatii athari za dawa mpya za kupunguza uzito, ambazo zinaweza kuwa na mchango mkubwa katika siku zijazo.

Wataalamu wanasema kwamba kama serikali zitachukua hatua za dharura sasa, bado kuna muda wa kuzuia kile kinachoweza kuwa janga kwa mifumo ya afya inayohitaji msaada.

Utafiti uliongozwa na Prof. Emmanuela Gakidou kutoka Taasisi ya (IHME) ya Chuo Kikuu cha Washington nchini Marekani.

Alisema: "[Serikali] zinaweza kutumia makadirio maalum ya kila nchi, wakati, na kasi ya mabadiliko ya sasa na yanayotarajiwa ili kutambua makundi muhimu yanayoishi na mzigo mkubwa wa unene ambayo yanahitaji usaidizi wa kimatibabu kwa haraka, na wale ambao bado ni wazito na wanapaswa kulengwa hasa na mikakati ya kuzuia."

Aliongeza kusema, "Suala la uzito mkubwa na unene ni janga kubwa la kimataifa na kushindwa kwa kijamii kwa kiwango kikubwa."

Kuna ongezeko la viwango vya unene kupita kiasi linalotokea sasa hivi, hasa miongoni mwa vijana.

Viwango vya unene kupita kiasi kwa watoto na vijana wadogo (kutoka 8.8% hadi 18.1%) na kwa vijana wale walio chini ya umri wa miaka 25 - kutoka 9.9% hadi 20.3%) vimeongezeka mara mbili zaidi kati ya mwaka 1990 na 2021.

Hata hivyo, ifikapo mwaka 2050, mmoja kati ya vijana watatu atakumbwa na tatizo hili.

Mwandishi mkuu wa ripoti hiyo, Dkt. Jessica Kerr kutoka Taasisi ya Utafiti ya Watoto ya Murdoch nchini Australia, anasema takwimu hizi zinawakilisha changamoto halisi kwa mifumo ya afya katika miaka ijayo.

"Lakini kama tutachukua hatua sasa, kuzuia mabadiliko kamili kudhibiti unene kwa watoto na vijana bado inawezekana," alisema.

"Makadirio yetu yanaonyesha watoto na vijana katika sehemu nyingi za Ulaya na Asia Kusini wanaishi na uzito mkubwa ambao wanapaswa kulengwa na mikakati ya kuzuia unene."

"Pia tumegundua idadi kubwa ya watu, hasa wasichana vijana, Amerika Kaskazini, Australia, Oceania, Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, na Amerika ya Kusini, ambao wanatarajiwa kugeuka kuwa na unene mkubwa na wanahitaji uingiliaji wa haraka, wa kijumla na kimatibabu."

"Hii ni muhimu kuepuka unene kutoka kizazi kimoja hadi kingine na kuzuia wimbi la magonjwa makubwa ya kiafya na gharama kubwa za kifedha na kijamii kwa vizazi vijavyo."