Nyangumi wa Urusi alivyokimbia mafunzo ya kijeshi

Muda wa kusoma: Dakika 5

Fumbo kuhusu nyangumi aina ya beluga, aliyeonekana kwenye ufuo wa Norway akiwa na kibandiko cha utambulisho, huenda sasa limefumbuliwa.

Nyangumi huyo mweupe, ambaye wenyeji walimpa jina la Hvaldimir, aligonga vichwa vya habari miaka mitano iliyopita, baada ya kuwepo uvumi kwamba alikuwa ni jasusi wa Urusi.

Sasa mtaalamu wa mamalia hao anaamini nyangumi huyo kweli alikuwa wa jeshi la Urusi na alitoroka katika kambi ya wanamaji huko Arctic Circle.

Ingawa Dk Olga Shpak haamini kwamba alikuwa jasusi. Anaamini beluga alikuwa akifunzwa kulinda kambi hiyo na akakimbia kwa sababu ni muhuni.

Urusi imekataa kuthibitisha au kukataa kwamba nyangumi huyo alifunzwa na jeshi lake.

Dk Shpak, alifanya kazi nchini Urusi akitafiti mamalia wa baharini kuanzia miaka ya 1990 hadi aliporejea nchini kwao Ukraine mwaka 2022.

Kauli ya Dk Shpak, inategemea mazungumzo na marafiki na wafanyakazi wenzake wa zamani nchini Urusi.

Mwanzo wa kuonekana

Nyangumi huyo wa ajabu alijuulikana kwa umma miaka mitano iliyopita alipokaribia wavuvi katika pwani ya kaskazini ya Norway.

"Nyangumi alianza kusugua mashua," anasema Joar Hesten, mmoja wa wavuvi. “Najua kuhusu wanyama walio katika dhiki ambao hujua kwamba wanahitaji msaada kutoka kwa wanadamu. Nilijua nyangumi huyu ana akili.”

Kuonekana kwake halikuwa jambo la kawaida kwa sababu beluga alionekana ni wa kufugwa na nyangumi wa aina hiyo hawaonekani sana kusini. Pia alikuwa na kamba amevalishwa, ambayo inawez kutumika kufungia kamera, na kuna maneno kwenye kamba hiyo yenye kutafsirika, "Kifaa cha St Petersburg."

Bw Hesten alisaidia kuondoa kamba kutoka kwa nyangumi huyo, ambaye baadaye aliogelea hadi kwenye bandari ya karibu ya Hammerfest, ambako aliishi kwa miezi kadhaa.

Alionekana kutoweza kukamata samaki hai ili kula, alivutia wageni kwa kugusa kamera zao.

"Ilikuwa dhahiri kwamba nyangumi huyu alifunzwa kugusa kitu chochote kwa pua yake ambacho kilionekana kama shabaha kwa sababu alikuwa akifanya hivyo kila wakati," anasema Eve Jourdain, mtafiti kutoka Norway Orca Survey.

"Lakini hatujui alikuwa katika kituo cha aina gani cha mafunzo, kwa hivyo hatujui alifunzwa kwa ajili ya jambo gani."

Hadithi yake ilivutia na Norway ikafanya mipango ili beluga afuatiliwe na kulishwa. Alipewa jina la - Hvaldimir - hval ikiwa na maana ya nyangumi kwa Ki- Norwegian, na dimir ni jina la Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Taarifa kutoka Urusi

Dk Shpak hakutaka kutaja vyanzo vyake nchini Urusi kwa usalama wao lakini alisema aliambiwa kwamba beluga alipoonekana nchini Norway, Urusi ilitambua mara moja kuwa mmoja wa mamalia wao hayupo.

"Kupitia msururu wa madaktari wa mifugo na wakufunzi – taarifa ilitolewa kwamba beluga anayeitwa Andruha huko, hayupo," anasema.

Kulingana na Dk Shpak, Andruha/Hvaldimir alikamatwa kwa mara ya kwanza mwaka 2013 katika Bahari ya Okhotsk, Mashariki ya Mbali ya Urusi.

Mwaka mmoja baadaye alihamishwa kutoka kituo cha pomboo huko St Petersburg hadi kituo cha mafunzo ya kijeshi huko Arctic, Urusi, ambapo wakufunzi wake waliendelea kuwasiliana naye.

"Naamini walipoanza kumpa mafunzo kwenye maji ya wazi, wakimwamini mnyama huyo hatotoroka, lakini alitoroka," anasema.

"Nilichosikia kutoka kwa watu katika kituo cha pomboo ambao walikuwa naye ni kwamba Andruha alikuwa mwerevu, kwa hivyo ni chaguo nzuri kufunzwa. Lakini wakati huo huo, alikuwa kama muhuni - kwa hivyo hawakushangaa kwamba alikataa kufuata boti na kutoweka."

Eneo la Mafunzo

Picha za satelaiti kutoka katika kituo cha jeshi la wanamaji la Urusi huko Murmansk zinaonyesha nyumba ya zamani ya Hvaldimir/Andruha. Kizimba kinachoonekana waziwazi ndani ya maji na nyangumi weupe ndani.

Thomas Nilsen, kutoka gazeti la mtandaoni la Norway, The Barents Observer, anasema: “Mahali walipo nyangumi hao ni karibu sana na nyambizi na vyombo vilivyopo juu za bahari, vinadhihirisha nyangumi hao ni sehemu ya ulinzi.

Urusi, kwa upande wake, haijawahi kuzungumzia rasmi madai kwamba Hvaldimir/Andruha alifunzwa na jeshi lake. Lakini ina historia ndefu ya kutoa mafunzo kwa mamalia wa baharini kwa madhumuni ya kijeshi.

Mwaka 2019, kanali wa akiba wa Urusi, Viktor Baranets, alisema: "Ikiwa tulikuwa tukimtumia mnyama huyu kwa upelelezi, unafikiri kweli tungeambatanisha nambari ya simu na ujumbe 'Tafadhali piga nambari hii'?"

Kifo chake

Cha kusikitisha ni kwamba hadithi ya ajabu ya Hvaldimir/Andruha haina mwisho mwema.

Baada ya kujifunza kujilisha, alitumia miaka kadhaa kusafiri kusini kando ya pwani ya Norway na Mei 2023 alionekana kwenye pwani ya Sweden.

Septemba 1, 2024 mwili wake ulipatikana ukielea baharini, karibu na mji wa Risavika, kwenye pwani ya kusini-magharibi ya Norway.

Je! Urusi ilimuua? Licha ya baadhi ya makundi ya wanaharakati kusema kwamba nyangumi huyo alipigwa risasi, maelezo hayo yametupiliwa mbali na polisi wa Norway.

Wanasema hakukuwa na chochote cha kuashiria kwamba shughuli za kibinadamu zilisababisha kifo cha beluga moja kwa moja.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa Hvaldimir/Andruha alikufa baada ya ujiti kukwama mdomoni mwake.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi