Kiongozi wa upinzani dhidi ya Taliban: ‘Afghanistan ya leo ni tishio kubwa zaidi kwa dunia kuliko ilivyokuwa mwaka 2001’

    • Author, Daud Qarizadah
    • Nafasi, BBC Persian

"Afghanistan ya leo ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa dunia kuliko ilivyokuwa mwaka 2001." Hili ni onyo kali kutoka kwa mtoto wa kiongozi maarufu wa upinzani dhidi ya Taliban.

Ahmad Massoud ana umri wa miaka 33 tu lakini tayari anafuata nyayo za babake. Baba yake alikuwa kamanda mwandamizi Ahmad Shah Massoud, anayejulikana kama 'simba wa Panjshir', jimbo la kaskazini mwa Kabul ambako familia hiyo inatoka. Aliuawa na maafisa wa al-Qaeda siku mbili kabla ya mashambulizi yao ya 9/11 dhidi ya Marekani mwaka 2001.

Hii ilikuwa katika kipindi cha mwisho cha utawala wa Taliban wakati kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Afghanistan liliruhusu makundi mengine ya kijihadi kuishi katika ardhi yake.

Sasa, mtoto huyo anaogopa namna historia inavyojirudia.

'Mahali salama zaidi kwa magaidi'

Ahmad Massoud anasema nchi yake kwa mara nyingine imekuwa kimbilio salama kwa makumi ya makundi ya kigaidi, yakiwemo ISIS na al-Qaeda, yanayotaka kusambaza itikadi zao kali kila mahali duniani. Serikali ya Afghanistan inayoungwa mkono na nchi za Magharibi ilianguka mwezi Agosti mwaka jana kufuatia kuondolewa kwa wanajeshi wa kigeni.

Kundi la Taliban lilichukua tena madaraka baada ya zaidi ya miaka 20 ya kupambana na uasi dhidi yao. Katika mahojiano maalum na BBC, Ahmad Massoud anaonya ulimwengu dhidi ya kupuuza Afghanistan, akisema nchi yake inahitaji uangalizi wa haraka na utulivu wa kisiasa.

Anasema makundi ya kigaidi yangetumia msukosuko huo kujaribu kushambulia maslahi ya kigeni.

Baba yake marehemu, Ahmad Shah Massoud, alitoa onyo kama hilo siku chache kabla ya 9/11. Ahmad Massoud anasema onyo la baba yake halikuzingatiwa na dunia imeishi na matokeo yake tangu wakati huo. Bwana Massoud anaelezea hali ya Afghanistan kuwa mbaya zaidi kuliko wakati wa baba yake.

"Ninatumai dunia na hasa Ulaya inaelewa ukali wa vitisho kutoka Afghanistan na kuingilia kati kwa njia ya maana kusaidia kuanzisha serikali inayowajibika na halali nchini Afghanistan," alisema.

'Kulazimishwa kupigana'

Ahmad Massoud alipata mafunzo ya mwaka mmoja katika Chuo cha Kijeshi cha Kifalme Sandhurst, ambapo Uingereza inawafunza maafisa wake wa jeshi. Kisha akamaliza shahada ya masomo ya vita katika Chuo cha King's College London.

Kiongozi huyo kijana anasema mzozo katika nchi yake lazima utatuliwe kwa mazungumzo ya kisiasa badala ya vita. Hata hivyo, anasema Taliban walimwacha bila chaguo ila kupinga na kupigana na kile anachokiita "uhalifu dhidi ya ubinadamu" wa Taliban.

Kufuatia kurejea kwa Taliban madarakani mwezi Agosti mwaka jana, Ahmad Massoud alirejea katika mji aliozaliwa wa Panjshir na kuunda kundi la National Resistance Front.

Bwana Massoud sasa anaongoza zaidi ya wapiganaji 3,000 wenye silaha. Kwa muda wa miezi 11 iliyopita, vikosi vyake vimekuwa vikipigana na Taliban, hasa katika mabonde na milima ya Panjshir na wilaya jirani ya kimkakati ya Andarab katika jimbo la Baghlan.

Yeye na kundi lake wamepinga madai ya Taliban kwamba wameleta usalama kote Afghanistan.

Tofauti na mapambano ya baba yake dhidi ya Taliban mwishoni mwa miaka ya 1990, hakuna nchi hadi sasa imeidhinisha hadharani upinzani wa kijeshi wa Ahmad Massoud dhidi ya Taliban.

Mwezi uliopita, serikali ya Uingereza ilitoa taarifa ikisema: "Haiungi mkono mtu yeyote, ikiwa ni pamoja na raia wa Afghanistan, anayetaka kufikia mabadiliko ya kisiasa kupitia vurugu, au shughuli yoyote ya kuchochea ghasia kwa madhumuni ya kisiasa, nchini Afghanistan."

Taliban wenyewe walipokea vyema taarifa hiyo. Lakini Ahmad Massoud anasema "inatia shaka kimaadili". Anauliza ni vipi mataifa yenye nguvu duniani yanaweza kusema kuwa haikubaliki kupigana dhidi ya Taliban sasa wakati madola ya Magharibi yalipounga mkono kampeni ya kijeshi dhidi yao kwa miongo kadhaa.

Pia anasema watu wa Afghanistan wana haki ya kupigania haki na uhuru.

"Kimaadili, hiyo ni sababu tosha ya kuungwa mkono," anasema.

Silaha duni na uhaba wa pesa

Kiongozi huyo wa National Resistance Front anakubali kwamba vikosi vyake vina rasilimali chache kuliko Taliban. Lakini anasema ari ya hali ya juu na hamasa walio nayo zimeweka upinzani kuendelea.

"Tuko mwaka 2022. Kizazi kipya kinataka Afghanistan mpya ambapo wanaweza kuamua mustakabali wao," anasema.

Ahmad Massoud anatoa wito kwa mataifa yenye nguvu duniani, ikiwemo Uingereza, kusimama na watu wa Afghanistan na kuongeza shinikizo kwa Taliban kukubali suluhu la kisiasa.

Takriban mwaka mmoja tangu kundi la Taliban kuchukua mamlaka mjini Kabul, hakuna nchi iliyoitambua serikali yao. Lakini, nchi kadhaa za kikanda, kama vile Urusi, zimeonyesha kuwa ziko tayari kuwa na uhusiano wa kawaida na serikali ya Taliban.

Ahmad Massoud anaonya dhidi ya kuwatambua Taliban. Anasema nchi yoyote itakayoamua kufanya hivyo itawajibika kwa dhulma na ukatili wa Taliban. Anawashutumu Taliban kwa kufanya kampeni iliyoenea ya kuwakamata, kuwatesa na kuwaua raia kinyume cha sheria huko Panjshir, Andarab na maeneo mengine. Umoja wa Mataifa umeangazia mauaji haya pia.

Ahmad Massoud anasema asilimia 97 ya waliokamatwa na Taliban hawana uhusiano na chama chake cha National Resistance Front. Anasema Taliban wanafanya hivyo ili kuwatisha na kuwapa hofu kisaikolojia. Bw. Massoud aliomba msamaha kwa familia za wahathiriwa na kusema kuwa hangeweza kuwasaidia kutokana na rasilimali zake chache.

Wito wa mazungumzo

Anasema mazungumzo ya kisiasa ndiyo njia pekee ya kutatua mzozo huo.

Bwana Massoud amekutana mara kadhaa na viongozi wa Taliban, ikiwa ni pamoja na kukutana ana kwa ana na waziri wa mambo ya nje wa Taliban, Amir Khan Mottaqi, mjini Tehran miezi sita iliyopita.

Alisema mazungumzo hayo hayakwenda vizuri. Anawalaumu Taliban na kusema hawajafikia mahali ambapo wanaamini katika suluhu la kisiasa.

Hata hivyo, Bw Massoud anasema kuna dalili kwamba ngazi za chini za Taliban wanataka mchakato wa wazi zaidi na shirikishi. Anatumai uelewa huu utawafikia viongozi wakuu.

Lakini anajua anakabiliwa na vita vya muda mrefu vya upweke.

"Ulimwengu umewaacha watu wa Afghanistan. Imetuacha sisi wenyewe kupigana na ugaidi wa kimataifa."